Jul 31, 2016 01:41 UTC
  • Jumapili, 31 Julai, 2016

Leo ni Jumapili tarehe 26 Shawwal 1437 Hijria inayosadifiana na 31 Julai 2016, Miladia.

Image Caption

Siku kama ya leo miaka 210 iliyopita ardhi ya Cape Colony huko kusini mwa bara la Afrika, ilidhibitiwa na askari wa Uingereza. Kwa utaratibu huo kipindi cha ukoloni wa Uingereza katika eneo la kusini mwa bara hilo kikawa kimeanza rasmi. Aidha ardhi hiyo inafahamika kwa kuwa na utajiri mwingi wa dhahabu na almasi na ni kwa msingi huo ndio maana ikapewa umuhimu mkubwa na wakoloni wa Uingereza.

Ayatullah Sayyid Abdul-Muhammad Musawi

Siku kama ya leo miaka 144 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Abdul-Muhammad Musawi, msomi mkubwa wa Kiislamu na marjaa wa Waislamu nchini Iran. Akiwa na miaka saba Sayyid Abdul-Muhammad Musawi aliweza kuhifadhi Qur'an Tukufu sambamba na kuanza masomo ya dini. Alipofikisha umri wa miaka 24 alifikia daraja la ijtihadi na kuanza kujishughulisha na kazi ya ufundishaji. Alikuwa miongoni mwa walimu mashuhuri wa elimu za fiqhi na usul fiqhi katika hawza za kidini za wakati huo. Kitabu cha 'Sharhu Istidlaali alaa Urwatul-Wuthqaa' na 'Dhakhiratul-Ibad' ni miongoni mwa athari za Ayatullah Sayyid Abdul-Muhammad Musawi.

Franz Liszt

Siku kama ya leo miaka 130 iliyopita, aliaga dunia Franz Liszt mtunzi wa nyimbo wa nchini Hungary. Franz alizaliwa mwaka 1811. Franz Liszt pia alikuwa na kipawa na maarifa makubwa katika utungaji wa nyimbo. Wimbo Hungarian Rhapsodies na shairi la Symphony ni miongoni mwa kazi za utunzi wa Franz Liszt. 

Antoine de Saint-Exupery

Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita aliaga dunia Antoine de Saint-Exupery mwandishi na mwana anga wa Kifaransa katika Vita vya Pili vya Dunia baada ya ndege yake kuanguka. Exupery alizaliwa mwaka 1900 katika mji wa Lyon nchini Ufaransa. Mwandishi Antoine de Saint Exupery alijishughulisha na masuala ya kusafiri angani kutokana na kupenda sana fani hiyo. Aidha alijiunga na jeshi la Ufaransa katika Vita vya Pili vya Dunia na kuwa afisa wa masuala ya usafirishaji wa posta. Siku hiyo Antoine de Saint Exupery alirusha ndege hewani akiwa katika kazi zake za kawaida, lakini ndege yake ilitoweka na athari za mwili wake na ndege hiyo hazijaonekana hadi leo. Mwandishi huyo ameandika vitabu kadhaa na miongoni mwake ni "The Little Prince", "Southern Mail" na "Night Flight."

Ayatullah Sayyid Muhammad Ali Shahrustan

Siku kama ya leo miaka 51 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Muhammad Ali Shahrustan, maarufu kwa lakabu ya 'Hibatud-Din' alim na mwanamapambano wa nchini Iraq. Hibatud-Din alizaliwa mwaka 1301 Hijiria mjini Karbala na kuanza masomo ya msingi eneo alikozaliwa na kisha kuelekea katika mji wa Najaf ambapo akiwa hapo aliweza kusomea elimu mbalimbali za Kiislamu na hatimaye kufikia daraja la ijtihadi. Aidha alimu huyo anafahamika kuwa msomi mchapakazi na mchaji-Mungu ambaye katika umri wake wote si tu kwamba  alijikita katika kuandika vitabu tofauti, bali pia alifanya juhudi kubwa katika kuhakikisha Uislamu unatawala na kuwa na nguvu. Mbali na hayo alifanya juhudi nyingi katika kuhakikisha taifa la Iraq linapata uhuru wake huku akishiriki mwenyewe katika mapambano dhidi ya askari wa Uingereza. Ameandika vitabu vingi, baadhi yavyo vikiwa ni 'Al-Muhiit' 'Hikmatul-Ahkam' na 'Nahdhatul-Hussein.'

Elijah Muhammad

Na siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, Elijah Muhammad, kiongozi wa Wamarekani wenye asili ya Kiafrika na Waislamu nchini Marekani alitoa pendekezo la kuundwa kwa serikali ya watu weusi chini ya usimamizi wa serikali ya federali. Pendekezo hilo lilitolewa ikiwa ni katika juhudi za Wamarekani weusi kuepukana na ubaguzi wa rangi ambao umekuwa ukishuhudiwa kila uchao nchini humo dhidi yao. Elijah Muhammad ambaye yeye mwenyewe aliingia dini ya Uislamu baada ya kuathiriwa na Fred Muhammad, kiongozi mwingine wa harakati za Wamarekani weusi Waislamu, alikuwa pia mwenye taathira kubwa katika harakati za kupinga ubaguzi nchini Marekani. Katika harakati hizo, Elijah Muhammad aliasisi chama cha 'Ummat Islam' sambamba na kujenga misikiti na vituo vya kielimu kwa ajili ya Waislamu.