Jumatatu, Julai 22, 2024
Leo ni Jumatatu tarehe 16 Mfunguo Nne Muharram 1446 Hijria sawa na Julai 22, 2024 Milaadia.
Miaka 411 iliyopita katika siku kama ya leo, Mikhail Ramanov alikalia kiti cha utawala wa Russia na kwa utaratibu huo, utawala wa miaka 304 wa familia ya Ramanov ukawa umeanza nchini humo.
Miaka mitatu baada ya mashambulio ya vikosi vya Poland dhidi ya Russia, mmoja wa makamanda wa Kirusi alifanikwa kuvishinda vikosi hivyo na kuudhibiti mji wa Moscow. Baada ya jeshi la Poland kufukuzwa nchini humo, Mikhail Ramanov akashika hatamu za uongozi wa nchi hiyo. Katika kipindi cha utawala wa familia ya Ramanov, Russia ilipanuka lakini kwa upande wa uchumi haikupiga hatua kubwa.

Katika siku kama ya leo miaka 109 iliyopita, kulitokea vita maarufu vilivyojulikana kwa jina la Vita vya Isonzo.
Vita hivyo vilitokea sambamba na kujiri Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia. Vita vya Isonzo vilitokea katika maeneo ya milimani yaliyojulikana kwa jina hilo hilo nchini Italia.
Vita hivyo vilikuwa baina ya jeshi la Italia lililokuwa katika safu ya waitifaki na Austria iliyokuwa upande wa Ujerumani. Watu wapatao 70,000 wengi wao wakiwa ni Wataliano waliuliwa katika vita vyab Isonzo. Pamoja na hayo, jeshi la Italia lilipata ushindi dhidi ya jeshi la Austria katika vita hivyo.

Siku kama ya leo miaka 63 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 22 Julai 1961, yalianza mapigano makali kati ya majeshi ya Ufaransa na Tunisia, baada ya vikosi vya Ufaransa kuushambulia mji wa kihistoria wa Bizerte ulioko kaskazini mashariki mwa Tunisia.
Mara baada ya Tunisia kujitawala kutoka kwa mkoloni Mfaransa mwaka 1956, mkoloni huyo aliendelea kuikalia kwa mabavu bandari ya Bizerte, na kuifanya kuwa kambi ya jeshi la anga la nchi hiyo.
Hata hivyo majeshi ya Tunisia yalifanikiwa kuikomboa bandari hiyo kwenye mapigano hayo makali yaliyopelekea Watunisia 750 kuuawa.

Siku kama ya leo miaka 22 iliyopita, ndege za kivita za utawala wa Israel zilishambulia eneo la Ukanda wa Gaza huko Palestina, na kuua watu 16 na wengine 150 kujeruhiwa.
Shambulio hilo la kushtukiza lililofanyika usiku, liliua watoto 9 wasiokuwa na hatia yoyote. Hali kadhalika miongoni mwa waliouawa shahidi katika shambulizi hilo ni Sheikh Swalah Shahadah, mmoja wa makamanda wa Brigedi ya Izzuddin Qassam tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya kiislamu ya Palestina HAMAS ambaye aliuawa akiwa pamoja na mkewe na binti yake.

Miaka 21 iliyopita katika siku kama ya leo inayosadifiana na tarehe 22 Julai 2003, waliuawa Uday na Qusay watoto wa Saddam Hussein, dikteta wa zamani wa Iraq pambizoni mwa mji wa Mosul, kaskazini mwa Iraq.
Uday na Qusay wakiwa wamefuatana na maafisa wa ngazi za juu wa Iraq walitoroka mjini Baghdad baada ya majeshi ya Marekani na Uingereza kuishambulia nchi hiyo mwezi Aprili 2003.
Majeshi ya Marekani yalishambulia nyumba walimokuwa wamejificha watoto hao wa Saddam Hussein na kuwauwa pamoja na wasaidizi wao.
