Nov 08, 2016 12:14 UTC
  • Familia Salama (12)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nasi katika mfululizo huu wa makala kuhusu Familia Salama.

Makala hizi huangazia masuala mbali mbali ya afya ya familia kama vile lishe, mazoezi, madhara ya matumizi ya mihadarati, umuhimu wa mahaba katika familia n.k. Katika makala ya leo tutatendelea kuangazia kuhusu tatizo sugu la mihadarati au dawa za kulevya. Karibuni kujiunga nasi hadi mwisho.
Katika makala yetu iliyopita tuliashiria kuhusu nafasi ya familia katika uraibu wa mihadarati na tukasema wazazi na walezi wana nafasi muhimu sana katika kuzuia vijana na mabarobaro kutumbukia katika uraibu wa dawa za kulevya. Tulisema utegemezi wa dawa za kulevya ni ugonjwa sugu lakini unaotibika.
Kwa mtazamo wa wataalamu wengi wa afya, uraibu ni ugonjwa ambao una mkondo wake wa kuingia mwilini hatua kwa hatua. Utumizi wa mihadarati huanza kwa utumizi mdogo kisha utumizi wa wastani na hatimaye utumizi wa kudumu ambao ni uraibu.
Waraibu wengi wa mihadarati wanapoanza utumizi huwa hawadhani kuwa watatumbukia katika uraibu.
Kwa kawaida watu wengi ambao hukumbwa na ugonjwa huwa hawajui kiasi ambacho ugonjwa huo umesonga mbele katika uharibifu na wakati wanapofahamu uhalisia wa mambo, huwa muda umeshapita sana na hivyo kufanya matibabu kuwa magumu.
Halikadhalika jamaa pia katika familia kwa kawaida huchelewa kubaini kuwepo tatizo la uraibu na wengi hutambua tatizo wakati wanapoona muathirika ameanza kupata matatizo ya kiakili na kitabia.
Mwanzoni wa tatizo, wanafamilia kwa kawaida hujiliwaza kwa kutokubali ukweli wa mambo na kulifanya tatizo kuwa dogo na wala huwa hawadhani litabadilika hatua kwa hatua na kuwa tatizo sugu la uraibu.
Lakini wakati tatizo la uraibu linapokuwa shahidi, kutafuta mihadarati huwa ndio kazi pekee ya mwenye uraibu na hapo huanza kukata uhusiano na familia.

 

Hii ni katika hali ambayo uhusiano baina ya mraibu wa mihadarati na familia hubadilika na kuwa tatizo na masaibu kwa familia yake, jamii na nchi kwa ujumla.
Wanafamilia huanza kushuhudia mabadiliko katika tabia za mraibu lakini wakati mwingine huwa wanashindwa kudiriki ni kitu gani hasi kinachojiri. Kile ambacho huwa wazi ni kuwa, nyumba huwa haiwezi tena kuwa mahala salama bali hugeuka uwanja wa malumbano, wasi wasi, na hitilafu. Mwenye kukumbwa na uraibu wa mihadarati hubadilika na kuwa tofuati kabisa na vile wanafamilia walivyokuwa wamemzoea na huwa tena hana hamu ya kuwa kando ya wanafamilia wenzake.
Wakati familia inapokumbana na mwanafamilia aliyetumbukia katika uraibu wa dawa za kulevya, huanza kuchukua hatua za kukabiliana na hali hiyo mbaya. Kwa mfano wazazi, mwanandoa, au watoto wa mraibu wa mihadarati hujaribu kuficha aibu iliyoikumba familia na hata wakati mwingine kumtetea. Jambo kama hili hupelekea mwenye uraibu kuzidi kutumbukia katika ugonjwa huo.

Aidha mtindo wa maisha ya familia hubadilika kutokana na kuwepo mraibu ndani yake. Familia nyingi hukumbwa na matatizo ya kifedha, kijamii na hata kiusalama kutokana na kuwepo mwanafmailia mwenye uraibu wa mihadarati.
Kwa mfano iwapo katika familia mume ni mraibu wa mihadarati na kama ndiye aliyekuwa tegemeo la pato, mama hulazimika kutafuta kazi ili kukidhi mahitaji ya familia. Na katika familia ambazo wazazi wote ni waraibu, jukumu hili huachiwa watoto.
Kwa hivyo tunaona namna tatizo la uraibu wa dawa za kulevya unavyoandamana na matatizo mengi ambayo huvuruga msingi wa familia.
Wapenzi wasikilizaji, mojawapo ya mambo yanayotisha kuhusu madawa ya kulevya ni athari zake mbaya kwa mwanadamu kiakili na kimwili. Na ni wazi kuwa athari zake ni za kiwango cha juu. Madhara ya dawa za kulevya yanategemea aina, kiwango na jinsi zitakavyotumika. Aidha madawa hayo yanategemea umri, afya ya mwili na ukomavu wa kiakili na mazoea ya matumizi ya madawa hayo. Madhara ya muda mfupi huonekana punde tu madawa hayo yakishatumiwa, huku yale ya muda mrefu yakionekana baada ya muda kupita, na mara nyingi husababisha kuongezeka kwa mapigo ya moyo, matatizo ya kumbukumbu ya muda mfupi pamoja na kupoteza umakini wa kujifunza, kufikiri n.k. Aidha madawa hayo yanaweza kusbabisha ulemavu wa aina fulani katika muundo wa viungo vya mwili.
Aidha madawa ya kulevya yanayodaiwa kuwa ni vichangamsho kama kokaini, huwafanya watumiaji kujiona wana nguvu na kujiamini. Matumizi ya madawa ya kulevya kwa muda mrefu husababisha matatizo ya akili na kifo. Madawa kama heroin humhadaa mtumiaji wake na kujihisi kuwa mtulivu, mwenye amani na furaha na hatimaye kumsababishia usingizi wa muda mrefu, kuzimia na hata kifo. Kiujumla tunaweza kusema kuwa, matumizi ya dawa za kulevya hupunguza uwezo wa vijana kuhimili na kutatua matatizo ya kijamii na kiakili. Aidha huwachochea vijana kujitumbukiza katika vitendo vya ujambazi, ngono na fujo. Takwimu mbalimbali zinaonyesha kuwa, utumiaji wa dawa za kulevya ni chanzo kikuuu cha ajali nyingi za barabarani, visa vya kujiuwa na maambukizo ya magonjwa hatari miongoni mwa kizazi cha vijana ulimwenguni na hivyo kuhatarisha misingi ya familia.

 

Kwa kuzingatia hayo, kuna haja ya kuwepo jitihada za kimataifa za kukabiliana na biashara ya dawa za kulevya. Hata hivyo kutokana na kuwa biashara ya mihadarati duniani ina faida ya mabilioni ya dola kila mwaka, inakuwa vigumu kwa serikali nyingi kukabiliana na tatizo hilo. Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2016 ya Bodi ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Bara la Afrika liliendelea kutumika kupitishia dawa za kulevya. Afrika Magharibi ilitumika mara kwa mara kupitishia Cocaine na dawa nyingine kuelekea bara la Ulaya wakati Afrika ya Kaskazini iliendelea kuwa chanzo kikuu cha dawa zilizoingia barani Ulaya. Kutumika kwa Afrika ya Mashariki kama kitovu cha kusafirishia heroin iliyotokea Afghanistan ikipelekwa bara la Ulaya kuliongezeka. Hali hii inachukuliwa kuwa ndiyo sababu ya kuongezeka kwa matumizi ya heroin katika eneo la Afrika ya Mashariki. Kwa maelezo hayo, kunahitajika jitihada maradufu za wanasiasa, wanaharakati wa kijamii na viongozi wa kidini ili kukabiliana na tatizo hilo ili kulinda familia na mustakabali wa familia za Afrika na jamii nyinginezo duniani.