Mustakabali mwema katika Muungano wa China, Russia na Iran
https://parstoday.ir/sw/news/world-i86116-mustakabali_mwema_katika_muungano_wa_china_russia_na_iran
Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Russia amesema China, Russia na Iran zitaunda muungano mkubwa katika mustakabali wa dunia.
(last modified 2024-06-01T06:57:28+00:00 )
Jul 21, 2022 03:10 UTC
  • Mustakabali mwema katika Muungano wa China, Russia na Iran

Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Russia amesema China, Russia na Iran zitaunda muungano mkubwa katika mustakabali wa dunia.

Kazem Jalali, Balozi wa Iran nchini Russia aliyasema hayo Jumatano usiku katika mahojiano maalumu na Televisheni ya Iran (IRIB) ambapo ameongeza kuwa, muundo mpya wa nguvu duniani unaibuka.

Jalali ameendelea kusema kuwa, Russia ni nchi jirani ya Iran katika upande wa kaskazini na ni nchi yenye nguvu na uwezo wa kiwango cha juu na katika upande wa pili Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nayo ni dola lenye nguvu na uwezo kieneo na kimataifa. Aidha amesema kilichowazi ni kuwa, kuna muungano mpya unaoibuka katika eneo na kuwepo muungano kama huo bila shaka kutaibua wasiwasi miongoni mwa madola makubwa duniani hasa Marekani.

Akizungumza katika mahojiano hayo, Mohamad Farazmand Balozi wa Iran nchini Uturuki ameashiria katika kikao cha Tehran cha Jumanne cha Marais wa Russia, Iran na Uturuki na kusema: "Katika kikao cha Tehran viongozi wa nchi hizi tatu walisisitiza kuhusu kulindwa mamlaka ya kujitawala Syria na kukumbusha kuwa kurejea uthabiti katika nchi hiyo hakuwezi kufikiwa kupitia njia za kijeshi."

Kazem Jalali, Balozi wa Iran nchini Russia

Naye Ali Asghar Khaji, msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran katika masuala ya kisiasa amesema: "Kikao cha Saba cha 'Mchakato wa Astana' kilichofanyika Tehran Jumanne kuhusu kurejesha amani Syria kilifanyika kwa mafanikio makubwa."

Ikumbukwe kuwa kikao cha saba cha viongozi wa nchi wadhamini wa 'Mchakato wa Mazungumzo ya Amani ya Astana', kilifanyika Jumanne mjini Tehran kwa kuhudhuriwa na marais wa nchi tatu za Iran, Russia na Uturuki.

'Mchakato wa Mazungumzo ya Amani ya Astana' ni ubunifi wa Iran, Russia na Uturuki kuhusu kuhitimishwa vita Syria na kutatuliwa mgogoro wa nchi hiyo ya Kiarabu kwa njia ya amani. Mkutano huo ulifanyika kwa mara ya kwanza Januari 2017 katika mji wa Astana nchini Kazakhstan na ndio maana ukapewa jina la 'Mchakato wa Astana.'