Jumatano, tarehe 23 Julai, 2025
Leo ni Jumatano tarehe 27 Muharram 1447 Hijria sawa na Julai 23 mwaka 2025.
Katika siku kama ya leo miaka 262 iliyopita alifariki dunia mwanafasihi na mwandishi wa michezo ya kuigiza wa Kifaransa Pierre Marivaux.
Marivaux alizaliwa tarehe 17 Novemba mwaka 1688 Miladia mjini Paris, Ufaransa. Mwanafasihi huyu alianza kujishughulisha na sanaa akiwa na umri wa miaka 18 baada ya kufahamiana na wanafikra na wataalamu wa fasihi wa nchi hiyo na alifanya kazi hiyo ya kuigiza kwa miaka kadhaa katika majumba ya mchezo huo hadi alipoanza kuandika michezo hiyo mwenyewe.
Pierre Marivaux alipata umashuhuri mkubwa haraka kutokana na kipawa chake kikubwa cha ukosoaji na uwezo wake mkubwa wa uandishi wa fasihi.
Miongoni mwa kazi za mwandishi huyo ni mchezo wa kuigiza wa The Prudent and Equitable Father, The Triumpth of Love, The Life of Marianne na The Fortunate Peasant.
Siku kama hii ya leo miaka 227 iliyopita jeshi la Napoleon Bonaparte liliwasili katika mji wa Cairo na mji huo ukakaliwa kijeshi na wavamizi wa Kifaransa. Utawala wa silsila ya Mamaliki ulifikia kikomo huko Misri baada ya mji wa Cairo kukaliwa kwa mabavu na wavamizi wa Kifaransa.
Napoleon alielekea Cairo mji mkubwa zaidi wa Misri ambao pia ulikuwa mji mkuu wa utawala wa silsila ya Mamalik baada ya jeshi lake kuikalia kwa mabavu bandari ya Alexandria kwa kutumia zana za kisasa za kivita.

Siku kama ya leo miaka 196 iliyopita kulivumbuliwa kwa mara ya kwanza mashine ya uandishi (typewriter).
Tarehe 23 Julai mwaka 1829 William Barrett raia wa Marekani aliweka rekodi kufuatia kuvumbua na kutengeza mashine hiyo ya uandishi katika jimbo la Michigan. Hata hivyo baada ya hapo hakukuwa na harakati zozote za kuendeleza mashine hiyo.
Miaka 31 baadaye yaani sawa na mwaka 1867, vijana watatu wa Marekani kwa majina ya Christopher Scholl, Carlos Glydn na Samuwel, walifanikiwa kutengeneza mashine ya kuandikia katika mji wa Milwaukee jimbo la Wisconsin nchini humo, mashine ambayo utumiaji wake ulikuwa mwepesi na rahisi.
Ni vyema kuashiria kuwa, juhudi za kuunda mashine ya uandishi zilianza tangu karne ya 14, lakini zikaja kuzaa matunda kuanzia karne ya 18.

Siku kama ya leo miaka 146 iliyopita, alizaliwa Ernst Herzfeld mtaalamu wa Ujerumani wa masuala ya mashariki ya dunia na Iran.
Alikuwa na umahiri mkubwa katika kufahamu ada na lugha za watu wa zamani. Herzfeld alifahamu vizuri historia ya kale ya Iran na Iraq ambapo pia alifundisha kwa miaka mingi katika chuo kikuu cha Berlin, Ujerumani historia hiyo. Aidha alipata kuandika yapata vitabu na makala mbalimbali 190 kuhusiana na historia ya lugha ya Kifarsi na dini tukufu ya Uislamu. Kitabu cha 'Iran na Mashariki ya Zamani' ni miongoni mwa athari za msomi huyo. Ernst Herzfeld alifariki dunia mwaka 1947.
Katika siku kama ya leo miaka 31 iliyopita kulijiri mapiduzi ya kijeshi dhidi ya serikali ya Sir Dawda Jawara wa Gambia. Gambia ilianza kujitangazia mamlaka ya ndani mwaka 1962 kutoka kwa mkoloni Mwingereza.
Mwaka 1965 na baada ya kujitangazia uhuru ilijiunga na Umoja wa Mataifa ambapo mwaka 1966 Dawda Jawara alitangazwa kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo. Mwaka 1981 wakati Jawara alipokuwa mjini London kulifanyika mapinduzi ya kijeshi ambayo hata hivyo yalisambaratishwa kwa uingiliaji wa kijeshi wa askari wa Senegal ambapo hatimaye Jawara aliweza kurejea tena madarakani.
Tarehe 23 Julai mwaka 1994 Yahya Abdul-Aziz Jemus Junkung Jammeh aliongoza tena mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Jawara na kumlazimu kiongozi huyo akimbie nchi. Mwaka 1984 Dawda Jawara aliongoza tume ya upatanishi iliyochaguliwa na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC kati ya Iraq na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita alifariki dunia Mfalme Hassan wa Pili wa Morocco baada ya kukalia kiti cha usultani kwa miaka 38.
Alizaliwa mwaka 1929 na kukalia kiti cha usultani mwaka 1961, yaani miaka mitano baada ya Morocco kupata uhuru wake. Mfalme Hassan wa Pili wa Morocco alinusurika kuuawa mara kadhaa wakati akiwa madarakani.
Hassan wa Pili wa Morocco alikuwa mfalme dikteta ambaye alikuwa akikandamiza na kuzima vikali harakati zozote za upinzani jambo ambalo lililalamikiwa sana na wananchi wa Morocco.