Jumatatu tarehe 29 Julai 2024
Leo ni Jumatatu tarehe 23 Mfunguo Nne Muharram 1446 Hijria mwafaka na tarehe 29 Julai 2024.
Tarehe 8 mwezi Mordad kwa mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsia ni siku ya kumuenzi mwanafalsafa, arifu na msomi mkubwa wa Kiislamu Shahabuddin Sohravardi aliyepewa lakabu ya Sheikhul Ishraq.
Sheikhul Ishraq alizaliwa mwaka 549 Hijria karibu na mji wa Zanjan kaskazini magharibi mwa Iran. Alibobea haraka katika taaluma nyingi za Kiislamu za wakati huo hususan falsafa. Sheikh Sohravardi alifanya safari katika miji mbalimbali ya nchi za Kiislamu kwa ajili ya kutafuta elimu. Aliasisi mfumo mpya wa falsafa uliopewa jina la Ishraq.
Sheikhul Ishraq ameandika vitabu vingi kama vile "Hikmatul Ishraq", al Mabda wal Maad", na "Talwihat".
Katika siku kama ya leo miaka 237 iliyopita aliaga dunia Allamah Mulla Muhammad Mahdi Naraqi, mwanazuoni na msomi mkubwa wa Kiislamu.
Baada ya kuhitimu masomo yake ya awali nchini Iran, msomi huyo mkubwa alielekea Hauza ya Najaf nchini Iraq kwa lengo la kuzidisha elimu ya kidini na alipata elimu kwa walimu mashuhuri wa zama hizo. Baada ya hapo Allamah Mulla Mahdi Naraqi alianza kufanya utafiti, kufundisha na kuandika vitabu.
Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya Allamah Naraqi ni "Jamiul Sa'adat" na " Anisul Muwahhidin".
Katika siku kama ya leo miaka 141 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 29 Julai 1883, alizaliwa Benito Mussolini mwanasiasa, dikteta na mwasisi wa chama cha Kifashisti nchini Italia.
Ufashisti ni utawala wa kidikteta uliojikita katika kuleta aidolojia ya kibaguzi na kiutaifa, kuwakandamiza wapinzani na kupotosha itikadi na fikra za wananchi. Mwaka 1922 Mussolini alinyakua wadhifa wa uwaziri mkuu wa Italia, na hivyo udikteta kuendelea kutawala nchini humo.
Muda mfupi baadaye Mussolini alishirikiana na Adolph Hitler na kuandaa mazingira ya kuanza Vita vya Pili vya Dunia.
Siku kama ya leo miaka 67 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 29 Julai 1957, Umoja wa Mataifa ulianzisha Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA.
Lengo la kuanzishwa taasisi hiyo ya kimataifa, ni kusimamia shughuli zote za mitambo ya nyuklia na kuhakikisha kwamba miradi ya nyuklia duniani inatekelezwa kwa njia za amani na kutotumika kwa malengo ya kijeshi na utengenezaji wa silaha za mauaji ya halaiki.
Katika siku kama hii ya leo miaka 19 iliyopita, Haram ya maimamu wawili, Ali al Hadi na Hassan al Askakri (as) huko Samarra, nchini Iraq walikozikwa wajukuu hao wawili wa Mtume Muhammad (saw) iliharibiwa na Mawahabi wa Kitakfiri wenye mafungamano na al-Qaeda.
Magaidi wa kitakfiri, wakiongozwa na Abu Musab al Zarqawi, siku ya Jumatano, tarehe 23 ya Muharram 1427 mwendo wa saa 7:00 asubuhi, wakiwa wamevalia sare za askari wa Iraq, waliingia kwenye haram ya maimamu hao wawili na kuteka silaha za walinzi na pamoja na watumishi wa eneo hilo takatifu, na kulipua eneo hilo kwa kutumia milipuko ya TNT yenye uzito wa kilo 200.
Nguvu ya mlipuko huu ilikuwa kubwa sana kiasi kwamba baadhi ya vifaa na jengo hilo nje vilirushwa umbali wa nusu kilomita.
Na siku kama ya leo miaka 16 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Ali Akbar Faydh mashuhuri kwa jina la Ayatullah Mishkini.
Ayatullah Mishkini alisoma kwa wanazuoni wakubwa wa zama hizo kama Ayatullah Burujerdi na Imam Khomeini. Alikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kujiunga na harakati ya mapambano ya Imam Khomeini dhidi ya utawala wa Shah. Alitiwa nguvuni na kufungwa jela mara kadhaa sambamba na kubaidishwa.
Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Mishkini alishika nyadhifa mbalimbali na muhimu zaidi ni ile ya Mwenyekiti wa Baraza la Wanazuoni wanaomchagua Kiongozi Muadhamu na Kusimamia Kazi Zake. Aidha alimu huyo ameandika vitabu vingi.