China yaitaka Marekani iiondolee Iran vikwazo haramu
Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Kudhibiti Silaha katika Wizara ya Mambo ya China ameitaka Marekani iiondolee Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vikwazo haramu.
Fu Cong alitoa mwito huo akihutubia Kongamano la 10 la Kuangaliwa Upya Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Usambazaji wa Silaha za Atomiki (NPT) mjini New York na kuongeza kuwa, changamoto zinazoikabili sekta ya nyuklia inapaswa kutatuliwa kupitia njia za siasa na diplomasia.
Amesema pande zote za makubaliano ya nyuklia ya JCPOA zinapaswa kujitolea kwa dhati kuhakikisha kuwa mapatano hayo ya kimataifa yanarejea katika mkondo kupitia mazungumzo ya kidiplomasia, na kujiepusha na tabia ya kushinikiza kupitia vikwazo na vitisho vya kutumia nguvu.
Ofisa huyo wa ngazi ya juu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China ameeleza bayana kuwa, "Marekani inapaswa kuiondolea Iran vikwazo vyote vinavyokiuka sheria, na kwa msingi huo Iran ianze tena kutekeleza majukumu yake ya kufungamana na makubaliano hayo kikamilifu."
Kabla ya hapo, Peter Szijjarto, Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland pia alilihutubia kongamano hilo na kusisitiza kuwa, inabidi mataifa ya dunia yashirikiane pamoja kufaidika kwa njia za amani na nguvu za atomiki na kusitumiwe vikwazo kama njia ya kuyazuia baadhi ya mataifa kufaidika na haki yao hiyo.
Marekani iko mstari wa mbele kuziwekea vikwazo nchi nyingine hasa Iran ili kujaribu kuizuia isifaidike kwa njia za amani na nishati muhimu sana ya nyuklia.