Kiwewe cha Marekani kwa kuzidi kuongezeka nguvu za China
(last modified Sat, 20 Aug 2022 02:41:55 GMT )
Aug 20, 2022 02:41 UTC
  • Kiwewe cha Marekani kwa kuzidi kuongezeka nguvu za China

Marekani ambayo imeingia kiwewe kutokana na kuzidi kuongezeka nguvu za China, imeahidi kuchukua hatua za kukabiliana na Beijing katika kipindi cha wiki na miezi ijayo karibu na kisiwa cha Taiwan, kwa tamaa ya kupunguza kasi ya nguvu za kijeshi na kiuchumi za China.

Edward "Ned" Price, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani alisema siku ya Jumatano kuwa, Washington itachukua hatua nzito na kali lakini pole pole ili kulinda kile alichodai ni amani na utulivu kutokana na kuongezeka juhudi za China za kujaribu kubadilisha hali iliyopo hivi sasa, kwa manufaa yake. 

Ned Price pia amesema, hatua hizo za Marekani zitajumuisha mambo mengi na zitatangazwa katika kipindi cha wiki na miezi ijayo kwani kuna changamoto nyingi na za muda mrefu zinaikabili Marekani kutoka kwa Beijing hasa kwa vile China imebakisha wanajeshi wake wa anga ya baharini karibu na kisiwa cha Taiwan licha ya kumalizika mazoezi yake ya kijeshi ya baada ya spika wa bunge la Marekani kufanya uchochezi wa kuitembelea Taiwan licha ya onyo kali lililotolewa na China. Price amedai kuwa: Hatua yoyote itakayochukuliwa na Marekani itachunga siasa za China Moja, sheria za Marekani kuhusu uhusiano wake na Taiwan na mambo mengine yanayohusiana na kadhia hiyo.

Mzozo baina ya Marekani na China umeongezeka mno hivi sasa kuliko wakati mwingine wowote

 

Madai mapya ya Washington ya kukabiliana na hatua ilizodai ni za kichochezi za China yametolewa katika hali ambayo, tunapoyatupia jicho matukio ya miezi kadhaa iliyopita hasa hatua ya Marekani ya kuchochea waziwazi kujitenga Taiwan na China na kukabiliana bila ya kificho na siasa za China Moja tutaona kuwa siasa hizo za kiistikbari za White House ndizo zilizoilazimisha Beijing kuchukua hatua kali za kujibu uchochezi huo wa Marekani. Mzozo baina ya China na Marekani umeongezeka zaidi baada ya spika wa bunge la nchi hiyo, Nancy Pelosi kutembelea kisiwa cha Taiwan tarehe pili mwezi huu wa Agosti 2022 licha ya China kupinga vikali ziara hiyo. Mara baada ya ziara hiyo, China ilimwita balozi wa Marekani nchini humo na kumkabidhi malalamiko yake makali kwa hatua hiyo ya kichochezi ya Nancy Pelosi kwani China inaihesabu Taiwan kuwa ni sehemu ya ardhi yake isiyotenganishika na ardhi nyingine za China na hatua ya kiongozi mkubwa huyo wa Marekani ya kuingia katika ardhi yake bila ya idhini ya Beijing ni uvunjaji wa wazi na wa kijeuri wa haki ya kujitawala ardhi yote ya China na ni uingiliaji wa wazi wa masuala ya ndani ya nchi hiyo. Suala la Taiwan kuwa sehemu ya ardhi ya China limethibitishwa na linatambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa. Beijing inaamini kuwa, ziara ya Pelosi huko Taiwan inapingana kikamilifu na siasa za China Moja. Tangu mwaka 1979, Marekani inaitambua Taiwan kuwa ni nchi huru. Licha ya China kupinga vikali, lakini Marekani katika miaka ya hivi karibuni hususan kwenye serikali ya hivi sasa ya Joe Biden, imeongeza kiwango cha silaha inazoiuzia Taiwan na kuichochea ijitenge na China. Si hayo tu, lakini pia Marekani inayaunga mkono waziwazi na kikamilifu makundi yanayopigania kujitenga na China, kisiwa hicho cha Taiwan. Bila ya shaka yoyote siasa hizo za kibeberu za Marekani haziwezi kuvumiliwa kwa hali yoyote ile na China na ndio maana Beijing imechukua hatua kali za kujibu ziara ya spika wa bunge la Marekani na familia yake huko Taiwan.

Ziara ya kichochezi wa spika wa bunge la Marekani, Nanchi Pelosi huko Taiwan

 

Tarehe 6 mwezi huu wa Agosti, China ilifanya luteka na maneva makubwa ya kijeshi karibu na kisiwa cha Taiwan na siku ya pili yake yaani tarehe 7 Agosti ilikata uhusiano wake na Marekani katika nyuga kadhaa muhimu sana kwa Washington yakiwemo masuala ya kijeshi, kupambana na uhalifu wa kimataifa, madawa ya kulevya na ushirikiano katika kukabiliana na uchafuzi wa hali ya hewa. Hatua hizo kali zilizochukuliwa na China kujibu ziara hiyo ya kichochezi na Nancy Pelosi huko Taiwan, zinatarajiwa kuongezeka na kuendelea. Kiujumla ni kwamba matukio ya hivi karibuni yamezidi kuvuruga uhusiano wa Marekani na China na hivi sasa uhusiano huo umefikia kiwango cha chini kabisa kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni. 

China haikuishia hapo, bali tayari hivi sasa imeanza kuchukua hatua nyingine za kuiadhibu Marekani katika nyuga tofauti za kisiasa, kidiplomasia, kiusalama na kijeshi ili kutoa funzo kwa siasa za kiuadui za Washington. Kwa kweli inaonekana kuwa Marekani haikutarajia kabisa kupokea majibu makali kama hayo kutoka kwa Beijing. Sasa hivi Marekani inalalamika na inaonekana wazi kuwa, hatua ambazo hivi sasa Washington inadai itazichukua dhidi ya China ni aina fulani ya kutapatapa huku Marekani ikijaribu kutafuta njia za kujikwamua kutoka kwenye mgogoro iliyojitumbukiza ndani yake.