Nov 15, 2024 02:24 UTC
  • Ijumaa, tarehe 15 Novemba, 2024

Leo ni Ijumaa tarehe 13 Mfunguo Nane Jamadil-Awwal 1446 Hijria ambayo inasafidiana na tarehe 15 Novemba 2024.

Siku kama ya leo miaka 1435 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria na kwa mujibu wa baadhi ya riwaya, Bibi Fatimatu Zahra binti wa Mtume Muhammad (saw) alikufa shahidi baada ya kuishi maisha mafupi lakini yaliyojaa mafunzo makubwa ya kimaadili na kimaanawi.

Baba yake ni Mtume Muhammad (saw) na mama yake ni Bibi Khadija Binti Khuwaylid (as). Bibi Fatima alishiriki katika medani mbalimbali za mapambano mwanzoni mwa kudhihiri Uislamu akiwa bega kwa bega na baba yake, Mtume Muhammad (saw), Imam Ali bin Abi Talib pamoja na watoto wake wema, yaani Imam Hassan na Hussein (as) ambao Mtume amewataja kuwa ni vinara wa mabarobaro wa peponi.

Bibi Fatima alisifika kwa tabia njema, uchamungu, elimu na maarifa, na alikuwa mfano na kigezo chema cha mwanamke na Waislamu kwa ujumla.

Katika siku kama ya leo miaka 1374 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Ibrahim bin Malik al Ashtar mmoja wa makamanda na mashujaa wa Uislamu aliuawa katika vita na jeshi la Bani Umayyah.

Alikuwa mtoto wa Malik al Ashtar, Swahibi na kamanda wa jeshi la Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as). Ibrahim alikuwa pamoja na baba yake katika kipindi cha ujana katika vita vya Siffin na alionesha ushujaa mkubwa dhidi ya jeshi la Muawiyyah. 

Ibrahim Malik Ashtari aling'ara zaidi katika harakati iliyoanzishwa na Mukhtar Thaqafi huko Kufah dhidi ya utawala dhalimu wa bani Umayyah. Harakati hiyo ilianzishwa kwa lengo la kulipiza kizazi cha damu ya Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) pamoja na masahaba zake waliouawa katika tukio la Karbala mwaka 61 Hijria.

Siku kama ya leo miaka 394 iliyopita, alifariki dunia Johannes Kepler, mwanahisabati, mnajimu na mtaalamu wa nyota wa Kijerumani.

Kepler alizaliwa mwaka 1517 na baada ya kuhitimu masomo yake alielekea Austria na kuanza kufundisha. Baadaye Kepler alifahamiana na Tycho Brahe, mnajimu mtajika wa Denmark na kuanzia hapo taratibu akavutiwa na elimu ya nyota kutoka kwa msomi huyo. Kepler alichunguza na kufanya utafiti katika uwanja huo kwa miaka mingi.   

Johannes Kepler

Siku kama ya leo, miaka 154 iliyopita, alizaliwa Vasily Bartold, mustashiriki maarufu wa Russia huko Saint Petersburg.

Bartold alisoma na kuhitimu elimu katika chuo kidogo cha lugha za Mashariki huko huko Saint Petersburg na kuwa hodari katika lugha za Kifarsi, Kiarabu na Kituruki. Akiwa na umri wa miaka 27, alifikia daraja la mhadhiri msaidizi katika chuo hicho kuifundisha historia ya mataifa ya Mashariki. Alifanya utafiti mkubwa katika uwanja huo. Aidha kwa kipindi fulani alifanya safari huko Turkestani kwa minajili ya kuendeleza utafiti wake na kubahatika kuandika utafiti huo katika kitabu chake alichokipa jina la 'Turkestani katika kipindi cha mashambulizi ya Mongoli.'   *

Vasily Bartold

Miaka 44 iliyopita katika siku kama leo mji wa mpakani wa Susangerd huko kusini magharibi mwa Iran ulishuhudia mapambano kati ya wapiganaji wa Kiislamu na wanajeshi vamizi wa utawala wa zamani wa Iraq.

Oparesheni hiyo ya kujihami ilifanywa na wapiganaji shupavu 200 wa Iran waliojumuisha wanajeshi wa ulinzi, wanamgambo wa kujitolea na idadi ya kadhaa ya wenyeji wa mji huo waliokuwa wakitumia silaha nyepesi dhidi ya jeshi vamizi la Saddam.

Katika operesheni hiyo wapiganaji shupavu wa Iran chini ya uongozi wa shahidi Dakta Mustafa Chamran, walipambana vikali na kufanikiwa kuukomboa mji wa Susangerd.

Tarehe 15 Novemba mwaka 1988 lilitolewa tangazo la kuundwa taifa huru la Palestina, na siku hiyo ikapewa jina la Siku ya Uhuru wa Nchi Palestina.

Katikati ya Novemba 1988, Baraza la Kitaifa la Palestina, ambalo lilianzishwa mwaka mmoja kabla, lilifanya mkutano nchini Algeria na kutangaza uwepo wa "nchi huru ya Palestina" mnamo Novemba 15, 1988. Baitul Muqaddas pia iliteuliwa kuwa mji mkuu wa nchi hiyo. Siku 10 baada ya mkutano huo, nchi 54 za dunia zilitambua kuwepo kwa taifa huru la Palestina.

Hata hivyo kuna vikwazo vingi vya ya kuweko utawala wa taifa huru la Palestina katika ardhi ya taifa hilo, kubwa zaidi ni utawala wa Kizayuni wa Israel. 

Siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, Allamah Muhammad Taqi Ja'fari, mwanafalsafa na mwanafikra mkubwa wa Kiislamu, aliaga dunia.

Alizaliwa mwaka 1304 Hijria Shamsia katika mji wa Tabriz kaskazini magharibi mwa Iran. Kipaji chake kilidhihiri na kuchomoza tangu akiwa katika kipindi cha kuinukia kwake ambapo kabla ya kuanza shule ya msingi tayari alikuwa amejifunza Qur'ani. Akiwa shule alionekana mwenye kipaji mno. Hata hivyo umasikini ulimfanya aache shule na kuanza kufanya kazi.

Pamoja na kufanya kazi aliutumia muda wake wa ziada kusoma masomo ya dini. Allama Muhammad Taqi Ja'fari ameandika vitabu vingi ambapo Tarjuma na Tafsiri ya Nahajul Balagha ndio kitabu muhimu zaidi cha mwanazuoni huyo. 

Katika siku kama ya leo miaka 24 iliyopita aliaga dunia Muislamu wa Italia, Mahdi Edoardo Agnelli.

Edoardo Agnelli alikuwa mtoto wa kiume wa pekee wa seneta mashuhuri wa Italia na mmiliki wa kiwanda cha magari ya Fiat, Gianni Agnelli. Alizaliwa mwaka 1954 katika mji wa New York nchini Marekani na akahitimu chuo kikuu katika taaluma ya dini na falsafa za Mashariki. Alipokuwa na umri wa miaka 20, Edoardo Agnelli alipata kitabu cha Qur'ani kwa sadfa katika maktaba za Marekani na akaikumbatia dini tukufu ya Uislamu baada ya kufanya uchunguzi kuhusu dini hiyo. Alichagua jina la Hisham Aziz na baadaye kidogo alikhitari kufuata madhehebu ya Ahlulbait na kubadili jina lake na kuwa Mahdi Edoardo Agnelli.

Miaka ya awali ya baada ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Edoardo Agnelli alifanya safari nchini Iran na kukutana na Imam Ruhullah Khomeini. Kusilimu mtoto huyo wa seneta wa Italia, mmiliki wa kiwanda cha magari ya Fiat na klabu ya soka ya Juventus kulitambuliwa kuwa kosa kubwa kwa familia yake kiasi kwamba alitishiwa kuwa atanyimwa urithi kwa kosa hilo.

Alikuwa akisema mara kwa mara kwamba anahofia kuuliwa na Wazayuni. Hatimaye tarehe 15 Novemba mwaka 2000 maiti ya Mahdi Edoardo Agnelli ilikutwa chini ya daraja moja la mji wa Turin nchini Italia ikiwa na alama za kupigwa na kujeruhiwa. Maiti yake ilizikwa harakaharaka bila ya kufanyiwa uchunguzi wa kubaini sababu ya kifo chake kilichotokea katika mazingira ya kutatanisha. 

Mahdi Edoardo Agnelli

Na miaka 24 iliyopita sawa na tarehe 25 Aban 1379 Hijria Shamsia, aliaga dunia Hujjatul Islam, Dakta Muhammad Hadi Amini Najafi, mmoja wa maulama na waandishi mahiri wa Kiirani.

Alizaliwa Tabriz kaskazini magharibi mwa Iran, na katika kipindi cha ujana wake alielekea huko Najaf, Iraq akiwa pamoja na baba yake, Allama Amini, mwandishi wa kitabu mashuhuri cha al-Ghadir. Msomi huyo alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha al-Azhar nchini Misri.

Mwaka 1350 Hijria Shamsia Dakta Muhammad Hadi Amini Najafi alirejea nchini Iran na kuanza kufanya kazi ya uandishi, kufundisha na kufanya uhakiki. 

Dakta Muhammad Hadi Amini Najafi