Feb 14, 2023 07:31 UTC
  • Kashfa Katoliki; Watu karibu 5,000 wahanga wa unyanyasaji wa kingono Ureno

Kwa mara nyingine tena Kanisa Katoliki limekumbwa na sakata jipya la ufuska; ambapo maelfu ya watu wameripotiwa kuwa wahanga wa udhalilishaji wa kingono wa kanisa hilo nchini Ureno.

Uchunguzi mpya umefichua kuwa, makasisi, maaskofu na maafisa wengine wa Kanisa Katoliki nchini Ureno wanakabiliwa na tuhuma za kuwanyanyasa na kuwadhalilisha kingono maelfu ya watoto wadogo.

Kamisheni Huru ya Uchunguzi inayofuatilia faili la kashfa za viongozi hao wa Kanisa Katoliki za kubaka na kuwalawiti watoto wadogo nchini Ureno imefichua kuwa, huenda watu 4,800 ni wahanga wa unyanyasaji wa kingono wakiwa watoto katika nchi hiyo ya Ulaya. 

Uchunguzi huo umefuatilia visa na kashfa za kunyanyaswa kingono watoto na makasisi, maaskofu, mapadri na wakuu wengine wa makanisa ya Katoliki nchini humo kuanzia mwaka 1950 mpaka sasa.

Maaskofu wa Katoliki nchini Ureno wanatazamiwa kuijadili ripoti ya kamisheni hiyo tarehe 3 mwezi ujao wa Machi katika mkutano maalumu. Hata hivyo tayari Askofu José Ornelas wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katiliki Ureno amewaomba radhi wahanga wa visa hivyo vya ufuska vilivyofanywa na viongozi wa kanisa hilo.

Papa Francis, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani

Haya yanajiri siku chache baada ya Papa Francis, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani kutetea vitendo vichafu vya mapenzi ya jinsia moja ambavyo vimekuwa vikilalamikiwa katika mataifa mbalimbali duniani.

Katika miaka ya hivi karibuni, kashfa za kubaka na kunajisi za makasisi, maaskofu na maafisa wa Kanisa Katoliki nchini Marekani na barani Ulaya zimekabiliwa na wimbi kubwa la ukosoaji dhidi ya makao makuu ya Kanisa hilo, Vatican.

Tags