Jumapili, tarehe 13 Aprili, 2025
Leo ni Jumapili tarehe 14 Shawwal 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe 13 Aprili mwaka 2025.
Katika siku kama ya leo miaka 872 iliyopita alifariki dunia Qutbuddin Rawandi, faqihi wa karne ya sita Hijria ambaye pia alikuwa mtaalamu wa Hadithi na teolojia ya Kiislamu.
Kwa miaka mingi alipata elimu na maarifa kwa wasomi wakubwa wa zama zake na kubobea katika taaluma za fiq'hi, Hadithi na tafsiri ya Qur'ani.
Msomi huyu mkubwa wa Kiislamu ameandika karibu vitabu 80 vikiwemo vya "Tafsirul Qur'an", "Risaalatul-Fuqahaa", "Tahafutul Falasifa", "Aayaatul-Ahkaam" na "Asbaabun-Nuzul."

Siku kama ya leo miaka 106 iliyopita, kulijiri tukio la umwagaji damu mkubwa katika Bustani ya Jallianwala (Jallianwala Bagh Massacre) nchini India.
Mwaka 1919 na kwa lengo la kuzuia uasi na mapambano ya wananchi, serikali ya kikoloni ya Uingereza ilipasisha sheria iliyowapa polisi haki ya kuwatia mbaroni wanaharakati wa India bila sababu yoyote na kuwashikilia kwa muda usiojulikana.
Sheria hiyo iliwakasirisha mno wananchi wa India na katika siku kama ya leo zaidi ya Wahindi elfu tano waliokuwa wamekusanyika kwa amani katika Bustani ya Jallianwala katika mji wa Amritsar walimiminiwa risasi kwa amri ya kamanda mmoja wa Uingereza. Watu 1200 waliuawa na wengine 4000 kujeruhiwa katika tukio hilo.
Baada ya mauaji hayo, harakati ya ukombozi wa India ikiongozwa na shujaa Mahatma Ghandhi ilipamba moto.

Tarehe 13 Aprili mwaka 1945 yaani miaka 80 iliyopita, Austria ilidhibitiwa na kukaliwa kwa mabavu na vikosi vya nchi Waitifaki.
Tukio hilo lilijiri katika miezi ya mwisho ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Kabla ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, Austria ilikuwa nchi huru na inayojitawala. Lakini muda mchache baada ya kuanza vita hivyo, Adolph Hitler aliiunganisha ardhi ya nchi hiyo na Ujerumani na wanajeshi wa Austria wakaingia vitani kupigana upande wa Ujerumani.
Baada ya Ujerumani kuondoka Austria na nchi hiyo kukaliwa kwa mabavu na madola Waitifaki, iligawanywa katika maeneo matano ambapo kila eneo likadhibitiwa na kuendeshwa na moja ya madola hayo, huku mji mkuu Vienna ukiendeshwa kwa pamoja na madola manne.
Hatimaye mwaka 1946, madola Waitifaki yalitambua rasmi uhuru wa Austria ambapo baada ya kutiwa saini mkataba wa amani kati ya pande mbili, mwaka 1955, majeshi ya nchi waitifaki yakaondoka katika ardhi ya Austria.

Katika siku kama ya leo miaka 50 iliyopita, shambulio la wanamgambo wa Kikristo wenye misimamo ya kufurutu ada wa kundi la Mafalanja lililolenga basi moja lililokuwa na Wapalestina na kuua watu 30 kati yao, lilipelekea kuibuka vita vya ndani nchini Lebanon.
Kufuatia mauaji hayo, Waislamu na wazalendo wa Lebanon walianzisha mapambano ya kukabiliana na Mafalanja hao. Muda mfupi baadaye harakati za wapiganaji wa Kipalestina pia ziliingia katika vita hivyo vya ndani vya Lebanon.
Vita hivyo ambayo vilikuwa vikichochewa na utawala haramu wa Israel, viliisababishia hasara kubwa ya mali na roho serikali ya Beirut.

Katika siku kama ya leo miaka 22 iliyopita, yaani tarehe 13 Aprili 2003, yalifanyika maandamano ya kwanza ya wananchi wa Iraq dhidi ya wavamizi baada ya miongo mitatu ya mbinyo na ukandamizaji ya utawala wa dikteta Saddam Hussein.
Baada ya kuangushwa utawala wa Saddam na chama cha Baath Aprili 9 mwaka 2003 na kisha nchi hiyo kukaliwa kwa mabavu na vikosi vamizi hususan majeshi ya Marekani, maandamano ya kwanza ya wananchi ya kupinga kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu nchi yao yalifanyika.
