Jumamosi 16 Julai 2016
Leo ni Jumamosi tarehe 11 Mfunguo Mosi Shawwal 1437 Hijria sawa na tarehe 16 Julai mwaka 2016 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1440 iliyopita yaani miaka 3 kabla ya Hijra, Mtume Muhammad (S.A.W) alielekea katika mji wa Ta'if karibu na Makka kwa lengo la kuwalingania Uislamu watu wa kabila la Thaqif. Safari hiyo ya Mtume mtukufu ilifanyika katika kipindi ambacho alikuwa ameondokewa na ami yake na mlezi wake kipenzi Abu Twalib, jambo lililowafanya Maquraishi wa Makka wazidishe maudhi na manyanyaso dhidi ya Mtume Muhammad (S.A.W) na wafuasi wake. Hivyo ilitarajiwa kuwa, iwapo wakazi wa Ta'if wangeukubali Uislamu, mji huo ungeweza kuwa kituo na makazi salama kwa Waislamu waliokuwa wakidhulumiwa wa Makka. Hata hivyo viongozi wa kabila la Thaqif sio tu kwamba hawakumwamini Mwenyezi Mungu Mmoja na risala ya Mtume Muhammad (S.A.W), bali pia baadhi ya watu wa kabila hilo walimfanyia maudhi, dhihaka na kumjeruhi Mtume mtukufu. ***
Miaka 126 iliyopita katika siku kama ya leo, James Parkinson aligundua ugonjwa wa Parkinson na namna unavyotokea. Kwa sababu hiyo ugonjwa huo ulipewa jina la tabibu huyo. Dalili za ugonjwa huo ni kama vile kutetemeka sana na kwa muda mrefu kwa ulimi, kichwa na mikono na kushindwa kuvuta miguu wakati wa kutembea hususan katika kipindi cha uzeeni na pia kukakamaa misuli katika sehemu yoyote ya mwili. Ugonjwa wa Parkinson unasababishwa na baadhi ya matatizo katika ubongo na hadi kufikia sasa hakuna dawa mujarabu iliyopatikana kwa ajili ya kutibu maradhi hayo.
Miaka 71 iliyopita katika siku kama hii ya leo bomu la kwanza la nyuklia la Marekani liliripuliwa wakati wa majaribio. Marekani ilifanya jaribio hilo la bomu la nyuklia ili kujiandaa kuishambulia Japan kwa kutumia mabomu hayo. Wakati huo Japan ilikuwa ikipigana na madola makubwa na majeshi ya nchi waitifaki, ikiwemo Marekani. ***
Miaka 65 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Nepal iliyoko katika bara la Asia ilipata uhuru. Ushawishi na uingiliaji wa Uingereza huko Nepal mwanzoni mwa karne ya 19 Miladia, ulisababisha vita kati ya nchi mbili hizo ambapo mwishoni mwa kumalizika vita mwaka 1816, Uingereza ikalikoloni eneo kubwa la ardhi ya Nepal na kuiunganisha ardhi ya India pia na nchi hiyo.
Na katika siku kama ya leo miaka 8 iliyopita, harakati ya Hizbullah ya Lebanon kwa mara nyingine tena ilifanikiwa kupokea mateka watano na miili ya karibu mashahidi 200 wa Kilebanoni kutoka kwa utawala wa Kizayuni mkabala wa kukabidhi mabaki ya maiti za askari wawili wa Kizayuni. Ubadilishanaji huo wa miili na mateka hao ulifanyika kufuatia mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya pande mbili hizo kwa usimamizi wa serikali ya Ujerumani. Nukta ya kushangaza katika oparesheni hiyo ni kwamba vyombo vya usalama na ujasusi vya utawala wa Kizayuni hadi dakika ya mwisho havikuwa na habari kwamba wanajeshi wake wawili waliuawa mwanzoni mwa mapigano kati ya jeshi la utawala wa Kizayuni na wapiganaji wa Hizbullah. Shakhsia wengine kutoka makundi ya mapambano ya Lebanon pia walikuwa miongoni mwa mateka walioachiwa huru na utawala wa Kizayuni. Shakhsia muhimu zaidi kuliko wote alikuwa Samir Kuntar ambaye alipoteza karibu miaka 30 ya umri wake akiwa katika jela za utawala wa Kizayuni. ***