Jun 01, 2023 01:23 UTC
  • Meli ya mwisho ya  kivita ya Ukraine, yaangamizwa na jeshi la Russia

Wizara ya Ulinzi ya Russia imetangaza kuwa, jeshi la nchi hiyo limeshambulia na kuangamiza meli ya mwisho ya kivita ya Ukraine katika bandari ya Odesa.

Kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa Russia imo vitani na Ukraine. Vita hivyo vimezuka kutokana na uchochezi wa nchi za Magharibi ambazo ziliisukuma Russia mpaka ikalazimika kuingia vitani na Ukraine baada ya viongozi wa Kyiv kukubali kuwa vibaraka wa Magharibi na kujiingiza kwenye vita angamizi na Russia.

Tangu mwanzoni mwa vita hivyo, miongoni mwa maeneo yanayolengwa sana na Russia ni ya majeshi ya anga na baharini ya Ukraine na kuangamiza zana na vifaa vya majeshi hayo. Moscow inatumia manuwari zake za kijeshi na makombora yake ya kisasa kuangamiza maeneo ya kijeshi ya serikali ya Kyiv.

Wanajeshi wengi wa Ukraine wanaendelea kuuawa siku baada ya siku kutokana na siasa mbovu za viongozi wao

 

Jana Jumatano, shirika la habari la IRNA lilinukuu taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Russia ikisema kuwa, jeshi la anga la nchi hiyo limetumia silaha yenye shabaha ya hali ya juu kuteketeza meli ya mwisho ya kivita ya Ukraine ijulikanayo kwa jina la Yuri Olefirenko katika bandari ya Udesa ya kusini magharibi mwa nchi hiyo.

Meli ya kivita vya Yuri Olefirenko ilitengenezwa nchini Russia katika muongo wa 1990. Lakini ilikuwa milki ya Ukraine baada ya kusambaratika Umoja wa Kisovieti. Meli hiyo imefanyiwa matengenezo kwa muda mrefu na matengenezo makubwa zaidi yalifayika mwaka 2016.

Wizara ya Ulinzi wa Russia pia imesema katika taarifa yake hiyo kwamba, hivi sasa mapigano makali yanaendelea katika eneo la Avdeevka lililoko katika njia ya kuelekea kwenye jimbo la Donetsk.

Wizara ya Ulinzi ya Russia imesema pia kuwa, idadi ya wanajeshi wa Ukraine waliouawa katika kipindi cha masaa 24 ya hadi wanatoa taarifa hiyo walikuwa 200.