Jumanne, 19 Agosti, 2025
Leo ni Jumanne tarehe 25 Mfunguo Tano Safar 1447 Hiijria sawa na tarehe 19 Agosti 2025.
Siku kama ya leo miaka 362 iliyopita, alifariki dunia Blaise Pascal, mwandishi, mwanahisabati na mvumbuzi wa calculator au kikokotoo wa Kifaransa.
Alizaliwa Juni mwaka 1623 na tangu utotoni Pascal alivutiwa mno na somo la hisabati. Vilevile urafiki wa baba yake Pascal na msomi mmoja maarufu wa zama hizo ulisaidia mno katika kuchanua kipawa na kugunduliwa uwezo wa kijana huyo katika taaluma ya hisabati.
Mwishoni mwa umri wake Blaise Pascal alijielekeza mno katika masuala ya dini na kuandika vitabu kadhaa katika uwanja huo.

Katika siku kama hii ya leo miaka 206 iliyopita aliaga dunia mvumbuzi na mhandisi wa Kiingereza James Watt.
Msomi huyo alipendelea na kuvutiwa mno na utafiti kuhusu masuala ya kisayansi. Katika utafiti wake Watt alifanikiwa kuvumbua nishati ya mvuke na kuzusha mapinduzi makubwa katika sekta ya viwanda hususan usafirishaji wa nchi kavu na baharini.

Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Shamsia, kulifanyika mapinduzi ya Kimarekani dhidi ya serikali ya Dakta Muhammad Musaddiq nchini Iran na baadaye kidogo Shah Reza Pahlavi akatwaa tena madaraka ya nchi. Mapinduzi hayo ambayo yalipangwa na shirika la ujasusi la Marekani CIA kwa ushirikiano wa Uingereza, yaliiondoa madarakani serikali ya Musaddiq kupitia njia ya kuzusha hitilafu na mifarakano kati ya wanaharakati wa kisiasa na wananchi na kueneza anga ya ghasia na machafuko nchini. Vilevile yalimrejesha Iran Shah Pahlavi ambaye siku tatu kabla alikuwa amekimbilia nchini Italia. Kabla ya tukio hilo la kusikitisha, wananchi Waislamu wa Iran walikuwa wamefanikiwa kukata mkono wa Uingereza hapa nchini na kutaifisha sekta ya mafuta iliyokuwa ikidhibitiwa na wakoloni hao.

Miaka 47 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 28 Mordad 1357, Hijria Shamsia, vibaraka wa utawala wa Shah walifanya maafa ya kutisha ya kuchoma moto jumba la sinema la Rex katika mji wa Abadan kusini mwa Iran. Katika tukio hilo la kinyama watu wasio na hatia 377 wakiwemo watoto na wanawake walipoteza maisha yao. Jinai hiyo ilifanywa na maajenti wa Shirika la Kiintelijensia na Usalama wa Taifa la Iran (SAVAK) na vibaraka wa utawala wa Shah. Watu karibu 700 waliokuwa wakitazama sinema katika jumba hilo walifungiwa ndani baada ya moto kuzuka na mamia miongoni mwao wakateketea. Tukio hilo lilizusha hasira kubwa baina ya wananchi. Utawala wa Shah ulifanya maafa hayo na kisha kuwatuhumu wanamapinduzi kuwa ndio waliotekeleza shambulizi hilo la kutisha kwa shabaha ya kuchafua sura la harakati za Mapinduzi ya Kiislamu mbele ya wananchi. Hata hivyo njama hizo za Shah zilifeli.

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, makamanda wa ngazi za juu wa jeshi la Urusi ya zamani wakiongozwa na Gennady Ivanovich Yanayev walifanya mapinduzi dhidi ya rais wa mwisho wa Muungano wa Sovieti, Mikhail Gorbachev.
Wanajeshi hao walitaka kukomeshwa marekebisho ya Gorbachev na kuzuia mpango wa kugawanywa Urusi ya zamani. Wakati wa mapinduzi hayo Mikhail Gorbachev alikuwa katika Peninsula ya Crimea huko kaskazni mwa Bahari Nyeusi. Hata hivyo Boris Yeltsin ambaye wakati huo alikuwa kiongozi wa Federesheni ya Urusi na ambaye alikuwa akiungwa mkono na Magharibi, alizima mapinduzi hayo kwa msaada wa wananchi na baadhi ya watu wenye ushawishi serikalini.
Kushindwa kwa mapinduzi hayo kulizidisha uwezo na satua ya Boris Yeltsin na kuharakisha mwenendo wa kusambaratika Urusi ya zamani hapo mwaka 1991. ***