Mar 23, 2025 02:21 UTC
  • Jumapili, Machi 23, 2025

Leo ni tarehe 22 mwezi Mtukufu wa Ramadhani 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe 23 Machi 2025 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1173 iliyopita, alifariki dunia Ibn Majah, mpokezi wa Hadithi na mfasiri mashuhuri wa Qur’ani wa Kiislamu.

Ibn Majah alizaliwa mwaka 209 Hijria katika mji wa Qazvin nchini Iran. Alielekea katika nchi mbalimbali za Kiislamu ili kujifunza elimu ya Hadithi. Aliandika kitabu chake mashuhuri kwa jina la "Sunan Ibn Majah" baada ya kuhitimu masomo katika elimu ya Hadithi, kitabu ambacho ni moja kati ya vitabu sita vya Hadithi vyenye itibari vya Waislamu wa madhehebu ya Suni.

Vitabu vingine vya Ibn Majah ni Tafsirul Qur'an na Tarikh Qazvin. ****

Ibn Majah

Miaka 373 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani sawa tarehe 23 Machi mwaka 1652, yalianza shambulizi la manowari za kijeshi za Uingereza dhidi ya majeshi ya Uholanzi.

Amri ya shambulizi hilo ilitolewa na Oliver Cromwell aliyekuwa dikteta wa wakati huo wa Uingereza. Akipata uungaji mkono wa Bunge la Uingereza, Cromwell alimpindua mfalme wa Uingereza na kisha kulivunja bunge la nchi hiyo.

Inasemekana kuwa, lengo la kutekeleza shambulio hilo lilikuwa ni kulimaliza nguvu jeshi la Uholanzi ambalo lilikuwa na nguvu kubwa ya majini.  *****

Oliver Cromwell 

Siku kama ya leo miaka 106 iliyopita, ilianzishwa harakati ya Ufashisti nchini Italia kwa uongozi wa Benito Mussolini.

Ufashisti kwa ujumla ni utawala wa kidikteta wenye kufuata aidolojia ya kibaguzi na kiutaifa, kuwakandamiza wapinzani, kukandamiza uhuru na kuzipotosha itikadi na fikra za wananchi. Hayo yalijiri baada ya Mussolini kunyakuwa wadhifa wa uwaziri mkuu nchini Italia mwaka 1922 na kuanza utawala wa kidikteta nchini humo.

Muda mfupi baadaye Mussolini alishirikiana na Adolph Hitler, na kuandaa mazingira ya kuanzishwa Vita vya Pili vya Dunia. ****

Benito Mussolini

Katika siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, liliasisiwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani 'WMO'. Shirika hilo linafungamana na Umoja wa Mataifa na taasisi zote za hali ya hewa ulimwenguni hushirikiana na shirika hilo.

Miongoni mwa malengo ya kuanzishwa shirika hilo ni kutoa msaada wa elimu ya hali ya hewa kwa wataalamu wa anga, mabaharia, wakulima na shughuli nyingine za kibinadamu.

Ni kwa ajili hiyo ndio maana siku ya leo yaani tarehe 23 Machi ikajulikana kuwa Siku ya Hali ya Hewa Duniani. ***