Jul 22, 2016 04:25 UTC
  • Ijumaa, Julai 22, 2015

Leo ni Ijumaa tarehe 17 Shawwal 1437 Hijria sawa na 22 Julai, 2016.

Siku kama ya leo miaka 13 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 22 Julai 2003, waliuawa Uday na Qusay watoto wa Saddam Hussein, dikteta wa zamani wa Iraq pambizoni mwa mji wa Mosul, kaskazini mwa Iraq. Uday na Qusay wakiwa wamefuatana na maafisa wa ngazi za juu wa Iraq walitoroka mjini Baghdad baada ya majeshi ya Marekani na Uingereza kuishambulia nchi hiyo mwezi Aprili 2003. Majeshi ya Marekani yalishambulia nyumba walimokuwa wamejificha watoto hao wa Saddam Hussein na kuwauwa pamoja na wasaidizi wao.

Tarehe 22 Julai 2002, ndege za kivita za utawala wa Israel zilishambulia eneo la Ukanda wa Gaza huko Palestina, na kuua watu 16 na wengine 150 kujeruhiwa. Shambulio hilo la kushtukiza lililofanyika usiku, liliua watoto 9 wasiokuwa na hatia yoyote. Hali kadhalika miongoni mwa waliouawa shahidi katika shambulizi hilo ni Sheikh Swalah Shahadah, mmoja wa makamanda wa Brigedi ya Izzuddin Qassam akiwa pamoja na mke na binti yake.

Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 22 Julai 1961, yalianza mapigano makali kati ya majeshi ya Ufaransa na Tunisia, baada ya vikosi vya Ufaransa kuishambulia bandari maarufu ya Bizerte iliyoko kaskazini mashariki mwa Tunisia. Mara baada ya Tunisia kujitawala kutoka kwa mkoloni Mfaransa mwaka 1956, mkoloni huyo aliendelea kuikalia kwa mabavu bandari ya Bizerte, na kuifanya kuwa kambi ya jeshi la anga la nchi hiyo. Hata hivy o majeshi ya Tunisia yalifanikiwa kuikomboa bandari hiyo kwenye mapigano hayo makali yaliyopelekea Watunisia 750 kuuawa.

Na tarehe 17 Shawwal mwaka wa 5 Hijria, yaani siku kama hii ya leo miaka 1432 iliyopita vilitokea vita vya Khandak vilivyopiganwa pambizoni mwa mji wa Madina. Wakati huo, washirikina wa Makka pamoja na wafuasi wa makabila mengine kadhaa yalioongozwa na Abu Sufiyan, walielekea Madina. Mara baada ya Mtume Mtukufu SAW kupata habari za shambulio la maadui, alishauriana na masahaba zake na hatimaye kufikia uamuzi wa kuchimbwa mahandaki pambizoni mwa mji huo, kutokana na ushauri uliotolewa na Salman Fars.

Kwenye vita hivyo vya Khandak, majeshi ya Kiislamu yalijipatia ushindi mkubwa, na Abu Sufiyan pamoja na washirika wake walishindwa na kulazimika kurejea Makka.

 

 

 

 

Tags