Marekani yaripoti kesi ya kwanza ya polio baada ya muongo mmoja
https://parstoday.ir/sw/news/world-i86148
Marekani imeripoti kesi ya kwanza ya ugonjwa wa kupooza au polio baada ya kupita karibu miaka kumi.
(last modified 2025-07-15T05:05:40+00:00 )
Jul 22, 2022 07:25 UTC
  • Marekani yaripoti kesi ya kwanza ya polio baada ya muongo mmoja

Marekani imeripoti kesi ya kwanza ya ugonjwa wa kupooza au polio baada ya kupita karibu miaka kumi.

Wizara ya Afya ya Marekani ilitangaza hayo jana Alkhamisi na kuongeza kuwa, mtu aliyegundulika kuwa na virusi vya polio ni mkazi wa kaunti ya Rockland katika jimbo la New York.

Kamishna wa Afya katika kaunti ya Rockland, Patricia Schnabel Ruppert amesema kwa sasa mgonjwa huyo hana hatari kubwa ya kuambukiza, lakini yupo chini ya uangalizi, huku wakifuatilia iwapo watu waliotangamana naye wameambukizwa.

Kwa mujibu wa Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa cha Marekani (CDC), kesi ya mwisho wa ugonjwa wa polio kuripotiwa nchini humo ilikuwa mwaka 2013.

Ugonjwa wa polio hushambulia mfumo wa neva na unaweza kusababisha ulemavu baada ya muda mfupi. Polio hauna tiba lakini maambukizi yanaweza kuzuiwa kwa chanjo.

Chanjo ya Polio

Ikumbukwe kuwa, mwaka 2020, Kamisheni Huru ya Kanda ya Afrika ya Uthibitisho wa Kutokomeza Polio, ARCC ilitangaza kwamba kuanzia Agosti 25 mwaka huo, virusi vya polio havipo tena katika ukanda wa Shirika la Afya Duniani, WHO, kwa kanda ya Afrika.

Katika nchi zote 54 za Afrika, nchi ambazo si wanachama wa WHO kanda ya Afrika ni Somalia, Sudan, Eritrea, Misri, Libya na Tunisia. Hata hivyo Mei mwaka huu, Msumbiji iliripoti kesi ya kwanza ya maambukizi ya ugonjwa huo wa kupooza, baada ya kupita miaka 30.