Jul 15, 2025 02:27 UTC
  • Jumanne, 15 Julai, 2025

Leo ni Tarehe 19 Mfunguo Nne Muharram 1447 Hijria inayosadifiana na tarehe 15 Julai mwaka 2025.

Siku kama ya leo miaka 1386 iliyopita, msafara wa mateka wa Karbala uliokuwa na familia ya mjukuu wa Mtume, Imam Hussein AS na mashahidi wengine waliouawa na utawala wa Yazid bin Muawiya katika medani ya Karbala uliondoka Kufa nchini Iraq ukielekea Damascus, makao makuu ya serikali ya Bani Umayyah.

Msafara huo hususan Imam Zainul Abidin na Bibi Zainab binti Ali bin Abi Twalib AS ulifichua na kuanika maovu ya Yazid bin Muawiyyah na kuwafanya watu wa Kufa wajute sana kwa kumuacha peke yake mjukuu wa Mtume (saw), Imam Hussein katika mapambano ya Karbala.

Watu wa mji wa Kufa walisikitika sana kutokana na kumwacha peke yake mjukuu huyo wa Mtume na wasiwasi ulizuka juu ya uwezekano wa kuanza harakati ya wananchi dhidi ya utawala wa Yazid mjini humo. Kwa msingi huo mtawala wa Kufa, Ubaidullah bin Ziyad, alikhitari kutuma wajukuu hao wa Mtume wetu Muhammad SAW huko Sham kwa mtawala dhalimu Yazid bin Muawiyyah wakitanguliwa na kichwa kilichotenganishwa na mwili cha Bwana wa Vijana wa Peponi, Imam Hussein AS. 

Katika siku kama ya leo miaka 437 iliyopita kulitokea vita vya Bahari ya Manche (English Channel) kati ya jeshi la majini la Uhispania maarufu kama Jeshi la majini lisiloshindwa na jeshi la majini la Uingereza.

Katika vita hivyo meli kubwa 135 za kivita za Uhispania ziliishambulia Uingereza kwa shabaha ya kulipiza kisasi cha mauaji ya malkia Mary Stuart wa Scotland lakini kutokana na kimbunga kikali meli 85 za Uhispania zilizama majini na kikosi cha jeshi la majini kisichoshindwa cha Uhispania kikapata kipigo kikubwa.

Tangu wakati huo nyota na umashuhuri wa kikosi hicho ukaanza kuzama.     

Siku kama ya leo miaka 121 iliyopita, alifariki dunia Anton Chekhov, mwandishi mashuhuri wa visa wa karne ya 19 wa Urusi akiwa na umri wa miaka 64.

Chekhov alikuwa tabibu na katika kujitolea alijenga kituo cha tiba ambacho alikitumia katika shughuli hiyo. Baada ya hapo alijiunga na taaluma ya uandishi ambapo alianza kujishughulisha na kazi za uandishi katika magazeti na kuandika makala tofauti wakati huo.

Alikuwa mahiri katika tenzi fupifupi na akatokea kuwa mashuhuri katika uga huo. Miongoni mwa athari za mwandishi huyo ni pamoja na kitabu cha "Jogoo wa Bahari".   

Anton Chekhov

Siku kama ya leo miaka 105 iliyopita, mfalme wa Syria aliyewekwa katika nafasi hiyo na Uingereza alifanikiwa kuwa mfalme wa Iraq baada ya kukimbia kutoka Damascus.

Julai 15 mwaka 1920, baada ya vikosi vya Ufaransa kukaribia mji wa Damascus, Amir Feisal aliyekuwa ametawalishwa na Uingereza huko nchini Syria aliukimbia mji huo. Syria na Lebanon ni miongoni mwa ardhi zilizokuwa chini ya mamlaka ya utawala wa Othmania ambazo mwishoni mwa Vita vya Kwanza vya Dunia ziliwekwa chini ya udhibiti wa Ufaransa.

Tarehe 18 Julai mwaka huo huo, mji wa Damascus ulitekwa na kukaliwa kwa mabavu na vikosi vya Ufaransa. Amir Feisal ambaye aliongoza Syria kwa miezi mitatu tu akiwa Mfalme, baadaye akatawalishwa na Uingereza kuwa Mfalme wa Iraq.

Siku kama ya leo miaka 86 iliyopita inayosadifiana na tarehe 24 Tir 1318 Hijria Shamsia, alizaliwa Ayatullah Sayyid Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mji wa Mash'had ulioko kaskazini mashariki mwa Iran.

Baada ya kumaliza masomo katika shule ya sekondari, alijikita zaidi katika masomo ya kidini kutoka kwa baba yake, na kupiga hatua kubwa ya kielimu katika kipindi kifupi. Ayatullah Khamenei alielekea Qum kwa masomo ya juu ya kidini na kupata fursa ya kunufaika na elimu kutoka kwa maulamaa wakubwa katika mji huo, kama vile Imam Ruhullah Khomeini, Ayatullahil Udhma Burujerdi na Allamah Tabatabai katika masomo ya fiqh, usululi na falsafa. Akiwa bado kijana, Sayyid Khamenei alikuwa mstari wa mbele katika harakati za mapinduzi dhidi ya utawala kibaraka wa Shah hapa nchini, na mara kadhaa alitiwa mbaroni, kutumikia vifungo na hata kupelekwa uhamishoni.

Baada ya kufariki dunia Imam Khomeini MA mwaka 1368 Hijria Shamsia, Baraza la Wanachuoni linalomchagua Kiongozi Mkuu wa Iran, lilimchagua Ayatullah Khamenei, wakati huo akiwa rais wa nchi, kuwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei

Siku kama ya leo miaka 81 iliyopita yaani tarehe 15 Julai mwaka 1944, jeshi la Marekani lilianza kuishambulia Japan kwa maelfu ya mabomu katika kipindi cha Vita vya Pili vya Dunia.

Mashambulio hayo ya mabomu ya Marekani yaliendelea hadi Japan iliposalimu amri. Tukio hilo chungu licha ya kusababisha makumi ya maelfu ya wananchi wasio na hatia wa Japan kuuawa kwa halaiki, lilipelekea pia zaidi ya viwanda elfu tatu vikubwa kwa vidogo kuharibiwa kabisa. 

Katika siku kama ya leo miaka 57 iliyopita yaani tarehe 24 Tir mwaka 1347 Hijria Shamsia, Ismail Balkhi mwanamapambano na mwanafikra wa Kiafghani aliuawa shahidi mjini Kabul.

Alizaliwa katika kijiji kimoja kaskazini mwa Afghanistan. Alianza kusoma kwa bidii masomo ya dini tangu akiwa mdogo na kipindi fulani alifanya safari nchini Iran na Iraq, lengo likiwa ni kujiendeleza zaidi kielimu. Ismail Balkhi alikuwa akiendesha mapambano dhidi ya udikteta na daima alikuwa akiwashajiisha wananchi Waislamu wa Afghanistan kupambana na tawala dhalimu.

Kutokana na harakati hizo, shahidi Balkhi alikuwa chini ya mashinikizo ya watawala wa wakati huo wa Afghanistan, na kwa miaka kadhaa alifungwa jela.

Ismail Balkhi

Siku kama ya leo miaka 15 iliyopita inayosadifiana na tarehe 24 Tir 1389 Hijria Shamsia, kwa akali watu 27 waliuawa na wengine 169 kujeruhiwa kwenye milipuko miwili ya mabomu iliyotokea katika mji wa Zahedan, ulioko kusini mashariki mwa Iran.

Milipuko hiyo ilitokea mkabala na Msikiti Mkuu wa Zahedan, wakati wa sherehe za kuadhimisha siku ya kuzaliwa Imam Hussein bin Ali bin Abi Talib (as) mmoja kati ya wajukuu wa Mtume Muhammad (saw). Kikundi cha kigaidi kilichojiita Jundullah, ndicho kilichotekeleza shambulio hilo la kigaidi. ***