Jul 13, 2016 01:43 UTC
  • Jumatano, Julai 13, 2016

Leo ni Jumatano tarehe 8 Shawwal 1437 Hijria sawa na tarehe 13 Julai 2016.

Siku kama ya leo miaka 1952 iliyopita, moto mkubwa ulitokea huko Roma mji mkuu wa utawala wa kifalme wa Rumi. Sehemu kubwa ya mji wa kihistoria na mkongwe wa Roma iliungua na wakazi wengi wa mji huo walipoteza maisha yao kutokana na moto huo. Moto huo ulikuwa kisingizio tosha kwa Nuren mtawala mmwagadamu wa Kirumi ambaye aliwauwa kwa umati watu zaidi ya laki moja na baadaye kuwatuhumu Wakristo kuwa ndio walioanzisha moto huo.

Tarehe 13 Julai miaka 245 iliyopita, baharia na nahodha mashuhuri wa Kiingereza aliyejulikana kwa jina la James Cook alikamilisha safari yake ya kitafiti na kielimu ya kuelekea The Great Southern Continent. Safari hiyo ilikuwa imeanza tarehe 26 Julai mwaka 1768. Safari hiyo ndefu iliishirikisha pia timu ya watalaamu wa elimu ya Sayansi Asilia au Natural Science kwa kimombo. Wataalamu hao walikuwa na nia ya kufanya utafiti wa kielimu kuhusiana na mimea pamoja na viumbe wanaopatikana katika maeneo hayo.

Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita inayosadifiana na 13 Julai 1971, watu wasiopungua 92 waliuawa akiwemo balozi wa Ubelgiji nchini Morocco, baada ya kutokea machafuko nchini humo. Machafuko hayo yalitokea baada ya kundi la waasi wa kijeshi kutoka chuo cha kijeshi cha Ahermoumou nchini Morocco waliposhambulia sherehe za kutimia miaka 42 ya kuzaliwa Mfalme Hassan wa Pili. Miongoni mwa majeruhi 133, alikuwemo Moulay Abdullah, ndugu wa mfalme wa Morocco.

Na miaka 113 iliyopita katika siku kama ya leo ambayo ni sawa na tarehe 8 Shawwal mwaka 1324 Hijria toleo la kwanza la gazeti la 'Majlis' lichapishwa nchini Iran. Gazerti hilo lilianzishwa na mtu aliyejulikana kwa jina la Mirza Sayyid Muhammad Sadiq Tabatabai. Mbali na gazeti hilo kuandika habari za ndani na nje ya nchi, liliakisi pia mazungumzo yote ya Majlisi ya Ushauri ya Iran yaani Bunge.