Sep 05, 2016 08:57 UTC
  • Maafa ya Mina (5)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum. Wazikilizaji wapenzi, tunaendelea na mfululizo wa vipindi vyetu hivi maalumu vya Hija ambapo tunazungumzia kumbukumbu ya tukio chungu la maafa ya eneo takatifu la Mina katika ibada ya Hija mwaka jana 1436 Hijria.

Mara baada ya tukio hilo dunia nzima hasa ulimwengu wa Kiislamu uliripuka kwa malalamiko kutoka kila kona, kulalamikia usimamiaji mbaya wa ibada ya Hija. Waislamu wa maeneo mbalimbali walionesha hasira zao kutokana na uzembe unaofanyika wakati wa msimu wa Hija na kusababisha maafa kwa Waislamu.

Baada ya kutokea tukio hilo, shakhsia mbalimbali walionesha radiamali kali akiwemo Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye alisema kuwa maafa ya kusikitisha sana na ya kutisha ya Mina ni moja ya mitihani ya Mwenyezi Mungu na kusisitiza kuwa, msiba huo mkubwa haupaswi kusahauliwa. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi alisema hayo wakati alipokuwa anahutubia hadhara ya wafanyakazi na wasimamizi wa msafara wa ibada ya Hija wa Iran mwaka jana na kuashiria majukumu ya serikali ya Saudi Arabia ya kukubali kubeba lawama za maafa yaliyotokea ya maelfu ya Waislamu wakati wa tukio hilo na kusema kuwa, ulimwengu wa Kiislamu ulipasa kupaza sauti moja na kulalamikia jambo hilo. 

Ayatullah Khamenei aliongeza kuwa, ni wazi kwamba maafa ya Mina yametokana na uzembe uliofanywa na serikali mwenyeji, lakini kwa hali yoyote ile, suala hio si suala la kisiasa, bali ni kadhia inayowahusu maelfu ya Waislamu ambao wameaga dunia wakati wakitekeleza ibada na amali ya Hija waliopotoza maisha katika mazingira ya kusikitisha mno huku wakiwa katika vazi la Ihram na kwamba  suala hilo inabidi lifuatiliwe kwa uzito wa hali ya juu.

Miongozi mwa Waislamu waliolalamikia uzembe huo walikuwa ni Waislamu wa nchini Kenya. Wakati huo mwandishi wa Radio Tehran alituandalia ripoti maalumu kuhusu suala hilo. 

Mpenzi msikilizaji, tukiendelea na mfululizo wa mwaka huu wa kuzungumzia maafa ya Mina tunakumbusha kuwa, sehemu iliyopita ya mfululizo huu tulikunukulieni kumbukumbu iliyohadhithiwa na Muhammad, mmoja wa mahujaji ambao walikwama vibaya katika msongamano wa Mina kwenye ibada ya mwaka jana ya Hija. Hujaji huyo alizungumzia sheria kali zilizowekwa na maafisa wa Saudi Arabia na kusema kuwa sheria hizo zilikuwa sababu kuu ya kutokea maafa ya Mina. Muhammad alizungumzia pia aliyoyaona baada ya kuanguka winchi ndani ya Masjidul Haram na kuua mahujaji kadhaa. Katika sehemu moja ya simulizi zake alisema: Jambo la kustaajabisha kabisa ni kwamba, njia ya dharura kwa ajili ya kutoka wimbi la mahujaji ilikuwa imefungwa na hofu kubwa ilituingia nyoyoni wakati tuliposikia kuwa askari wa kulinda usalama wa Saudia walikuwa wameifunga njia ya kutokea eneo hilo. Kwa hakika makumi ya maelfu ya mahujaji walikwama katika barabara ya 204, na idadi yao iliongezeka kila sekunde ilivyokuwa inapita. Leo tutaendelea kukunulieni kisa chake akiwa ni mtu aliyeshuhudia kwa macho yake na ambaye alikuwa miongoni mwa waliokumbwa na mkasa huo. 

Muhammad anaendelea kuhadithia kwa kusema: Baada ya tukio chungu la mahujaji kuangukiwa na winchi ndani ya Masjidul Haram, niliona sina njia nyingine ya kuweza kuutuliza moyo wangu ila kwenye msikitini humo na kuwaombea dua mashahidi waliokufa kwenye maafa hayo. Lakini muda wote nilipokuwa naenda msikitini, nilikuwa ninaendelea kuona makumi ya mawinchi yakiwa yamezunguka kona zote za msikiti. Muda wote nilikuwa na wasiwasi kuwa huenda mawinchi hayo yakawaangukia tena mahujaji.

Siku zilipita kwa kasi na baada ya kufanya Umra, ukafika wakati wa kutekeleza ibada ya Hija. Sote tulivaa Ihram na tukajiunga na mahujaji wa nchi nyingine kuelekea Arafa. Mazingira niliyoyaona hapo yalikuwa ni ya kupendeza mno. Mazingira yote yalichukua rangi ya umaanawi katika kila upande. Siku ya Arafa ambayo ni mwezi Tisa Mfunguo Tatu Dhulhijja, tulikusanyika Arafa na kuomba dua maarufu iliyojaa umaanawi ya Imam Husain AS, na kwa hakika mazingira ya hapo yalikuwa ya aina ya kipekee, yasiyoelezeka kwa maneno. Hususan wakati tuliposikia qiraa cha Qur'ani Tukufu kutoka kwa Mohsin Hajji Hasani, qiraa hiyo ya Qur'ani ilileta hali ya kipekee kabisa katika eneo la Arafa. Kiza kilipoingia, kundi kubwa la watu lilianza kuondoka Arafa na kuelekea kwenye aneo jengine takatifu lijulikanalo kwa jina la Mash'arul Haram. Huko nako tulikuwa na kazi moja tu ya kufanya ibada, kuomba dua na kunong'ona na Mola wetu. Baadhi ya mahujaji walianza kukusanya vijiwe kwa ajili ya kwenda kumpiga mawe shetani katika siku itakayofuata kwenye eneo la Mina. 

Mahema ya Arafa

 

Baada ya kuchomoza jua siku ya pili yake na kuingia sikukuu ya Idul Adh'ha, hamasa kubwa iliongezeka kati ya mahujaji, na makundi kwa makundi wakawa wanaelekea kwa shauku na hamasa kubwa kwenye eneo takatifu la Mina. Njia ya kutoka Mash'arul Haram kuelekea Mina ni ndefu kwani masafa ya baina ya maeneo hayo mawili matakatifu ni makubwa. Lakini shauku kubwa tuliyokuwa nayo ya kuendelea kutekeleza amali zilizojaa baraka na utukufu za Hija kwa ajili ya kutafuta radhi za Muumba wetu, zilitufanya tuyaone masafa hayo ni mafupi na tusihisi uchovu kabisa. Hatimaye tulifika mahala ambapo miaka yote Wasaudia huwa wamepatenga kwa ajili ya mahujaji wa Kiirani. Kwa kweli ni eneo lililojaa uchafu na ndiyo sehemu iliyo mbali zaidi  kutoka sehemu ya kumpiga mawe shetani ikilinganishwa na maeneo mengine ya eneo hilo. Tulistaftahi na kufungua kinywa kimuhtasari sana, na pamoja na kwamba tulikuwa na machofu mengi tuliamua tuanze safari mara moja kuelekea eneo la kumpiga mawe shetani ili kukwepa joto kali mno la Mina. Nilikuwa najua kwamba, katika miaka yote ya huko nyuma kumekuwa kukitokea maafa yasiyotarajiwa katika eneo hilo kutokana na usimamiaji mbovu wa maafisa wa Saudi Arabia. Hata hivyo mwaka huu (2015) idadi ya mahujaji imepungua, hivyo kiwango cha matukio kama hayo mabaya hakikuwa kikubwa hadi wakati huu. Pamoja na hayo nilijisemea moyoni kuwa, kutokana na uanagenzi wa maafisa wa Saudia, jambo lolote linaweza kutokea tena wakati wowote kama ambavyo tuliona jinsi mahujaji walivyokuwa wahanga wa kuangukiwa na mawinchi ndani ya Msikiti Mtakatifu wa Makkah kutokana na uzembe huo huo wa maafisa wa Saudi Arabia.

Polisi wa Saudi Arabia waliwaongoza mahujaji wa Kiirani upande wa barabara ya 204. Kibarabara chembamba ambacho kinawapeleka mahujaji hadi kwenye eneo la kufanya ibada ya Jamarati yaani ya kumpiga mawe shetani. ilikuwa ni saa mbili asubuhi wakati huo, na kasi ya mwendo wa kundi kubwa la mahujaji ilikuwa ndogo. Pamoja na kibarabara hicho kuwa chembamba, mara tuliona polisi wa Saudia wanawaongoza mahujaji wa Kiafrika kuingia katika barabara hiyo hiyo ya 204. Jambo hilo lilitustaajabisha sana. Baada ya kumiminika wimbi hilo kubwa la mahujaji wa Kiafrika walioingizwa kwenye barabara ya 204 kutoka barabara nyingine, kasi ya kusonga mbele mahujaji katika barabara hiyo ilizidi kuwa ndogo na kila sekunde jekejeke na fukuto la joto kali liliongezeka. Mkuu wa msafara wetu alitumia uzoefu wake wa miaka mingi alitutuliza nyoyo na kutwambia kuwa, katika kila kona ya eneo hilo kuna kamera, na maafisa wa Saudi Arabia huwenda wakafungua njia nyingine ili kupunguza msongamano huo mkubwa. Lakini cha kustaajabisha zaidi ni kuona kuwa njia nyingine za kutokea kwenye barabara ya 204 nazo zilikuwa zimefungwa. Fadhaa kubwa zaidi ilitukumba baada ya kusikia kuwa hata hiyo barabara ya 204 nayo ilikuwa imefungwa katika eneo la mwisho la kutokea. Kwa hakika makumi ya mahujaji tulikuwa tumekwama katika barabara ya 204, hatuwezi kwenda mbele na wala kurudi nyuma, na kila sekunde idadi ya mahujaji waliendelea kumiminika kwenye barabara hiyo.

Sehemu palipotokea maafa ya Mina

 

Hali yetu ilizidi kuwa mbaya kila sekunde. Maji yetu ya kunywa yalikuwa yameisha, na uchovu na fukuto la joto kali vilitumaliza nguvu mwilini. Kiongozi wa msafara wetu alitwambua, karibu na hapo palikuwa na vituo viwili vya Wasaudi kwa ajili ya kuwasaidia mahujaji, na tuliingia tamaa kuwa wangelikuja maafisa wa Hija kuja kutusaidia angalau kwa kuwapa maji mahujaji. Lakini hilo halikutokea. Inaonekana Wasaudia waliamua kuwafanya mahujaji wahanga wa sikukuu ya Idul Adh'ha badala ya kondoo wanaochinjwa siku hiyo. Naam, Ilipofika saa tatu asubuhi, mahujaji dhaifu walianza kuzimia baada ya kuzidiwa nguvu na fukuto la joto kali, uchofu na kiu. Sote tulielekeza matumaini yetu kwa Mwenyezi Mungu kwani ni kwa ajili ya kutii amri Zake na kutafuta radhi Zake ndio maana tumekuja katika ardhi hii. Lakini cha kusikitisha ni kuwa amali hii tukufu inasimamiwa na watawala ambao hawana uwezo kabisa wa kuisimamia. Wale waliokuwa bado wana nguvu za kupumua, walienedelea kunong'ona na Mola wao wakitaradhia msaada kutoka Kwake ili awaokoe na mtihani huo mkubwa waliokuwa wametumbukizwa ndani yake. Kufikia hapo tulikuwa tumeshapata yakini kwamba tumekwama kwenye kinamasi kikubwa na ni muujiza wa Mwenyezi Mungu tu ndio ungeliweza kutuokoa na msongamano, joto kali na mauti ambayo yangelitufika sekunde yoyote kutokea wakati huo.

Barabara ya 204 

Wapenzi wasikilizaji sehemu nyingine ya simulizi za Hujaji huyu wa Kiirani ambaye aliokoka katika maafa ya kutisha ya Mina mwaka jana, imeisha kwa leo. Tutaendelea kukuleteeni simulizi hiyo katika sehemu ya sita ya mfululizo huu. Ishini Salama.

 

Kwa maelezo zaidi kuhusu Maafa ya Mina: http://kiswahili.irib.ir/habari/mina

Kwa maelezo zaidi kuhusu makala za Hija: http://kiswahili.irib.ir/uislamu/hija

Tags