Ijumaa, AGOSTI 19, 2016
Leo ni Ijumaa tarehe 16 Dhulqaada 1437 Hijria sawa na 19 Agosti 2016.
Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita Marekani ilikiri kwamba ilifanya makosa kuishambulia ndege ya abiri ya Iran hapo tarehe 3 Julai mwaka 1988. Siku hiyo ndege ya abiria aina ya Airbus ya shirika la ndege ya Iran iliyokuwa ikitoka Bandar Abbas kusini mwa Iran na kuelekea Dubai Umoja wa Falme za Kiarabu ilishambuliwa kwa makombora mawili kwenye maji ya Ghuba ya Uajemi. Manowari ya kijeshi ya Marekani USS Vincennes ilifyatua makombora hayo na kuua shahidi watu 298 waliokuwemo. Shambulio hilo lilionyesha wazi unyama wa serikali ya Marekani na ukatili wake hata kwa wanawake na watoto wadogo waliokuwemo ndani ya ndege hiyo. Viongozi wa Marekani walizidisha ukatili wao pale walipomzawadia medali ya ushujaa nahodha wa meli hiyo kutokana na kitendo hicho kilichoonekana na serikali ya Washington kuwa eti ni cha kishujaa.
Miaka 25 iliyopita katika siku kama ya leo makamanda wa ngazi za juu wa jeshi la Urusi ya zamani wakiongozwa na Gennadi Ivanovich Yanayev walifanya mapinduzi dhidi ya rais wa mwisho wa Muungano wa Sovieti, Mikhail Gorbachev. Wanajeshi hao walitaka kukomeshwa marekebisho ya Gorbachev na kuzuia mpango wa kugawanywa Urusi ya zamani. Wakati wa mapinduzi hayo Mikhail Gorbachev alikuwa katika Peninsula ya Crimea huko kaskazni mwa Bahari Nyeusi. Hata hivyo Boris Yeltsin ambaye wakati huo alikuwa kiongozi wa Federesheni ya Urusi na ambaye alikuwa akiungwa mkono na Magharibi, alizima mapinduzi hayo kwa msaada wa wananchi na baadhi ya watu wenye ushawishi serikalini. Kushindwa kwa mapinduzi hayo kulizidisha uwezo na satua ya Boris Yeltsin na kuharakisha mwenendo wa kusambaratika Urusi ya zamani hapo mwaka 1991.
Siku kama hii ya leo miaka 197 iliyopita alifariki dunia James Watt mvumbuzi na mhandisi wa Kiingereza katika mji wa Greenock huko Scotland. Watt alionyesha hamu kubwa ya kutwalii na kufanya uhaqiqi katika masuala ya kielimu. Katika uhaqiqi wake, mvumbuzi huyo wa Kiingereza alifanikiwa kuvumbua injini inayofanya kazi kwa kutumia mvuke na kwa msingi huo uvumbuzi wake huo ukawa muhimu katika kuleta mabadiliko katika mapinduzi ya viwanda khususan katika sekta ya usafiri wa ardhini na baharini.
Na tarehe 19 Agosti miaka 354 iliyopita alifariki dunia Blaise Pascal, mwandishi, mwanahesabati na mvumbuzi wa mashine ya kuhesabia (calculator) wa Kifaransa. Alizaliwa Juni mwaka 1623 na tangu utotoni Pascal alivutiwa mno na somo la hesabati. Vilevile urafiki uliokuwepo kati ya baba yake Pascal na msomi mmoja maarufu wa zama hizo ulisaidia mno katika kuchanua kipawa na kugunduliwa uwezo wa kijana huyo katika taaluma ya hisabati. Mwishoni mwa umri wake Blaise Pascal alijielekeza mno katika masuala ya dini na kuandika vitabu kadhaa katika uwanja huo.