Sep 30, 2024 02:23 UTC
  • Jumatatu, tarehe 30 Septemba, 2024

Leo ni Jumatatu tarehe 26 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe 30 Septemba 2024.

Siku kama ya leo miaka 1,102 iliyopita yaani tarehe 26 Rabiul Awwal mwaka 344 Hijiria alifariki dunia Ibn Sammak, mtaalamu mkubwa wa masuala ya itikadi ya Kiislamu huko Baghdad.

Historia haijaweka wazi tarehe na mahala alipozaliwa msomi huyo, lakini ripoti zinasema kwamba aliishi mjini Baghdadi, Iraq na kupata elimu na maarifa kwa wasomi wa mji huo. Vilevile historia inasema Ibn Sammak alilea wasomi wengine mashuhuri akiwemo Haakim Nishaburi.

Miongoni mwa vitabu vya Ibn Sammak ni kile cha "al Aamali" na vitabu vingine kadhaa kuhusu fadhila na matukufu ya Ahlulbait wa Mtume Muhammad (saw).

Siku kama ya leo miaka 86 iliyopita, ulifayika mkutano wa kihistoria wa Munich nchini Ujerumani.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Adolph Hitler na Benito Mussolini viongozi wa Ujerumani na Italia na pia Neville Chamberlain na Edouard Daladier, Mawaziri Wakuu wa wakati huo wa Ufaransa na Uingereza. Mkutano huo wa Munich ulifanyika kwa shabaha ya kutafuta njia ya kumaliza hitilafu kati ya Ujerumani na Czechoslovakia.

Mkutano huo ulimalizika kwa kufikiwa makubaliano ya kuiunganisha sehemu moja ya ardhi ya Czechoslovakia na Ujerumani.   

Mkutano wa kihistoria wa Munich

Siku kama ya leo miaka 58 iliyopita yaani tarehe 30 mwezi Septemba mwaka 1966, nchi ya Botswana ilijipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza.

Botswana ilianza kukoloniwa na Uingereza mwaka 1885 Miladia. Harakati za wananchi wa Botswana za kuikomboa nchi yao zilishtadi tangu mwaka 1920 na kupelekea kupatikana uhuru wa nchi hiyo mwaka 1966.

Nchi ya Bostwana iko kusini mwa bara la Afrika ikipakana na Afrika Kusini, Zimbabwe na Namibia.

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, alifariki dunia mvumbuzi wa kipimo kinachotumiwa kupimia nguvu ya mtetemeko wa ardhi Charles Richter.

Akishirikiana na mhakiki mwingine, Richter alipima mtetemeko huo kwa mujibu wa nishati inayotokana na mawimbi ya mitetemeko ya ardhi toka daraja moja hadi 9 na kusajili kipimo cha Rishta.

Kabla ya hapo wataalamu walikuwa wakipima mitetemeko ya ardhi kwa kutegemea athari ya nje ya kipimo ambacho hakikuwa cha kuaminika.

Charles Richter

Na leo tarehe 30 Septemba ni Siku ya Kimataifa ya Viziwi. Lengo la siku hii kupewa jina hilo ni kutaka kuimarisha utamaduni wa kuwa na mawasiliano na watu wenye ulemavu huo, kustawisha maarifa ya lugha ya ishara na kuwazindua wanasiasa na watu wa kawaida kuhusu matatizo ya watu wa tabaka hilo.

 

Tags