UN: Watu milioni 65 wamelazimika kuwa wakimbizi duniani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i9601-un_watu_milioni_65_wamelazimika_kuwa_wakimbizi_duniani
Idadi ya wakimbizi duniani imeendelea kuvunja rekodi na kutia wasi wasi, ambapo watu milioni 65.3 wamelazimika kuwa wakimbizi katika kona mbali mbali za dunia kufikia mwishoni mwa mwaka jana 2015.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 20, 2016 03:38 UTC
  • UN: Watu milioni 65 wamelazimika kuwa wakimbizi duniani

Idadi ya wakimbizi duniani imeendelea kuvunja rekodi na kutia wasi wasi, ambapo watu milioni 65.3 wamelazimika kuwa wakimbizi katika kona mbali mbali za dunia kufikia mwishoni mwa mwaka jana 2015.

Hayo yamesemwa na Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR leo Jumatatu, kwa mnasaba wa Siku ya Wakimbizi Duniani. Takwimu mpya za shirika hilo zinaonyesha kuwa, kiwango hicho ni ongezeko la kutia wasi wasi ikilinganishwa na idadi ya wakimbizi iliyosajiliwa mwishoni mwa mwaka juzi 2014 ya watu milioni 5.8. Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya wakimbizi ametaka jinamizi hilo la wakimbizi lishughulikiwe haraka iwezekanavyo. Filippo Grandi, Mkuu wa Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa ameashiria idadi kubwa mno ya watu waliobaki bila ya makaazi na kulazimika kuwa wakimbizi kutokana na machafuko katika maeneo mbalimbali duniani na kuitaka Jamii ya Kimataifa ilishughulikie haraka suala hilo. Mkuu huyo wa UNHCR amesema kuendelea raia kupoteza makazi yao, kuongezeka kiwango cha chuki dhidi ya wageni duniani na kutolingana kiwango cha fedha zilizopo na gharama zinazohitajika kwa ajili ya kushughulikia matatizo ya kibinadamu duniani, ni miongoni mwa changamoto zenye udharura wa kutatuliwa.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, kutokana na idadi jumla ya watu duniani kukadiriwa kuwa bilioni 7.34, kwa kila watu 113, mmoja ni mkimbizi ima wa ndani au nje ya nchi yake.