Oct 04, 2025 02:23 UTC
  • Jumamosi, 04 Oktoba, 2025

Leo ni Jumamosi 11 Mfunguuo Saba Rabiu Thani 1447 Hijria mwafaka na 4 Oktoba 2025 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1228 iliyopita, alifariki dunia Abu Ali Khayyat, mnajimu na mtaalamu wa hesabati wa Kiislamu. Abu Ali ni mmoja wa shakhsia aliyekuwa na nafasi kubwa wakati wake huku jina lake likiwekwa mstari wa mbele katika kitabu cha majina ya wasomi wakubwa na mashuhuri wa dunia. Msomi huyo ameandika vitabu vingi maarufu zaidi kikiwa ni kitabu cha 'Mawaalid' na 'Siyarul-A'amaal.' Vitabu vingi vya Abu Ali Khayyat vimetarjumiwa kwa lugha ya Kilatini.   

Abu Ali Khayyat

 

Siku kama ya leo miaka 840 iliyopita, alizawa mjini Mosul, moja ya miji mashuhuri ya Iraq, Ibn Khallikan, kadhi, mwanahistoria na mtaalamu wa fasihi wa Kiislamu. Akiwa kijana alisoma elimu za awali katika mji alikozaliwa na kisha kufanya safari mbalimbali na kukutana na wanasheria wa Kiislamu na wanahistoria wakubwa sanjari na kustafidi na elimu kutoka kwao. Kwa muda mrefu Ibn Khallikan alikuwa kadhi mjini Damascus, Syria ya leo huku akiwa mtaalamu pia katika elimu za historia, fasihi ya Kiarabu na mashairi. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia mwezi wa Rajab mwaka 681 Hijiria baada ya kuugua na kuzikwa chini ya mlima Qasioun ulio Damascus ambako pia wamezikwa wasomi wengi. Kitabu muhimu zaidi cha Ibn Khallekan ni Wafayatul A'yan.

Ibn Khallikan, kadhi, mwanahistoria na mtaalamu wa fasihi wa Kiislamu

 

 Siku kama ya leo miaka 195 iliyopita, Ubelgiji ilijitangazia uhuru. Mwanzoni mwa karne ya 18 Ubelgiji ilikuwa chini ya udhibiti wa Austria, huku ikidhibitiwa na Ufaransa mwishoni mwa karne hiyo hiyo. Hata hivyo baada ya Napoleon Bonaparte kushindwa na madola ya Ulaya, mwaka 1815 Ubelgiji na Uholanzi ziliunda muungano. Hata hivyo muungano huo haukudumu kwa muda mrefu kufuatia Wabelgiji wa Kikatoliki kuanzisha uasi dhidi ya Waholanzi wa Kiprotestanti na hivyo kuamua kujitangazia uhuru wao katika siku kama ya leo.

 

Katika siku kama ya leo miaka 97 iliyopita tabibu Alexander Fleming alivumbua dawa ya penicillin. Fleming ambaye alikuwa daktari maarufu nchini Uingereza, alizaliwa tarehe Sita Agosti mwaka 1881 katika familia ya wakulima mjini Lochfield farm, magharibi mwa Scotland. Fleming alivumbua dawa hiyo baada ya kuona kuwa askari wengi walikuwa wakipoteza maisha kutokana na kukumbwa na bakteria wa maambukizi kwenye majeraha, suala ambalo lilimtia wasi wasi mkubwa. Miaka 10 baada ya kumalizika vita, sawa na tarehe Nne Oktoba mwaka 1928 Miladia, Fleming alifanikiwa kuvumbua dawa ya penicillin, ambayo huua vijidudu vya maambukizi kwenye kidonda.

Alexander Fleming

 

Siku kama ya leo miaka 68 iliyopita satalaiti ya kwanza ilirushwa angani na msomi wa Urusi ya zamani na kwa utaratibu huo zama za udhibiti wa anga zikawa zimeanza. Satalaiti hiyo iliyopewa jina la Sputniki 1 ilizunguka dunia mara 1400 kwa siku 92 na kwa mara ya kwanza ikafikisha ujumbe wa radio kutoka angani kuelekea ardhini. 

 

Mwaka mmoja uuliopita katika siku kama ya leo, Sayyed Hashem Safi al-Din, mmoja wa viongozi wa Hizbollah nchini Lebanon na Mkuu wa Baraza Kuu la harakati hiyo, aliuawa shahidi. Alizaliwa mwaka wa 1964 katika kijiji kilichoko kusini mwa Lebanon katika familia yenye ushawishi na kidini. Katika ujana wake, alimwoa binti wa Sayyed Muhammad Ali Amin, mjumbe wa Baraza Kuu la Kiislamu la Mashia wa Lebanon, na kisha akaenda katika vyuo vya kidini (Hawza) vya  Najaf , Iraq na Qom Iran kwa ajili ya masomo. Miaka yake ya kuishi huko Qom, hasa kufahamu kwake fikra ya Velayat al-Faqih na kazi za Imam Khomeini (RA), ni mambo yaliyokuwa na nafasi muhimu katika kuunda mitazamo yake ya kisiasa na kifikra. Safi al-Din alijiunga na Hizbullah mwanzoni mwa miaka ya 1980 na kupanda haraka safu za uongozi za harakati hiyo. Mnamo 1992, alikua Mwenyekiti wa Baraza za Utendaji la Hizbullah na mmoja wa wajumbe saba wakuu wa Baraza la Ushauri la kuchukua maamuzi la Hizbullah. Seyyed Hashem Safiuddin alikuwa kwenye orodha ya vikwazo vya Marekani kwa miaka mingi na alikuwa akilengwa na tetesi za mauaji mara kadhaa. Hatimaye aliuawa shahidi katika siku kama ya leo kuufuatia shambulio la anga la utaawala ghasibu wa Israel kusini mwa Beirut.