Jul 11, 2016 23:09 UTC
  • Jumanne, Julai 12, 2016

Leo ni Jumanne tarehe 7 Mfunguo Mosi Shawwal 1437 Hijria sawa na 12 Julai 2016.

Siku kama hii ya leo miaka 1434 iliyopita kulipiganwa vita vya Uhud kando kando ya mlima wenye jina hilo kaskazini mwa mji wa Madina, kati ya Waislamu na Washirikina. Baada ya washirikina wa Kiquraishi kushindwa vibaya na Waislamu katika vita vya Badr walianzisha vita hivi vya Uhud kwa kuandaa jeshi la watu 3,000 waliokuwa na zana kamili kwa ajili ya vita hivyo, huku wapiganaji wa Kiislamu wakuwa 700 tu. Kabla ya kuanza kwa vita hivyo, Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w) aliwashauri masahaba zake juu ya namna atakavyopambana na Maquraishi na iliamuliwa kuwa vita hivyo vipiganwe nje ya mji wa Madina. Mwanzoni mwa vita hivyo, Waislamu walionekana kushinda, hata hivyo kufuatia kughafilika na baadhi yao kuasi amri ya Mtume (saw) aliyewataka kuendelea kubakia mlimani, Waislanu hao walishuka mlimani kwa tamaa za kupata ngawira hali iliyowafanya washirikina kuwashambulia Waislamu na kudhoofika nguvu na uwezo wao. Waislamu 70 waliuawa shahidi katika vita hivyo akiwemo Hamza ami yake Mtume (s.a.w). Hata hivyo washirikina hawakuweza kupata ushindi wa moja kwa moja na hivyo wakalazimika kurejea Makka.

Siku kama ya leo miaka 1305 iliyopita, kwa mara ya kwanza katika historia ya mapambano ya Waislamu, akiwa na jeshi kubwa la Kiislamu Twariq bin Ziyad aliweza kuingia Uhispania. Ushindi huo ulikuwa mwanzo wa maendeleo ya Waislamu barani Ulaya ambapo umeendelea hadi leo kufikia Ufaransa. Twariq bin Ziyad aliwasili Uhispania baada ya kuvuka lango bahari kati ya Morocco na Uhispania linalojulikana kwa jina lake mwenyewe yaani "Jabal Tariq." Mlango bahari huo unatumika kama njia ya mawasiliano kati ya Bahari za Atlantic na Mediterranean. Waislamu walitawala kwa karne nane huko Uhispania na kueneza mafunzo na utamaduni wa Kiislamu barani Ulaya baada ya kutekwa Andalusia, moja ya sehemu za Uhispania ya leo.

Siku kama ya leo miaka 198 iliyopita, alizaliwa Henry David Thoreau, msomi na mwanaharakati wa Kimarekani. David alikuwa akiheshimu mazingira asilia kama viumbe vya Mwenyezi Mungu na alisika kwa kuwa na akhlaqi na maadili mema. Henry David alikuwa akisisitiza kuwa, haifai kuangamiza maisha ya wanadamu kwa tamaa ya kufikia mali na fedha nyingi. Aidha mwanaharakati huyo, aliamini kuwa kama vile ambavyo serikali inavyomuadhibu mtu mkosefu, kadhalika inapotokea serikali hiyo ikashindwa kutekeleza wadhifa wake wa kiuongozi, basi wananchi nao wanatakiwa kuiondoa madarakani kwa uasi wa kijamii. Miongoni mwa athari muhimu za Henry David Thoreau ni pamoja na kitabu cha 'Uasi wa Kijamii' na alifariki dunia mwaka 1862.

Tarehe 12 Julai miaka 70 iliyopita, kundi la Kizayuni la Irgun lililipua mabomu katika Hoteli ya Mfalme Daud huko Baitul Muqaddas. Hoteli hiyo ilikuwa ikitumiwa sana na raia wa Palestina. Bomu lililokuwa limetegwa ndani ya hoteli hiyo liliripuka na kuuawa watu zaidi ya 200. Kuweko Wayahudi 15 miongoni mwa waliouawa katika mlipuko huo kunabainisha wazi namna Wazayuni wasivyothamini hata maisha ya Wayahudi ili kufikia malengo yao ya kujitanua na kuzusha hofu miongoni mwa Wapalestina.

Na siku kama ya leo miaka 10 iliyopita Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel kwa mara nyingine tena lilifanya mashambulizi ya anga na bahari huko Lebanon. Utawala wa Kizayuni ulifanya mashambulizi hayo kwa kisingizio cha kukamatwa mateka wanajeshi wake wawili na wapiganaji wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon kupitia oparesheni yake ya kujilinda. Tel Aviv ilifanya mashambulizi hayo ya kijeshi huko Lebanon ikiungwa mkono na Washington lengo lake kuu likiwa ni kuvunja uwezo wa kijeshi wa Hizbullah na kuipokonya silaha harakati hiyo inayohesabiwa kuwa nguvu kuu ya mapambano huko Lebanon mbele ya jeshi ghasibu la utawala wa Kizayuni.