Leo katika Historia, Jumatano tarehe Pili Agosti 2023
Leo ni Jumatano tarehe 15 Muharram 1445 Hijria sawa na tarehe Pili Agosti 2023.
Siku kama ya leo miaka 1092 iliyopita, yaani tarehe 15 Muharram mwaka 353 Hijiria, alifariki dunia Ibn Sakan mwanazuoni na mpokezi mashuhuri wa hadithi wa karne ya nne Hijiria. Ibn Sakan alizaliwa mwaka 294 Hijiria huko mjini Baghdad, Iraq ambapo alisafiri katika nchi mbalimbali kwa ajili ya kutafuta elimu. Ibn Sakan alikusanya hadithi nyingi katika miji ya nchi kama Uzbekistan, Tajikistan, Kazakhstan Kyrgyzstan (Transoxiana), Khorasan, Iraq, Sham na Misri na mwishowe akaweka makazi yake nchini Misri. Mpokezi huyo wa hadithi ameacha athari nyingi na mojawapo ni kitabu cha historia kinachohusu maswahaba wa Mtume SAW, kinachoitwa Al Huruf fi Al -Swahaba.

Katika siku kama ya leo, miaka 856 iliyopita, sawa na tarehe 15 Muharram mwaka 589, alizaliwa Ali bin Mussa bin Ja'far maarufu kwa jina la Ibn Twaus, faqihi, mpokezi wa hadithi na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu katika eneo la Hillah nchini Iraq. Ibn Twaus alipitisha kipindi cha utotoni katika mji huo na baadaye alihamia mjini Baghdad ambako aliishi kwa kipindi cha karibu miaka 15. Ibn Twaus alipata umashuhuri mkubwa katika elimu na ucha-Mungu na ameandika vitabu vingi ambavyo ni marejeo ya taaluma za Kiislamu. Kitabu mashuhuri zaidi cha msomi huyo ni "al Luhuuf" ambacho ndani yake alizungumzia kwa namna bora zaidi matukio ya Siku ya Ashura na harakati ya Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) katika medani ya vita vya Karbala. Kitabu kingine mashuhuri cha mwanazuoni huyo ni "Al Iqbal". Ibni Twaus alifariki dunia mwaka 664 akiwa na umri wa miaka 75.

Siku kama ya leo miaka 89 iliyopita inayosadifiana na tarehe Pili Agosti 1934, alifariki dunia Field Marsha Paul von Hindenburg, rais wa zamani wa Ujerumani na Amiri Jeshi Mkuu wa vikosi vya majeshi ya nchi hiyo wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia. Hindenburg alichaguliwa kuwa Rais wa Kwanza wa Ujerumani mwaka 1925.

Tarehe Pili Agosti miaka 78 iliyopita, kongamano la Potsdam lilikamilisha kazi zake. Kongamano hilo la tatu na la mwisho la viongozi waitifaki walioshiriki katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, lilianza tarehe 17 mwezi Julai na kumalizika tarehe Pili Agosti 1945. Kongamano hilo lililofanyika katika mji wa Potsdam karibu na mji mkuu wa Ujerumani, Berlin lilihudhuriwa na Joseph Stalin, Harry S. Truman na Winston Churchill, marais wa wakati huo wa Urusi ya zamani, Marekani na Uingereza.

Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulitumwa katika nchi za Iran na Iraq na ukatoa ripoti mbili ambazo zilieleza kuwa, utawala wa zamani wa Iraq ulitumia mara kadhaa silaha za kemikali dhidi ya majeshi na raia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa kukiri waziwazi kwamba, jeshi la Iraq lilitumia silaha za kemikali dhidi ya Iran. Pamoja na hayo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halikutoa azimio lolote dhidi ya utawala wa dikteta Saddam Hussein wa Iraq ambao ulikuwa ukiungwa mkono na nchi za Magharibi, kwa kutumia silaha za kemikali. Masaa kadhaa baada ya kutolewa ripoti hizo, ndege za kivita za Iraq ziliushambulia tena mji wa Ushnawiye kwa mabomu ya kemikali na kujeruhi watu 2400.

Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, jeshi la Iraq liliishambulia na kuikalia nchi jirani ya Kuwait. Huo ulikuwa uvamizi wa pili wa Iraq kwa jirani zake baada ya ule wa Iran wa mwaka 1980. Utawala wa Saddam ulikuwa ukidai kwamba, ardhi ya Kuwait ni sehemu ya ardhi yake. Mashambulio ya Iraq dhidi ya Kuwait yalikabiliwa na radiamali kali ulimwenguni. Nchi nyingi duniani na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilaani uvamizi huo na kuvitaka vikosi vya Iraq kuondoka mara moja katika ardhi ya nchi hiyo. Nchi kadhaa zikiongozwa na Marekani zilituma vikosi vyao vya kijeshi katika Ghuba ya Uajemi ili kuviondoa vikosi vamizi vya Iraq kutoka katika ardhi ya Kuwait na kuhitimisha uvamizi huo Februari 28 mwaka 1991.
