Jumatano, 13 Novemba, 2024
Leo ni Jumatano tarehe 11 Jamadil Awwal 1446 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 13 Novemba 2024.
Siku kama ya leo miaka 1064 iliyopita alifariki dunia Ali bin Isa Rumani, mtaalamu mkubwa wa elimu ya nahwu na fasihi ya Kiarabu.
Bin Issa mbali na kutabahari katika elimu ya fasihi ya Kiarabu, alikuwa pia mtaalamu wa elimu za fiqhi, teolojia, na sayansi ya Qur’ani.
Miongoni mwa vitabu muhimu vya mwanazuoni huyo ni kile cha ‘I’jaazul-Qur’an’.
Siku kama ya leo miaka 849 iliyopita, alizaliwa Nasiruddin Tusi, mwanafalsafa, mtaalamu wa hesabati na nujumu na msomi mkubwa wa Kiislamu huko katika mji wa Tusi, kaskazini mashariki mwa Iran.
Nasiruddin Tusi aliishi katika kipindi cha Hulagu Khan Mongol na mwanaye na kuasisi kituo kikubwa na cha kwanza cha sayansi ya nujumu huko Maraghe. Kituo hicho kiliasisiwa mwaka 657 Hijria, huko kaskazini magharibi mwa Iran.
Nasiruddin Tusi ameandika vitabu zaidi ya 80 kwa lugha za Kiarabu na Kifarsi. Vitabu muhimu zaidi vya msomi huyo ni pamoja na ‘Asasul-Iqtibaas’, ‘Akhlaaqe Naasiri’, ‘Awswaful-Ashraaf’ na ‘Sharhul Ishaarat.
Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita hayati Hafidh Assad alichukua hatamu za uongozi wa Syria baada ya mapinduzi ya kijeshi mwaka 1970 na baadaye akachaguliwa kuwa kiongozi wa chama cha Baath.
Hafidh Assad alizaliwa mwaka 1930 na mwaka 1964 alichaguliwa kuwa kamanda wa kikosi cha anga cha jeshi la Syria. Miaka mitatu baadaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo.
Hafidh Assad alifariki dunia mwezi Juni mwaka 2000 baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Miaka 54 iliyopita katika siku kama ya leo, mwafaka na tarehe 13 Novemba 1970, tufani kubwa na kimbunga cha kutisha kiliikumba nchi ya Bangladesh.
Janga hilo lilitokea wakati mapambano ya Wabangali kwa ajili ya kujitenga na Pakistan na kupata uhuru yalipokuwa kileleni. Tufani hiyo kubwa ilisababisha vifo vya watu laki mbili na kujeruhi wengine laki nane. Kimbunga na tufani hiyo pia iliwalazimisha mamia ya maelfu ya watu kukimbia makazi yao na kusababisha hasara kubwa katika mashamba, viwanda, makazi ya raia na miundombinu ya nchi hiyo.
Bangladesh ni miongoni mwa nchi zinazokumbwa na majanga ya kimaumbile kama vimbunga, tufani na mafuriko ya mara kwa mara. ***
Na miaka 9 iliyopita tarehe 13 Novemba saa tatu na dakika 16 usiku kwa wakati wa Ulaya ya Kati, milipuko kadhaa ya kigaidi ilitokea katika vitongoji nambari 1, 10 na 11 vya jiji la Paris nchini Ufaransa na kuua watu 130 na kujeruhiwa wengine 368.
Baadhi ya milipuko hiyo ilitokea karibu na uwanja wa michezo wa Stade de France ulioko kaskazini mwa jiji la Paris wakati wa mechi ya mpira wa miguu kati ya timu za taifa za Ufaransa na Ujerumani. Wakati huo huo watu wengine 87 waliuawa katika utekeji nyara uliofanyika katika ukumbi wa michezo ya kuigiza wa Bataclan mjini Paris.
Mashambulizi hayo yalihesabiwa kuwa makubwa zaidi kutokea nchini Ufaransa baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Siku moja baadaye kundi la kigaidi la Daesh lilitangaza kuwa ndilo lililohusika na mashambulizi hayo.