Aug 01, 2016 00:14 UTC
  • Jumatatu, Agosti Mosi, 2016

Leo ni Jumatatu tarehe 27 Shawwal 1437 Hijria sawa na tarehe Mosi Agosti 2016.

Siku kama ya leo miaka 107 iliyopita inayosadifiana na tarehe 11 Mordad 1288 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi Ayatullah Sheikh Fadhlullah Nouri mwanachuoni mkubwa ambaye alikuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na utawala wa kidikteta wa Qaajar hapa nchini Iran. Ayatullah Fadhlullah Nouri alikuwa mstari wa mbele katika kupigania mapinduzi ya katiba, na hali kadhalika alisimama kidete kupinga sheria zilizopitishwa bungeni ambazo zilikuwa zikikinzana na sheria za Kiislamu.

Miaka 41 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo mkutano wa wakuu wa Urusi ya zamani, Marekani na Canada na nchi za Ulaya isipokuwa Albania ulianza huko Helsinki mji mkuu wa Finland. Mkutano huo ambao ulipewa jina la Mkutano wa Usalama na Ushirikiano wa Ulaya, ulifanyika kwa lengo la kuondoa mivutano kati ya nchi za kambi ya Mashariki chini ya uongozi wa Urusi ya zamani na kambi ya Magharibi chini ya uongozi wa Marekani. Hata hivyo mkutano huo wa usalama na ushirikiano haukuwa na mafanikio muhimu katika kuzikurubisha pamoja kambi mbili hizo kufuatia uvamizi uliofanywa na Jeshi Jekundu la Urusi ya zamani nchini Afghanistan mwaka 1979.

Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita ujumbe wa Umoja wa Mataifa uliokuwa umetumwa katika nchi za Iran na Iraq ulitoa ripoti mbili ukitangaza kuwa, utawala wa zamani wa Iraq ulitumia mara kadhaa silaha za kemikali dhidi ya majeshi na raia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa kukiri waziwazi kwamba, jeshi la Iraq lilitumia silaha za kemikali dhidi ya Iran. Pamoja na hayo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halikutoa azimio lolote dhidi ya utawala wa dikteta Saddam Hussein wa Iraq ambao ulikuwa ukiungwa mkono na nchi za Magharibi, kwa kutumia silaha za kemikali. Masaa kadhaa baada ya kutolewa ripoti hizo, ndege za kivita za Iraq ziliushambulia tena mji wa Ushnawiye huko magharibi mwa Iran kwa mabomu ya kemikali na kujeruhi watu 2400.

Na miaka 11 iliyopita katika siku kama ya leo Fahd bin Abdulaziz, mfalme wa zamani wa Saudi Arabia alifariki dunia baada ya kuugua kwa miaka mingi. Alizaliwa mwaka 1921 huko Riyadh. Mwaka 1967 Fahd bin Abdulaziz alikuwa Naibu Waziri Mkuu na miaka minane baadae akawa mrithi wa kiti cha ufalme. Mwaka 1982 Fahd bin Abdulaziz alichukua madarakani na kuwa mfalme wa tano wa silsila ya kizazi cha Aal Saud baada ya kifo cha kaka yake, Khalid bin Abdulaziz. Uhusiano wa Riyadh na Washington ulikuwa wa karibu sana wakati wa utawala wa Mfalme Fahd. Fahd pia aliusaidia kwa hali na mali utawala wa Saddam Hussein wakati wa vita vya miaka minane dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.