Aug 11, 2024 04:19 UTC
  • Jumapili, 11 Agosti, 2024

Leo ni Jumapili 6 Mfunguo Tano Safar 1446 Hijria mwafaka na 11 Agosti 2024.

Katika siku kama ya leo miaka 812 iliyopita alizaliwa mwanafalsafa, mnajimu na tabibu mashuhuri wa Kiislamu Qutbuddin Mahmoud Shirazi katika mji wa Shiraz nchini Iran. Alianza kujifunza tiba akiwa bado mdogo na alianza kutibu wagonjwa katika moja ya hospitali za Shiraz baada ya kufariki dunia baba yake. Katika kipindi cha miaka kumi ya kazi ya utabibu, Qutbuddin Shirazi alitalii vitabu mbalimbali vya tabibu mwingine wa Kiislamu Bin Sina na vitabu vingine vya tiba na falfasa.Baada ya kuasisiwa kituo cha utafiti wa elimu ya nujumu katika eneo la Maraghe kaskazini magharibi mwa Iran, Qutbuddin Shirazi aliishi kipindi kirefu na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu Khaja Nasiruddin Tusi na kupata elimu ya nujumu.Katika kipindi chote cha umri wake, tabibu huyo wa Kiislamu alitembelea miji na nchi mbalimbali na kukutana na wasomi na maulamaa wa maeneo hayo. Ameandika vitabu vingi kikiwemo kile cha Jaamiul Usul.Alifariki dunia mwaka 710 Hijria. ***

Qutbuddin Mahmoud Shirazi

 

Tarehe 11 Agosti miaka 495 iliyopita Martin Luther alitangaza rasmi madhehebu ya Protestant. Uprotestanti ulianzishwa na Martin Luther kama harakati ya kidini katika karne ya 16 kwenye ulimwengu wa Kikristo kwa lengo la kufanya mageuzi ya kidini. Harakati hiyo ilianza dhidi ya kanisa Katoliki na udikteta wa viongozi wa madhehebu hiyo kuhusu suala la msamaha wa dhambi unaotolewa na makasisi na Papa. Martin Luther aliyekuwa Mjerumani alianza harakati hiyo ya uasi ndani ya kanisa Katoliki baada ya kufasiri Injili kwa lugha ya Kijerumani tofauti kabisa na amri ya Papa kwa lengo la kuvunjilia mbali taasubu za kimadhehebu za Kikatoliki.***

Martin Luther

 

Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita Haile Selassie, aliyekuwa mfalme wa Ethiopia alitia saini azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililokuwa na lengo la kuiunganisha Eritrea na Ethiopia. Ardhi ya Waislamu ya Eritrea ambayo hapo kabla ilikuwa ikikoloniwa na Italia, katika Vita vya Pili vya Dunia ilikaliwa kwa mabavu na Uingereza. Mwezi Disemba 1950 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliidhinisha Eritrea kuongozwa kwa mfumo wa shirikisho sambamba na kuunganishwa na Ethiopia. Hata hivyo kutokana na kwamba wananchi wengi wa Eritrea hawakuridhishwa na hatua hiyo pamoja na kupuuzwa haki zao na utawala wa Ethiopia, walizidisha upinzani dhidi ya utawala wa Addis Ababa na hatimaye kuanzisha harakati ya kupigania uhuru wa nchi yao mnamo mwaka 1960. Mwaka 1993 mapambano ya wananchi wa Eritrea yalizaa matunda ambapo walishiriki katika kura ya maoni na kupiga kura ya kujitenga na Ethiopia.  ****

Haile Selassie,

 

Katika siku kama ya leo miaka 64 iliyopita nchi ya Chad ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa na siku hii hutambuliwa kama siku ya kitaifa nchini humo. Mwishoni mwa karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20 wakoloni wa Ufaransa waliishambulia Chad na katika kipindi cha miaka mitatu wakaidhibiti ardhi yote ya nchi hiyo. Mwaka 1958 Ufaransa iliipa Chad hiari ya kujiongoza na miaka miwili baadaye na katika siku kama ya leo nchi hiyo ikapata uhuru kamili na kuchagua mfumo wa uongozi wa jamhuri. Nchi ya Chad inapakana na nchi za Libya, Cameroon, Sudan, Afrika ya Kati, Nigeria na Niger. *** 

 

Tags