Jumanne, Julai 26, 2016
Leo ni Jumanne tarehe 21 Shawwal 147 Hijria sawa na tarehe 26 Julai 2016.
Siku kama ya leo miaka 1345 iliyopita, Jeshi la Waislamu, likiongozwa na Twariq bin Ziyad liliidhibiti Uhispania. Ushindi huo ulikuwa mwanzo wa maendeleo ya Waislamu barani Ulaya ambapo umeendelea hadi leo kufikia Ufaransa. Twariq bin Ziyad aliwasili Uhispania baada ya kuvuka lango bahari kati ya Morocco na Uhispania linalojulikana kwa jina lake mwenyewe yaani "Jabal Tariq." Mlango bahari huo unatumika kama njia ya mawasiliano kati ya Bahari za Atlantic na Mediterranean. Waislamu walitawala kwa karne nane huko Uhispania na kueneza mafunzo na utamaduni wa Kiislamu barani Ulaya baada ya kutekwa Andalusia, moja ya sehemu za Uhispania ya leo.
Miaka 1083 iliyopita katika siku kama hii ya leo, alifariki dunia Ibn Habban, mtaalamu wa hadithi, elimu ya fiq'hi na mwanahistoria mashuhuri wa karne ya 14 Hijiria. Alipata elimu ya msingi kwa walimu mashuhuri wa zama zake na kisha akaelekea Neishabur kaskazini mwa mashariki mwa Iran, ambao katika kipindi hicho ulikuwa ni moja ya vituo muhimu vya elimu. Ibn Habban anahesabika kuwa mtu mwenye nadharia muhimu katika elimu ya hadithi. Miongoni mwa athari muhimu za msomi huyu mkubwa ni pamoja na kitabu cha"At-Thuqat" na Rawdhatul-Uqalaai wa Nuzhatul-fudhalaai."
Siku kama ya leo miaka 169 iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Liberia ilipata uhuru wake na siku hiyo hutambuliwa nchini humo kama siku ya kitaifa. Liberia iko katika mwambao wa bahari ya Atlantic huku ikipakana na nchi za Guinea, Sierra Leone na Ivory Coast. Idadi kubwa ya raia wa taifa hilo lenye jumla ya watu milioni tatu wanafuata dini za kitamaduni na kimila, huku asilimia 16 ya raia wake ikiundwa na Waislamu. Lugha rasmi ya raia wa Liberia ni Kingereza huku wakitumia kuandika kwa herufi za Kilatini. Mwaka 1822 Miladia na kwa uungaji mkono wa serikali ya Marekani, ilifikia uhuru kwa ajili ya Wamarekani weusi na mji wake mkuu Monrovia, ukijengwa kwa amri ya rais wa wakati huo wa Marekani. Mwaka 1841 nchi hiyo iliandika katiba na kuitwa kubadili jina lake kuwa Liberia likiwa na maana ya ardhi ya watu walio huru. Hatimaye mwaka 1847, nchi hiyo ikatangaza uhuru wake kutoka mikononi mwa Marekani.
Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, yaani tarehe 26 Julai mwaka 1979 Zuheir Muhsein, Katibu Mkuu wa wakati huo wa Harakati ya as-Sa'iqa tawi la Harakati ya Ukombozi ya Palestina (PLO) aliuawa kigaidi na maajenti wa shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni (Mossad) huko katika mji wa Cannes nchini Ufaransa. Magaidi wa Kizayuni walikimbia na kutoweka baada ya kufanya mauaji hayo na polisi wa Ufaransa wakidai kuwa hawakupata uthibitisho kwamba Mossad ilihusika na mauaji hayo.
Miaka 60 iliyopita katika siku kama ya leo, Gamal Abdu l-Nasser Rais wa wakati huo wa Misri aliitangaza kuutaifisha Mfereji wa Suez. Mfereji huo ulianzishwa mwaka 1896 baada ya Misri kukaliwa kwa mabavu na Uingereza na kwa utaratibu huo, njia ya baharini baina ya Ulaya na Asia ikawa imefupishwa. Udhibiti wa Uingereza na Ufaransa kwa Mfereji wa Suez uliendelea hadi serikali ya Abdu l-Nasser ilipokuja kuutaifisha na kuutangaza kuwa mali ya taifa. Hatua hiyo ilifuatiwa na mashambulio ya kijeshi ya Uingereza, Ufaransa na utawala dhalimu wa Israel. Hata hivyo mashinikizo ya kimataifa dhidi ya madola vamizi na mapambano ya wananchi Waislamu wa Misri, yalivifanya vikosi vamizi viondoke katika kanali hiyo muhimu na mfereji huo ukawa katika miliki ya serikali na taifa la Misri.
Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita katika siku kama ya leo mwafaka na tarehe 5 Mordad mwaka 1358 Hijria Shamsiya, Swala ya kwanza ya Ijumaa katika mji wa Tehran baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ilisaliwa katika Chuo Kikuu cha Tehran ikiongozwa na marehemu Ayatullah Talaqani, mmoja wa maulamaa wakubwa wa Kiislamu, kufuatia agizo la Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini, Swala ya Ijumaa haikuwa ikifanyika kutokana na kuweko anga ya udhibiti na ukandamizaji wa serikali ya Shah.
Na siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, Muhammad Reza Pahlavi mfalme wa mwisho wa Iran aliaga dunia huko Cairo, Misri. Aliingia madarakani baada ya baba yake yaani Rezakhan kuondolewa kwenye uongozi na kubaidishwa na Waingereza. Kama alivyokuwa baba yake, Muhammad Reza Pahlavi alikuwa na uhusiano mkubwa na Uingereza na ndio maana akafanya jitihada za kulinda maslahi haramu ya nchi hiyo nchini Iran. Hata hivyo baada ya harakati za wananchi na kushinda harakati ya kuitaifisha sekta ya mafuta, maslahi ya Waingereza nchini Iran yalifikia tamati. Shah aliwakandamiza wananchi wa Iran kwa ngumi ya chuma na alikuwa kibaraka mkubwa wa Marekani. Suala hilo lilizidisha kasi ya harakati za Mapinduzi ya Kiislamu zilizoongozwa na hayati Imam Khomeini na mwaka 1357 Mapinduzi ya Kiislamu yalihitimisha utawala dhalimu wa Shah ambaye alikimbilia nje ya nchi na kufia Misri katika siku kama hii ya leo.