Ujerumani yanunua mafuta ya Iran licha ya vikwazo vya Marekani
Data zilizotolewa na Kituo cha Takwimu cha Ulaya cha Eurostat zimefichua kuwa, Ujerumani imeagiza shehena kubwa ya mafuta kutoka Iran kwa mara ya kwanza tokea mwaka 2018, licha ya vikwazo vya Marekani.
Takwimu mpya za Eurostat zimebainisha kuwa, kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Ujerumani imenunua tani 69,737 za mafuta ghafi na bidhaa za mafuta kutoka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Mehr, uagizaji huo wa mafuta ya Iran ulifanyika mwezi Machi mwaka huu 2023. Ujerumani imeanza tena kununua mafuta ya Iran katika hali ambayo, Marekani haijatangaza kuiondolea vikwazo haramu Jamhuri ya Kiislamu.
Bulgaria, nchi nyingine mwanachama wa Umoja wa Ulaya, pia imeripotiwa kununua tani 147 za mafuta na bidhaa za mafuta za Iran katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka huu.

Nchi za Ulaya hivi sasa zinaendelea kukabiliwa na mgogoro mkubwa wa nishati baada ya nchi za bara hilo kuiwekea vikwazo Russia kwa kisingizio cha vita vya Ukraine. Nchi hizo zinanunua mafuta ya Iran licha ya kuwepo kwa vikwazo vya Marekani na EU.
Aidha inaarifiwa kuwa, nchi hizo za Ulaya hivi sasa zimeamua kukimbilia barani Afrika katika jitihada za kukabiliana na mgogoro wa nishati unaozidi kulisakama bara Ulaya.