Aug 09, 2016 06:11 UTC
  • Jumanne, tarehe 9 Agosti, 2016

Leo ni Jumanne tarehe 6 Dhilqaada 1437 Hijria sawa na Agosti 9 2016 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, siku tatu baada ya Marekani kushambulia mji wa Hiroshima nchini Japan kwa bomu la nyuklia, Washington iliushambulia pia kwa bomu jingine la nyuklia mji wa bandari wa Nagasaki kwa amri ya Harry Truman, Rais wa wakati huo wa nchi hiyo. Jumla ya watu elfu themanini walifariki dunia dakika chache tu baada ya shambulizi hilo la bomu la nyuklia huko Nagasaki, na wengine walipoteza maisha baada ya kupita miezi na miaka, kutokana na athari mbaya za mada hatari za mionzi ya nunurishi au radioactive kwa kimombo. Maafa makubwa ya mashambulizi ya mabomu ya nyuklia ya Marekani huko Hiroshima na Nagasaki yaliyofanyika kwa lengo la kuilazimisha Japan isalimu amri kikamilifu mbele ya majeshi ya waitifaki, yalikuwa kengele ya hatari kwa walimwengu kwamba, nchi zinazomiliki silaha za atomiki hususan Marekani, hazisiti kufanya jinai za kutisha kama kuangamiza kizazi cha wanadamu kwa ajili ya kufikia malengo yao.

Miaka 51 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Singapore ilijitenga na Malaysia. Japan iliiteka Singapore katika Vita vya Pili vya Dunia lakini mnamo mwaka 1945 uvamizi huo wa Japan ulikomeshwa na kwa mara nyingine tena nchi hiyo ikakoloniwa na Uingereza. Mwaka 1963 Singapore iliunganishwa na Shirikisho la Malaysia na mwaka 1965 ilijitenga na kuwa nchi huru.

Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita, Hermamn Hesse mwandishi na malenga mashuhuri wa nchini Ujerumani aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 1877 katika familia ya kidini na kuanza kazi ya utunzi wa mashairi katika kipindi cha kuinukia kwake. Akiwa na umri wa miaka 20, Hesse alitoa mjumuiko wake wa kwanza wa mashairi. Mwaka 1912 mwandishi na malenga huyo mashuhuri wa Ujerumani alichukua uraia wa Uswisi na kuichagua nchi hiyo kuwa makazi yake ya kudumu. Mwishoni mwa umri wake alifanya safari katika baadhi ya nchi za mashariki na kuathirika na tamaduni, mafunzo na mienendo ya kimaadili ya watu wa maeneo hayo. Mnamo mwaka 1946 malenga huyo alitunukiwa tuzo ya Nobel.

Na miaka 42 iliyopita katika siku kama ya leo Richard Nixon Rais wa zamani wa Marekani kutoka chama cha Republican alilazimika kujiuzulu kwenye wadhifa huo, baada ya kukumbwa na kashfa ya kufanya udanganyifu kwenye uchaguzi wa Rais, kashfa iliyojulikana kwa jina la "Watergate". Nixon alilazimika kung'atuka kwenye nafasi ya urais na kumpisha Gerald Ford aliyekuwa Makamu wa Rais ambaye aliendeleza kipindi hicho cha urais kwa muda wa miaka minne.

Tags