Kifo cha Gorbachev na mafunzo ya kihistoria
https://parstoday.ir/sw/news/world-i87640-kifo_cha_gorbachev_na_mafunzo_ya_kihistoria
Mikhail Gorbachev, kiongozi wa mwisho wa Shirikisho la Sovieti, alifariki dunia Jumanne usiku akiwa na umri wa miaka 91 katika hospitali moja mjini Moscow baada ya kuugua kwa muda mrefu. Kifo cha Gorbachev kimekabiliwa na hisia nyingi za ndani na nje, ambapo Rais Vladimir Putin wa Russia, maafisa wa UN na Katibu Mkuu wake na wakuu kadhaa wa nchi, wametuma salamu za rambirambi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 31, 2022 10:26 UTC
  • Kifo cha Gorbachev na mafunzo ya kihistoria

Mikhail Gorbachev, kiongozi wa mwisho wa Shirikisho la Sovieti, alifariki dunia Jumanne usiku akiwa na umri wa miaka 91 katika hospitali moja mjini Moscow baada ya kuugua kwa muda mrefu. Kifo cha Gorbachev kimekabiliwa na hisia nyingi za ndani na nje, ambapo Rais Vladimir Putin wa Russia, maafisa wa UN na Katibu Mkuu wake na wakuu kadhaa wa nchi, wametuma salamu za rambirambi.

Gorbachev, ambaye aliingia katika ngazi za juu za uongozi mwaka 1985, alianzisha wimbi la mageuzi ya kisiasa na kiuchumi yenye lengo la kulifanya Shirikisho la Sovieti kuwa na mfumo wa kisasa kwa sababu wakati huo shirikisho hilo lilikuwa linakumbwa na migogoro mikubwa. Alikuwa mtetezi wa uhusiano wa karibu na nchi za Magharibi na alishinda Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 1990. Kuanzia 1990 hadi 1991, Gorbachev alichukua uongozi wa Shirikisho  la Sovieti; na akiwa uongozini kulishuhudiwa kuanguka kwa Shiriksho la Sovieti na hatimaye akalazimika kujiuzulu mnamo Desemba 25, 1991. Akiwa madarakani Gorbachev alichukua hatua muhimu za kuleta mabadiliko katika Shirikisho la Sovieti. Katika utawala wake, alifuata sera mbili ambazo ni; sera ya mageuzi ya kisiasa inayojulikana kama glasnost (uwazi), ambayo iliruhusu kuongezeka uhuru wa kusema na uhuru wa vyombo vya habari, na sera ya mageuzi ya kiuchumi inayojulikana kama perestroika (urekebishaji), ambayo ilijaribu kugatua maamuzi ya kiuchumi ili kuboresha ufanisi.

Katika uga wa sera za kigeni, mwaka 1988 Gorbachev akiwa Mwenyekiti wa Kamati Kuu Tendaji ya Bunge alitangaza kwamba Umoja wa Kisovieti haungefuata tena Mafundisho ya Brezhnev na kwamba mataifa ya Kambi ya Mashariki yalikuwa na uhuru wa kuamua juu ya maswala ya kigeni. Gorbachev alitaka kumalizwa Vita Baridi na kuelekeza juhudi zake katika kupunguza uhasama na kuongeza mawasiliano na biashara na nchi za Magharibi. Alikuwa na mtazamo mzuri na chanya kuelekea Magharibi. Katika juhudi za kuboresha uhusiano na Marekani, Gorbachev alichukua hatua za kutokomeza na kudhibiti silaha, ambazo hatimaye zilipelekea kutiwa saini mkataba wa kutokomeza Silaha za Nyuklia za Masafa ya Kati (INF) ambao ulianza kutekelezwa mwaka 1988.

Mikhail Gorbachev na Ronald Reagan wakitia saini mapatano ya INF

Licha ya matumaini ya Gorbachev na juhudi zake za kupitisha sera mpya katika kujikurubisha upande wa kambi ya Magharibi, lakini juhudi zote za Marekani, kama kinara wa kambi ya Magharibi wakati wa Vita Baridi, zililenga kupanua mashindano ya silaha na Shirikisho la Sovieti na hivyo kudhoofisha uchumi  wa shirikisho hilo.  Aidha licha ya Gorbachev kunyosha mkono wa urafiki, Marekani ilikuwa inatekeleza njama nyuma ya pazia kwa ajili ya kupunguza kiwango cha ustawi wa watu wa Soviet, na hiyo ikawa moja ya sababu za kusambaratika Shirikisho la Sovieti mwaka1991. Nukta hii daima ilikuwa ni dosari kubwa ambayo ilipelekea Gorbachev aendelee kulaumiwa na waungaji mkono wa Shirikisho la Sovieti wanaoamini kuwa alikuwa sababu ya kusambaratika shirikisho hilo. Ni kwa msingi huo ndio, wakati Mikhail Gorbachev alikuwa anatazamwa kama bingwa katika ulimwengu wa Magharibi, hakuwahi kupata heshima ndani ya Russia na hivyo alipogombea urais mwaka 1996, alipata chini ya asilimia 5 ya kura.

Baada ya kusambaratika Shirikisho la Sovieti mnamo Desemba 1991 na kuundwa kwa nchi mpya 15, Russia (Urusi) ilikubaliwa kuwa mrithi wa Shirikisho la Sovieti katika Umoja wa Mataifa.

Licha ya matumaini ya awali ya Warusi kuelekea Magharibi katika miaka ya 1990, na hata wazo la waliokuwa na misimamo ya Kimagharibi  kwamba Russia ingekubaliwa kuwa katika kambi ya Magharibi, kivitendo, Marekani, kama kinara wa Kambi ya Magharibi na muungano wa kijeshi wa NATO, imefuata sera ya kuidhoofisha au kuiangusha Russia kwa kupanua NATO kuelekea katika mipaka ya Russia.

Kwa sababu hiyo, tangu Vladimir Putin, rais wa sasa wa Russia, aingie madarakani mwaka 2000, kutokana na mitazamo yake ya utaifa na juhudi zake za kufufua hadhi ya zamani ya Russia, uhusiano wa Russia na Kambi ya Magharibi umekuwa ukizorota hatua kwa hatua  na taharuki baina ya pande mbili zimeongezeka zaidi baada ya kuibuka mzozo wa Ukraine mnamo 2014.

Rais Vladimir Putin wa Russia

Uhusiano baina ya Russia na madola ya Magharibi ulichukua mkondo mbaya zaidi baada ya kuzuka kwa vita vya Ukraine mnamo Februari 2022.

Jahangir Kerami, mhadhiri  wa chuo kikuu, anasema kuhusu nukta hii kuwa: sehemu kubwa ya mgogoro huu ni matokeo ya miaka 30 ya mashinikizo ya madola ya Magharibi dhidi ya Russia na kufedheheshwa kwa serikali ya Moscow tangu wakati wa kusambaratika Shirikisho la Sovieti hadi sasa. Aidha madola ya Magharibi yamekiuka mapatano yaliyopigiwa debe na Gorbachev kuhusiana na masuala ya silaha na majeshi.

Hivi sasa Wamagharibi wakiongozwa na Marekani pamoja na kukabiliana na Moscow katika nyanja ya usalama na kijeshi wanafuata sera ya kushadidisha mashinikizo dhidi ya Russia katika nyanja mbalimbali za kisiasa na kidiplomasia, kibiashara na kiuchumi, kijeshi na kivita na nishati. Mashinikizo hayo sasa yamechukua mkondo wa kuiwekea Russia vikwazo vikubwa na ambavyo havijawahi kushuhudiwa.

Kwa maelezo hayo, utawala wa Gorbachev na vitendo vyake vya ndani na nje, ambavyo kwa mtazamo wa wazalendo wa Russia vilikuwa moja ya sababu kuu ya kuporomoka kwa Shirikisho la Soveiti vimekuwa somo kwa viongozi wa sasa wa Russia, haswa Vladimir Putin ambaye hawezi tena kukariri makosa ya Gorbachev, hasa ya kuwaaamini Wamagharibi na kuchukua hatua za kutaka kuwaridhisha.