Oct 20, 2023 12:50 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (83)

Assalaam alaykum wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu, ili kwa pamoja tufungue ukurasa mwingine katika maisha Maulamaa wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu, bila kusahau athari na vitabu vyao.

 

Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 83 ya mfululizo huu kitamzungumzia msomi na alimu mwingine na wa kipekee. Huyu ni Sayidah Nusrat Amin ambaye ni mwanamke wa kwanza wa Kiislamu kufikia daraja ya Ijtihadi. Kuweni pamoja nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

I

Mwaka 1925 wakati Reza Khan aliposhika hatamu za uongozi nchini Iran, hakuna mtu aliyekuwa akifahahamu anapanga kufanya nini. Alikuwa akisema, lengo lake ni kuifanya Iran iwe ya kisasa na kuandaa fursa zaidi za kijamii kwa ajili ya wanawakke. Fursa za masomo, haki ya kuchagua na kuchaguliwa katika medani za kijamii na kisiasa, uhuru na kuwaondolea vizingiti wanawake vya kuingia katika jamii ni miongoni mwa ahadi ambazo Reza Khan aliwapa wanawake. Miaka kumi baadaye wakari Reza Khan alipotoa amri ya kupinga kuvaa Hijabu, hapo ndipo wananchi wa Iran walipofahamu makusudio yake ya uhuru na mahudhurio ya wanawake kijamii yalikuwa nini.

Baada ya kutekelezwa kwa Sheria ya kuvua Hijabu, wanawake na wasichana wa Kiislamu wa Iran walipendelea kukaa nyumbani badala ya kuhudhuria mikusanyiko ya watu. Kwa hakika kivitendo wanawakke na mabinti walilazimika kuacha masomo ili kulinda hijabu na utakasifu wao.

Hili ndilo lilikuwa tatizo la familia zote zilizokuwa zimeshikamana na dini. Sadr al-Ashraf, mmoja wa maofisa wa utawala wa Pahlavi, anasema kuhusu hili: “Nilipomwomba mke wangu kushiriki katika sherehe lakini bila ya vazi la hijabu, aliniomba nimpe talaka badala ya kutekeleza takwa langu hilo. Zikapita siku kadhaa. Nikamwambia mke wangu, kadhia ni muhimu na nyeti mno, hivyo kesho  unapashwa kushiriki katika sherehe bila ya kuwa na vazi la hijabu. Mke na mabinti zangu wakakubali na kesho yake wakashiriki katika hafla ile bila ya kujistiri kwa hijabu; lakini kuanzia siku ile na kuendelea, mke wangu akaugua na hakutoa mguu wake ndani ya nyumba mpaka baada ya mwaka mmoja siku ambayo jeneza lake lilitolewa kwa ajili ya kwenda kuzikwa.

Kuwavuta wanawake na wasichana wa Kiirani upande wa ufuska ilikuwa ni moja ya sera kuu za serikali ya Iran enzi ya utawala wa ukoo wa Kipahlavi..... lakini... Mungu alikuwa akitaka kitu kingine kwa wanawake wa Iran.

Takriban sambamba na Reza Khan kutoa amri ya kuvua hijabu, kitabu kimoja kiliwafikia wanazuoni wa Najaf. Kitabu ambacho maudhui yake ya kidini na itibari ya kielimu kilikuwa kikitoa habari ya daraja ya kielimu, kidini na kiirfani yya mwandishi wake. Lililokuwa la ajabu zaidi kwa Maulamaa ni pale walipofahamu kwamba, mwandishi wa kkitabu hicho ni mwanamke. Licha ya kuweko ufisadi na ufuska wa wanawake katika televisheni na tasnia ya sinema ya Iran ambao ulikuwa ukidhihirika wazi, kwa Maulamaa lilikuwa jambo gumu mno kwao kuamini kwamba, kitabu cha Arbain kimeandikwa na mwanamke.

 

Shaka hii ilikwenda mbali zaidi kiasi kwamba mmoja wa wanachuoni wa Najaf alikwenda alifanya safari na kwenda Isfahan ili kuhakikisha utambulisho wa mwandishi. Baada ya kukutana na Bibi Esfahani, alimuuliza maswali kuhusu fiqhi, usul, falsafa, mantiki na Qur'an, na aliposikia majibu safi na ya kipekee ya bibi huyo, akapata yakini kuwa "Sayedah Nusrat Amin" ndiye mwandishi wa kitabu cha "Arbain". Kufuatia tukio hili, wanachuoni wengine pia walimuuliza maswali bibi huyu wa Kiirani na baada ya kubainika umahiri wake wa elimu kidini, walimpa idhini ya ijtijadi na kupokea hadithi. Ndiyo Bibi Nusrat Amin Isfahani" ndiye mwanamke wa kwanza wa Kiislamu aliyefikia daraja ya Ijtihad.

Kipaji na kung'ara mwanamke kama mwanachuoni wa kidini miongoni mwa kundi kubwa la wanazuoni, ambao wote walikuwa wanaume, wakati ambapo kila kitu kilitayarishwa kuwadhalilisha wanawake, je, hiki hakikuwa kitu kingine ghairi ya muujiza?! .....

Mara hii alizaliwa kutoka katika kizazi cha Hadhrat Ali (a.s.) na Hadhrat Fatima (s.a.) msichana, kama Bibi Zainab (s.a.). Msichana huyu alizaliwa Isfahan mwaka 1895 na alianza kujifunza Quran na elimu nyinginezo kuanzia umri wa miaka minne. Inashangaza kwamba msichana huyu alikuwa hajasafiri kwenda Najaf wala Karbala, wala hajaona rangi za majengo ya Hawza Tehran, wala hajatia mguu katika Hawza za Qom au Isfahan.

Seyedah Nusrat Amin alipitisha karibu hatua zote za elimu yake akiwa nyumbani. Muda wote alipokuwa na wazazi wake, walimfundisha, na alipoanzisha familia akiwa na umri wa miaka kumi na tatu, mume wake akiwa na lengo la kumuunga mkono aliwaalika maustadh na walimu nyumbani. Seyedah Nusrat Amin alijitolea kwa wanawake wa Iran akiwa na umri wa miaka 40, na wakati huo alikuwa na huzuni kifuani mwake ya kuwapoteza watoto saba, jambo ambalo lilimfanya kufanana zaidi na Bibi Zainab (as).

Hojjat al-Islam, Nusrat Amin Esfahani aliandika vitabu vingine vingi baada ya kitabu cha "Arbain" ambacho kilikuwa na hadithi arobaini na maelezo ya kifalsafa, kiirfani na fiqhi. Aliandika kitabu cha Miad "Ufufuo" kuhusu njia ya tabia ya mwanadamu kutoka kwa ulimwengu huu hadi ulimwengu wa akhera. Kitabu ambacho kinaweza kupendekezwa kwa wale ambao wanataka kujua zaidi juu ya kifo na maisha ya baadaye.

Pamoja na kuwa Bibi Nusrat Amin alikuwa akitoka nje ya nyumba kwa nadra sana, fikia daraja ya Ijtihad alianzisha harakati za kijamii. Hata harakati zake za kijamii pia alizianzia nyumbani ambapo wanawake kadhaa waliokuwa wakitafuta elimu ya dini walikwenda kwake kama wanafunzi na hivyo akaanzisha darsa yake ya kufundisha nyumbani kwake.

Kidogo kidogo, darsa na masomo haya ya nyumbani yalipelekea kuanzishwa kwa shule iliyoitwa "Shule ya Fatima (as), " Shule ambayo wasichana wapatao elfu moja kutoka Isfahan walisoma, na hii ilikuwa seminari ya kwanza kwa wanawake pekee.

 

Katika hali ambayo serikali ya ukoo wa Kipahlavi ilizilazimisha familia za kidini kuchagua kati ya kuhifadhi staha na utakasifu wa mabinti zao na ulazima wa kujifunza elimu, Bibi Amin alianzisha shule ya upili ya wasichana, ambapo walimu, wanafunzi na wafanyakazi wote walikuwa wanawake, na hii ilikuwa ni nuru ya matumaini kwa waumini ambao walizingatia kusoma elimu ni mojawapo ya mambo wajibu kwao. Bidii na ustahimilivu wa bibi huyu mwema ulifanya elimu iwe rahisi kwa wasichana wengi.

Wanafunzi wote wa Bibi Nusrat Amin walikuwa wakiamini kwamba, ingawa Bibi Amin Esfahani alikuwa fakihi, alimu na mujtahidi, lakini juu ya yote alikuwa mtu wa mtu aliyebobea katika elimu ya irfani. Alikuwa akifungukiwa na mambo mengi ambayo baadhi yake ameyatolea ufafanuzii katika kitabu cha Nafhat al-Rahmaniya.

Hojjat al-Islam Nusrat Amin, ingawa alikuwa tajiri sana, lakini hakuithamini kabisa dunia, hakuwa mtu wa kupindukia sana au kuzembea sana na alijali na kuichunga sana nafsi. Alisema namna ya kutunza nafsi yako ni kujiwekea ahadi kwanza kila siku kwamba, kwa mfano, hutafanya dhambi fulani au kuepuka maovu fulani ya kimaadili, kisha mchana jihadhari na ahadi yako na hesabu mwisho wa siku umeshika agano kwa kiasi gani na ukikosea basi jilaumu.

Ingawa Hujjat al-Islam, Bibi Amin alikuwa mwanamke aliyekuwa amebobea kikamilifu katika elimu ya Irfan na alikuwa akiheshimu sana maadili na kuhifadhi staha na hijabu kwa wanawake, lakini hakuwahi kukwepa kuwa katika jamii. Kila alipoona ni muhimu, alijitokeza katika mikusanyiko ya kielimu, kidini na hadhara na kutoa hotuba ili kuelimisha mawazo ya watu, hotuba zake nyingi zilikuwa za kidini na kimaadili, na inaonyesha kujali kwake suala la kulinda maadili na utakasifu katika jamii na kuinua kiwango cha ufahamu wa watu.

Bibi huyu mpendwa na mujtahidi hatimaye aliaga dunia baada ya miaka 97 ya juhudi katika njia ya elimu. Hiyo ilikuwa 1983). Mwili wake mtakasifu ukazikwa huko Isfahan, na tangu wakati huo kaburi lake limekuwa sehemu ya watu wa elimu na uchamungu kufanya ziara.

Wapenzi wasikilizaji, muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati tukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya mfululizo huu.

Tags