Aug 07, 2016 01:33 UTC
  • Jumapili, Agosti 7, 2016

Leo ni Jumapili tarehe 4 Dhul-Qaadah mwaka 1437 Hijiria, sawa na tarehe 7 Agosti 2016 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 24 iliyopita, Ayatullahil-Udhma Haji Sayyid Abul-Qaasim Musawi Khui, faqihi na marjaa mkubwa wa Waislamu, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 96. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu, alizaliwa mjini Khoy, kaskazini magharibi mwa Iran na akiwa kijana na kwa idhini ya baba yake alielekea mjini Najaf, Iraq kwa ajili ya kuendelea na masomo. Akiwa mjini hapo Abul-Qaasim Musawi Khui alipata kusoma elimu mbalimbali kama vile mantiki, balagha, misingi ya dini, fiqhi na falsafa na kufikia daraja ya ijtihadi. Ameacha athari kadhaa baadhi yake ikiwa ni Tafsiri ya Qur'an ya 'Al-Bayaan Fii Tafsiiril-Qur'an' 'Jawaahirul-Usuul' 'Mis'baahul-Fuqahaa' na 'Muntakhabur-Rasaail.' Aidha Ayatullahil-Udhma Haji Sayyid Abul-Qaasim Musawi Khui alikuwa na nafasi maalumu katika masuala muhimu ya ulimwengu wa Kiislamu, moja wapo ikiwa ni kuhusiana na kadhia ya Palestina ambapo alitoa fatwa mashuhuri ya udharura wa kuitetea Palestina na kukombolewa Quds Tukufu.

Siku kama ya leo miaka 781 iliyopita, alifariki dunia Mahlabi, mwandishi na msomi mashuhuri wa nchini Misri akiwa na umri wa miaka 57. Mahlabi alitabahari katika fani ya mpangilio mzuri wa vina na mashairi huku akiwa hodari pia katika uchoraji wa hati nzuri, kiasi cha kumfanya hata mwanahistoria mashuhuri Ibn Khalkan kuandika kumuhusu shakhsia huyo kwa kusema: "Nilifanikiwa kumuona na kushuhudia kipaji chake." Mwisho wa kunukuu. Mahlabi alikuwa na uwezo mkubwa katika fani ya mashairi ambapo ameacha vitabu vya mashairi. Mashairi yote ya Mahlabi ni mepesi kiasi cha kuwavutia watu wengi.

Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, alifariki dunia Rabindranat Tagore, mwandishi, malenga na mwanafalsafa wa nchini India. Tagore alizaliwa mwaka 1861 Miladia katika mji wa Kolkata, mashariki mwa nchi hiyo. Sambamba na kujishughulisha na harakati za mwamko wa kitaifa kwa ajili ya uhuru wa India, alijikita pia katika uwanja wa mashairi na uandishi. Maandishi na mashairi ya Rabindranat Tagore yalijikita sana katika kuelezea ubora wa mazingira kwa kutumia fikra za kidini na kifalsafa. Ameacha athari nyingi kati yazo ikiwa ni kitabu cha 'Mtunza Bustani' 'Mwezi Mpya' 'Barua kwa Rafiki' na 'Kiungo cha Tabia Njema.'

Siku kama ya leo miaka 59 iliyopita, Oliver Hardy muigizaji wa filamu za vichekesho wa nchini Marekani alifariki dunia. Hardy aliunda kundi la vichekesho la watu wawili na Stan Laurel ambalo lilizalisha filamu nyingi za vichekesho kwa kipindi cha miaka 30. Tunaweza kusema kuwa, baada ya  Charlie Chaplin, filamu za vichekesho zinazoshika nafasi ya pili katika uga huo ni za Oliver Hardy na Stan Laurel duniani.

Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, Ivory Coast ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Wareno waliivamia Ivory Coast katika karne ya 16, na Ufaransa ikaifanya nchi hiyo kuwa koloni lake mwaka 1891. Hatimaye mwaka 1960, Ivory Coast na nchi nyingine kadhaa makoloni ya Ufaransa barani Afrika zilipata uhuru na kuasisi mfumo wa Jamhuri.

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, yaani tarehe 7 Agosti 1982, Marekani, Lebanon na Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) zilisaini makubaliano ya kuwaondoa wapiganaji wa harakati hiyo huko Beirut mji mkuu wa Lebanon. Makubaliano hayo yalisainiwa kufuatia mashambulio makubwa yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel huko Lebanon tangu mwezi Juni 1982. Lengo la mashambulizi hayo lilikuwa kuwaangamiza au kuwafukuza wanamapambano wa Palestina waliokuweko huko Lebanon. Jeshi la kibaguzi la utawala wa Israel lilitumia silaha nyingi na za kisasa katika mashambulio hayo. Hatimaye Yasir Arafat kiongozi wa zamani wa harakati ya PLO alilazimika kuwaondoa huko Lebanon wanamapambano elfu 12 wa Kipalestina na kuwatuma katika nchi nyingine nane za Kiarabu.

Na siku kama ya leo miaka 8 iliyopita vikosi vya jeshi la Georgia vikisaidiwa na serikali ya Marekani vililishambulia eneo linalopigania kujitenga la Ossetia ya Kusini huko kaskazini mwa nchi hiyo. Mamia ya raia wasio na hatia wala ulinzi waliuawa na kujeruhiwa kwenye mashambulio hayo. Siku moja baadaye, wanajeshi wa Russia waliingilia kati na kuamua kuwaunga mkono wapiganaji wanaopigania kujitenga Ossetia ya Kusini na kulilazimisha jeshi la Georgia kurudi nyuma. Vikosi vya jeshi la Russia vilifanikiwa kuiteka bandari muhimu ya Patumi na kusonga mbele karibu na Tiblis mji mkuu wa nchi hiyo. Jeshi la Russia liliondoka huko Georgia Agosti 12 kwa upatanishi wa Rais wa Ufaransa, na Moscow ikayatambua rasmi kuwa huru maeneo mawili yaliyokuwa yakipigania kujitenga yaani Ossetia ya Kusini na Abkhazia.