Aug 15, 2016 03:00 UTC
  • Jumatatu tarehe 12 Dhilqaada 1437 Hijria sawa na tarehe 15 Agosti 2016

Miaka 56 iliyopita katika siku kama ya leo mwafaka na tarehe 15 mwezi Agosti mwaka 1960 Jamhuri ya Kongo maarufu kwa jina la Kongo Brazaville ilipata uhuru.

Kongo ilikuwa sehemu ya ardhi ya Kongo iliyozijumuisha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (Zaire ya zamani) na Angola. Kongo Brazaville iligunduliwa na Wareno katika karne ya 15 na baadaye ilikaliwa kwa mabavu na wakoloni wa Kifaransa kwa miaka kadhaa.

Siku kama ya leo miaka 23 iliyopita aliaga dunia Ayatullah Sayyid Abdul Ali Musawi Sabzavari mmoja wa wanazuoni mashuhuri wa Iran. Ayatullah Sabzavari alizaliwa mwaka 1290 Hijria shamsia katika mji wa Sabzavar huko kaskazini mashariki mwa Iran. Mwanazuoni huyo alianza masomo ya Kiislamu akiwa na umri wa miaka 14 na baadaye akaendelea na masomo hayo katika mji mtakatifu wa Mash'had, Iran. baadaye alielekea katika mji wa Najaf nchini Iraq na kunufaika na elimu ya wanazuoni wakubwa wa mji huo mtakatifu na kupata daraja ya juu ya elimu ya Ijtihad katika kipindi kifupi. Mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi lakini mashuhuri zaidi ni tafsiri ya Qur'ani ya Mawahibur Rahman yenye juzuu 20.

Siku kama ya leo miaka 11 iliyopita utawala wa Kizayuni wa Israel ulilazimika kuondoka Ukanda wa Ghaza magharibi mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Eneo la Ukanda wa Ghaza lilikaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel wakati wa vita kati ya Waarabu na utawala huo mwaka 1967. Wanajeshi na walowezi wa Kizayuni walikataa kuondoka katika Ukanda wa Ghaza licha ya kutiwa saini mapatano kati ya Tel Aviv na Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) mwaka 1993 na kuundwa serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina ambayo inapaswa pia kulisimamia eneo la Ukanda wa Ghaza.