Jumapili, Agosti 14, 2016
Leo ni Jumapili tarehe 11 Dhil-Qaadah mwaka 1437 Hijria, sawa na tarehe 14 Agosti 2016.
Siku kama ya leo miaka 1289 iliyopita, yaani tarehe 11 Dhil-Qaadah mwaka 148 Hijiria, alizaliwa mjini Madina, Imamu Ali Bin Musa al-Ridha (as), mmoja wa Ahlu Bayti watukufu wa Mtume Muhammad (saw) na imamu wa nane wa Waislamu. Imamu Ridha (as) alianza kuongoza umma wa Kiislamu mwaka 183 baada ya kufariki dunia baba yake mtukufu, yaani Imamu Musa al-Kaadhim (as). Katika uhai wake alifahamika kama shakhsia wa pekee katika ulimwengu wa Kiislamu kutokana na elimu yake ya hali ya juu na uchaji-Mungu. Ni kutokana na hali hiyo na katika kujaribu kudhibiti hali ya mambo na kuzuia taathira chanya za mtukufu huyo katika ulimwengu wa Kiislamu, ndipo khalifa wa utawala wa Bani Abbasi yaani Ma'amun, akamlazimisha kuwa mrithi wake wa kiti cha ufalme lengo kuu likiwa ni kumdhibiti Imamu Ridha (as). Hatua hiyo ilimlazimu mtukufu huyo kupelekwa mjini Mar'wu, kaskazini mashariki mwa Iran ambao ulikuwa makao makuu ya utawala wa Bani Abbasi enzi hizo. Hata hivyo njama chafu hizo za mtawala Ma'amun ziligonga mwamba baada ya watu wengi kuvutiwa sana na Imam Ridha kutokana na elimu ya hali ya juu na mawaidha yake aliyokuwa akiyatoa kwa Waislamu suala ambalo lilipelekea mtawala huyo kupanga njama za kumuua. Hatimaye mwaka 203 Hijiria, Imam Ridha akauawa shahidi baada ya kulishwa sumu ndani ya chakula.
Siku kama ya leo miaka 1101 iliyopita, alizaliwa mjini Baghdad, Iraq, Muhammad Bin Muhammad, maarufu kwa lakabu ya 'Sheikh Mufid', msomi na faqihi mkubwa wa Waislamu. Sheikh Mufid alikulia katika familia ya watu wenye elimu na imani, huku akisoma masomo yake ya msingi katika familia yake na kisha kwa walimu mashuhuri wa enzi hizo. Baada ya hapo Muhammad, alitokea kuwa alimu mkubwa katika uga wa theolojia na sheria za Kiislamu wa zama hizo. Miongoni mwa harakati za kifikra na kitamaduni za Sheikh Mufid ni pamoja na kujadiliana kielimu na wasomi wa sheria za Kiislamu na maulama wa madhehebu tofauti za Kiislamu suala ambalo lilimfanya kuibukia kuwa alimu hodari katika uga wa theolojia na sheria. Sheikh Mufid ameacha athari nyingi za vitabu ambavyo vinafikia juzuu 200 baadhi yavyo ikiwa ni vitabu vya 'Al-Irshaad' 'Al-Arkaan' na 'Usulul-Fiqhi.'
Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Allamah Mirza Muhammad Hussein Naini, marjaa na faqihi mkubwa na mmoja wa wahakiki wa elimu ya usulu fiq’h wa hawza ya mjini Najaf, Iraq. Allamah Naini alizaliwa mwaka 1276 Hijiria Qamaria mkoani Nain, ambao ni moja ya mikoa ya katikati mwa Iran katika familia ya kidini. Allamah Naini alisoma na kuhitimu masomo yake ya awali nyumbani kwao na kuendelea na masomo ya juu huko mjini Najaf, Iraq. Akiwa mjini hapo, alipata kusoma kwa wasomi wakubwa wa zama hizo kama vile Allamah Mirza Shirazi na kufikia daraja ya juu ya elimu za hesabu, falsafa ya sayansi, falsafa, irfan na fiq’hi. Miongoni mwa athari za Allamah Naini ni pamoja na vitabu vya “Wasiilatun-Najjat” na “Tanbiihul-Ummah wa Tanziihul-Millah” kitabu ambacho kilitoa mchango mkubwa katika kuathiri mapambano dhidi ya viongozi dhalimu wa zama hizo.
Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, nchi ya Japan ililazimika kusalimu amri mbele ya nchi waitifaki katika Vita vya Pili vya Dunia. Kwa utaratibu huo vita vilivyoanza mwaka 1939 Miladia kwa jeshi la Wanazi wa Ujerumani kuishambulia Poland, vikafikia tamati. Tangu mwezi Disemba mwaka 1941 Miladia, Japan na Marekani, zilikuwa zikipigana vikali katika vita vya kimaslahi. Hata hivyo vita hivyo vilimalizika baada ya Marekani kuishambulia kwa mabomu ya nyuklia miji miwili ya Japan ya Heroshima na Nagasaki ambapo watu karibu laki mbili waliuawa. Hivyo kusalimu amri kwa Japan ndiko kulikohitimisha vita hivyo vya pili vya dunia.
Siku kama ya leo miaka 69 iliyopita, Pakistan ilijitenga na India na kujitangazia huru wake. Dini ya Kiislamu iilingia India katika karne ya nane Miladia na sehemu ya ardhi ya nchi hiyo ambayo leo hii inajulikana kama Pakistan ilikuwa chini ya himaya ya Waislamu, wakati ilipokaliwa kwa mabavu na Waingereza mwishoni mwa karne ya 18 Miladia. Aidha chama cha Muslim League kiliasisiwa mwaka 1906 chini ya uongozi wa Muhammad Ali Janah sambamba na kuanza mapambano ya wananchi wa India dhidi ya mkoloni Muingereza.
Siku kama ya leo miaka miaka 60 iliyopita yaani tarehe 14 Agosti 1954, aliaga dunia malenga na mwandishi wa Kijerumani aliyejulikana kwa jina la Bertolt Brecht. Brecht alizaliwa mwaka 1898 Miladia katika jimbo la Ugsbourg nchini Ujerumani. Malenga na mwandishi huyo wa Kijerumani alihitimu elimu ya juu katika masuala ya asilia (nature). Malenga huyo wa Kijerumani ameacha vitabu na picha ambazo nyingi zinaeleza kuhusu utawala wa Manazi na udhalimu waliokuwa wakiutenda.
Na siku kama ya leo miaka 11 iliyopita, vita kati ya Harakati ya Mapambano ya Lebanon Hizbullah na utawala wa Kizayuni wa Israel vilimalizika kufuatia kupitishwa azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kukubaliwa na pande hizo mbili. Tarehe 12 Juni mwaka 2006, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilianzisha vita huko Lebanon kwa lengo la kuangamiza uwezo wa kijeshi wa Hizbullah. Hata hivyo wananchi wa Lebanon waliendesha mapambano makubwa mbele ya mashambulizi ya kinyama ya Wazayuni. Katika vita hivyo, harakati ya Hizbullah iliendesha mashambulizi ya kijasiri na ya ghafla dhidi ya wanajeshi wa Kizayuni na kufanikiwa kuangamiza manowari mbili za kisasa, ndege 6 za kivita, makumi ya vifaru na wanajeshi wengi wa utawala huo haramu.