Oct 16, 2024 15:19 UTC
  • Jumatano, tarehe 16 Oktoba, 2024

Leo ni Jumatano tarehe 12 Mfunguo Saba Rabiuthani 1446 Hijria sawa na Oktoba 16 mwaka 2024.

Siku kama ya leo miaka 1314 iliyopita, yaani tarehe 12 Mfunguo Saba Rabiuthani mwaka 132 Hijria, Abul Abbas Abdullah bin Muhammad maarufu kwa jina la 'Saffah' alikalia kiti cha uongozi akiwa khalifa wa kwanza wa kizazi cha Bani Abbasi.

Utawala huo wa Kiabbasi kwa kushirikiana na Abu Muslim Khorasani na majeshi yake, ulimuuwa Marwan wa Pili, mtawala wa mwisho wa ukoo wa Bani Umayyah na kuondoa madarakani utawa wao.

Bani Abbas nao kama walivyokuwa watawala wa Bani Umayyah, waliwakandamiza raia na Ahlubaiti wa Mtume Muhammad (saw) na kufanya dhulma kubwa, na utawala wao uliendelea kushika madaraka katika ulimwengu wa Kiislamu hadi mwaka 656 Hijria.

Siku kama ya leo miaka 231 iliyopita, yaani tarehe 16 Oktoba mwaka 1793, aliuawa kwa kukatwa kichwa kwa shoka, malikia wa Ufaransa, Marie Antoinette, kwa amri ya Baraza la Katiba la nchi hiyo na pia amri ya Maximilien Robespierre.

Louis wa 16 aliyekuwa mume wa  Antoinette, miezi 10 kabla ya hapo alikuwa tayari amepatwa na hatma hiyo hiyo iliyomkuta mke wake. Marie Antoinette alikuwa binti wa Maria Theresa Walburga, mtawala wa Austria na Ufaransa. Antoinette aliolewa na Louis, mrithi wa kiti cha ufalme wa Ufaransa, mnamo mwaka 1770 akiwa na umri wa miaka 14. Hatua ya Louis ya kumuoa mwanamke huyo ilikuwa na nia ya kuzikurubisha pamoja nchi za Austria na Ufaransa ambazo wakati huo zilikuwa zikishindana barani Ulaya.

Hata hivyo Wafaransa wengi hawakuridhia ndoa hiyo kiasi cha kuwafanya kuendelea kumwita ‘Muaustria’ hata kipindi alipokuwa tayari ni malikia wa Ufaransa. 

Marie Antoinette

Katika siku kama ya leo miaka 170 iliyopita alizaliwa Oscar Wilde mwandishi mashuhuri Dublin huko Ireland.

Oscar Wilde alipata elimu ya msingi katika mji wa Skyline kaskazini mwa Ireland na akajiunga na chuo kikuu cha Trinity na baadaye Oxford. Oscar Wilde alipata umaarufu baada ya kuandika mfululizo wa vitabu vya kisa cha Mwanamfalme Mwenye Furaha (The Happy Prince).

Oscar Wilde

Siku kama ya leo miaka 79 iliyopita liliasisiwa Shirika la Chakula Duniani (FAO).

Hati ya kuasisiwa shirika hilo ilipasishwa Oktoba 16 mwaka 1945 katika mji wa Québec nchini Canada. Lengo ya kuasisiwa shirika la FAO ni kuzisaidia nchi wanachama kukusanya taarifa, ripoti na takwimu zinazohusiana na chakula, kilimo, utunzaji wa misitu na uvuvi na kufanya tathmini kuhusu uzalishaji wa chakula, ugavi wake na juhudi za kuboresha uzalishaji, masoko ya chakula, kulinda maliasili, kupanga sera zinazohusiana na kilimo na chakula na kadhalika.

Siku hii pia inatambuliwa kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Chakula.   

Miaka 78 iliyopita katika siku kama ya leo, mwafaka na tarehe 16 Oktoba 1946, kwa mujibu wa hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Nuremberg walinyongwa viongozi 10 wa Ujerumani ya utawala wa Kinazi baada ya kupatikana na hatia za kutenda jinai za kivita.

Herman Goering aliyekuwa Kamanda Mkuu wa kikosi cha Jeshi la Anga la Ujerumani na msaidizi wa dikteta Adolphe Hitler ambaye alikuwa amehukumiwa adhabu ya kifo, pia aliamua kujinyonga yakiwa yamebakia masaa machache kabla ya kutekelezwa hukumu hiyo ya kifo.

Hali kadhalika mahakama hiyo iliwahukumu adhabu ya kifungo cha muda mrefu viongozi wengine 9 wa Ujerumani ya Wanazi na wengine watatu hawakupatikana na hatia.

Mahakama ya Nuremberg iliyoundwa na wawakilishi wa Marekani, Urusi ya zamani, Uingereza na Ufaransa kwa shabaha ya kuwahukumu maafisa 22 wa Manazi wa Ujerumani kwa tuhuma za kufanya jinai za kivita ilikamilisha shughuli zake tarehe 30 Septemba mwaka 1946. ***

Tags