Russia: Azimio la IAEA dhidi ya Iran ni la kipumbavu
Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika taasisi za kimataifa zenye makao yao mjini Vienna, Austria amelitaja azimio lililopasishwa hivi karibuni na Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA dhidi ya Iran kuwa ni la kipumbavu.
Mikhail Ulyanov alisema hayo jana Ijumaa, katika ujumbe wenye maneno makali alioutuma kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter na kuhoji: Je umepata habari mpya kutoka Iran? Sasa unaelewa ni kwa nini Russia ililipiga kura ya hapana, azimio la kipumbavu la Bodi ya Magavana ya IAEA dhidi ya Iran?
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Russia amefafanua kuwa, "kwa masikitiko, wenzetu Wamagharibi wameonyesha kuwa hawafahamu chochote kuhusu sehemu tulipo."
Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika taasisi za kimataifa zenye makao yao mjini Vienna amezihutubu nchi za Ulaya kwa kusema: Nyinyi ndio watu wa mwisho ambao mtazamo wao unaweza kuaminiwa na yeyote au kutiliwa maanani.
Azimio hilo lilipendekezwa na Marekani pamoja na nchi tatu za Ulaya za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani na lilipasishwa Jumatano iliyopita na Bodi ya Magavana ya IAEA licha ya upinzani mkali wa China na Russia.
Kufuatia hatua hiyo ya Bodi ya IAEA dhidi ya Iran kwa kushinikizwa na Wamagharibi, Jamhuri ya Kiislam imeondoa kamera 18 za ukaguzi katika taasisi zake za nyuklia, likiwa ni jibu madhubuti kwa chokochoko hizo.
Kadhalika Tehran imeanza kumimina gesi ya urani kwenye mashinepewa zake za kisasa kama sehemu ya radimali yake kwa uchokozi huo; hayo ni kwa mujibu wa Mohammad Eslami, Rais wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (AEOI).