Jumanne, Julai 19, 2016
Leo ni Jumanne tarehe 14 Mfunguo Mosi Shawwal 1437 Hijia sawa na Julai 19, 2016.
Miaka 37 iliyopita katika siku kama ya leo mapinduzi ya wananchi wa Nicaragua yalipata ushindi dhidi ya dikteta Anastasio Somoza wa nchi hiyo na muitifaki wake mkubwa yaani Marekani. Dikteta huyo kibaraka wa Marekani alichukua hatamu za uongozi wa Nicaragua mwaka 1967 na tangu wakati huo wimbi kubwa la upinzani lilianza kuenea nchini kote na katika America ya Kati dhidi ya kiongozi huyo. Mapambano ya silaha ya wapiganaji wa msituni ya Harakati ya Ukombozi wa Kitaifa ya Sandinista (FSLN) yaliyoanza mwaka 1963 yalipamba moto zaidi katikati ya muongo wa 1970 na kuungwa mkono na wananchi. Hatimaye Somoza alilazimika kukimbia nchi baada ya jeshi la Sandinista kuingia Managua mji mkuu wa Nicaragua katika siku kama ya leo. Karibu watu elfu 40 waliuawa katika mapinduzi ya Nicaragua.
Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, Kuwait iliondokana na ukoloni wa Uingereza. Katika kipindi cha utawala wa Achaemenid, Kuwait ilikuwa ikihesabiwa kuwa sehemu ya ardhi ya Iran. Mwaka 1899 Miladia, Kuwait iliwekeana saini na Uingereza, suala lililoifungulia London mlango wa kuikoloni nchi hiyo. Mwenendo huo uliendelea hadi baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Kuwepo kwa visima vya mafuta kulipanua uingiliaji mkubwa wa mashirika mengi ya Uingereza na Marekani katika taifa hilo. Hatimaye mwaka 1961 Kuwait na Uingereza zilitiliana saini makubaliano yaliyoifanya nchi hiyo kujipatia uhuru wake.
Miaka 123 iliyopita alizaliwa malenga wa Russia kwa jina la Vladimir Mayakovsky. Mashairi ya Mayakovsky yalikuwa na nafasi kuu wakati wa mapinduzi ya Kikomonisti ya Urusi ya zamani mwaka 1917. Vladimir Mayakovsky alikuwa akiamini kuwa fasihi inapasa kuwa lugha ya watu wengi na inayobainisha maisha yao ya kijamii.
Na siku kama ya leo miaka 864 iliyopita alifariki dunia Qutbud-Din Rawandi, faqihi wa karne ya sita Hijria ambaye pia alikuwa mtaalamu wa hadithi na mtaalamu wa elimu ya aqida ya Kiislamu. Kwa miaka mingi alikwenda kwa wasomi wakubwa wa zama zake na kupata utaalamu mkubwa wa elimu za fiq'hi, hadithi na tafsiri ya Qur'ani Tukufu. Zipo athari kadhaa za msomi huyu mkubwa zinazokaribia vitabu 80 ambavyo miongoni mwake ni kitabu kiitwacho "Tafsirul Qur'an", "Risaalatul-Fuqahaa", "Aayaatul-Ahkaam" na "Asbaabun-Nuzul."
Na siku kama ya leo miaka 29 iliyopita Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio lililohusu udharura wa kusitishwa vita kati ya Iraq na Iran. Azimio ni miongoni mwa mazimio nadra yaliyopasishwa kwa sauti moja na wanachama wote watano wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika historia ya umoja huo.