Nov 08, 2016 12:18 UTC
  • Familia Salama (13)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nasi katika mfululizo huu wa makala kuhusu Familia Salama.

Makala hizi huangazia masuala mbali mbali ya afya ya familia kama vile lishe, mazoezi, madhara ya matumizi ya mihadarati, umuhimu wa mahaba katika familia n.k. Katika makala ya leo tutaendelea kuangazia tatizo sugu la mihadarati au dawa za kulevya. Karibuni kujiunga nasi hadi mwisho.

Katika makala yetu iliyopita tulisema kuwa, kutumika kwa eneo la Afrika ya Mashariki kama kitovu cha kusafirishia heroin iliyotokea Afghanistan ikipelekwa bara Ulaya kumeongezeka. Hali hii inachukuliwa kuwa ndiyo sababu ya kuongezeka kwa matumizi ya heroin katika eneo la Afrika Mashariki. Kwa maelezo hayo, kunahitajika jitihada maradufu za wanasiasa, wanaharakati wa kijamii na viongozi wa kidini ili kukabiliana na tatizo hilo ili kulinda familia na mustakabali wa familia za Afrika na jamii nyinginezo duniani. Wapenzi wasikilizaji, kati ya matatizo sugu ambayo familia zinakumbana nayo leo ni kuwepo watoto wenye uraibu wa dawa za kulevya.
Katika familia kama hizi, wazazi hudhani kuwa, utendaji wao mbovu ndio sababu ya waototo wao kutumbukia katika uraibu na hivyo huhisi kuwa ni wenye kulaumiwa.
Watoto waraibu nao hutumia vibaya hali hii ya wazazi kujihisi ndio wanaopaswa kulaumiwa kutokana na uraibu wao wa dawa za kulevya. Kwa hivyo watoto kama hawa huendelea kutumbukia zaidi katika uraibu wao huku wakiwalaumu wazazi kuwa ndio waliowasababishia tatizo wanalokumbana nalo.
Wakati wazazi au wanafamilia wanapohisi kuwa ndio wanaobeba lawama za walio na uraibu miongoni mwao, jambo hili hupelekea baadhi kuanza kumtetea mwenye uraibu na jambo hilo kuandamana na madhara makubwa.

 

Kwa mfano, iwapo mama atahisi kuwa hakuwa mama mzuri kwa watoto wake na kwamba hakuweza kuwalea vizuri, au kuhisi kuwa hakumpenda mwanae ipasavyo na hakumuonyesha mahaba na hii ndio sababu iliyompelekea mwanae kuwa mraibu; jambo kama hili humpelekea kujaribu kuficha uraibu wa mwanae au hata kutetea tatizo hilo. Katika hali kama hiyo mzazi hufika hata kiasi cha kumpa mwanae fedha za kukidhi mahitaji yake ya mihadarati na kimaisha.
Mwenendo kama huu na uungaji mkono usio salama hupelekea mwenye uraibu wa mihadarati kujisahau na kutodiriki uzito wa tatizo alilonalo na hivyo kuendeleza uraibu wake.
Katika upande mwingine, wakati wanafamilia wanapokumbana na changamoto zisizo na kikomo kutokana na kuwepo mraibu wa mihadarati, wengi hukumbwa na hali ya kupoteza matumaini kuhusu kupona mraibu huyo.
Hasira na ghadhabu zinazotokana na uraibu wa mmoja wa wanafamilia ni jambo ambalo hupelekea kuchanganyikiwa na kupoteza matumaini mraibu na wanafamilia wengine. Hii ni kwa sababu kadiri wanavyojitahidi kuhakikisha mtu mwenye uraibu anaacha tabia yake hiyo, aghalabu huona jitihada zao zinaambulia patupu ambapo mraibu huendelea na tabia zake zenye kuudhi na kuleta madhara kwake binafsi, kwa familia, jamii na nchi nzima kwa jumla. Hali kadhalika wanafamilia wengi hujaribu kulinda heshima ya familia yao ili tatizo la urabu wa mmoja wao lisifahamike na wengine. Lakini jambo kama hilo si tu kuwa halimsaidii mraibu bali humpelekea kukumbwa na mfadhaiko wa nafasi na kuendelea kudhoofika. Hali kadhalika ni vigumu kuficha tatizo hilo kwa muda mrefu hasa iwapo uraibu umesonga mbele na kufika kiwango cha juu. Ni bora kuliweka wazi tatizo la uraibu hasa kwa watu wanaoweza kusaidia au kutoa mchango wa aina fulani katika kulitatua kama vile viongozi wa kidini, washauri wa kijamii n.k

Kwa mtazamo wa wataalamu, iwapo tatizo la uraibu wa mmoja kati ya watoto wa familia limejiri, kunapaswa kuchukuliwa hatua za kuzuia watoto wengine katika familia kutumbukizwa na mwenzao katika uraibu.
Awali ni kuwa, wazizi wanapaswa kujifunza kuhusu mihadarati iliyosababisha uraibu kama vile aina ya mihadarati, namna inavyotumiwa, sababu na chanzo cha kuanza utumizi na vile vile madhara ya utumizi wa mihadarati.
Wazazi wanapaswa kufahamu kuwa kwa kawaida watoto huwa wanataka kujua na huwa na maswali mengi kuhusu mihadarati na hilo ni jambo la kawaida. Hivyo wanapaswa kujitahidi kuwajibu kwa kuwapa maelezo kamili kuhusu mihadarati na madhara yake.
Kwa mfano, yamkini mtoto akamuuliza baba yake iwapo amewahi kutumia mihadarati au la. Mzazi anapaswa kuwa tayari kujibu swali hili kwa umahiri.
Wataalamu wanasema mzazi anapaswa kuwa tayari kumfahamisha mwanae kwa maneneo sahali na yanayofahamika kuhusu sababu ya yeye kutotumbukia katika uraibu wa mihadarati. Iwapo mzazi amewahi kutumia mihadarati anapaswa kumfahamisha mtoto ni kwa nini hapaswi kurudia kosa kama hilo.
Katika kubainisha hilo mzazi pia hapaswi kutoa maelezo kupita kiasi kwani yamkini jambo hilo likamfanya mtoto awe na hamu ya kujaribu uzoefu aliopitia mzazi wake.
Wataalamu wanasisitiza sana suala la wazazi kuwa na mahaba na upendo kwa watoto ili kuwazuia kutumbukia katika uraibu wa mihadarati.
Kuna haja kwa jamii kuacha tabia ya kuwanyanyapaa watumiaji wa dawa za kulevya kwa kuwaona watu wasiofaa badala ya kuwapenda na kutumia mwanya huo kuwashauri waachane na uraibu.
Kwa msingi huo kuna haja ya kuwepo mipango maalumu ya kuwaelimisha wanafamilia na wanajamii kuepuka kuwanyanyapaa watumiaji wa mihadarati.

 

Ni wazi kuwa, kwa kuwaonesha wenye uraibu upendo inakuwa rahisi kuwapa elimu ya kuachana na uraibu kuliko kuwaadhibu kwa kuwafunga jela.
Kama tulivyotanuglia kusema ugonjwa wa uraibu pia huandamana na magonjwa mengine hatari. Mraibu sio tu atadhoofisha kinga ya mwili, lakini pia anajiweka katika tabia hatarishi ya matumizi ya kujidunga sindano na kufanya ngono isiyo salama. Mchanganyiko huu wa tabia huongeza maradufu hatari ya kuambukizwa HIV, virusi vya hepatitis na magonjwa mengine mengi.
Matibabu ya uraibu wa mihadarati yamegawanyika katika makundi makuu mawili, nayo ni matibabu ya ushauri nasaha kuhakikisha mtumiaji anabadili tabia na pili ni matumizi ya dawa ambazo hutibu dalili za ugonjwa pamoja na kumwezesha mtumiaji kuachana na matumizi ya dawa hizi hatari.
Kwa kumalizia tunashauri kuwa iwapo kuna mtumiaji wa dawa za kulevya ni vyema afikishwe kwa daktari au mfamasia katika kituo cha afya kilicho karibu kwa ushauri zaidi. Ni vyema kuwahi mapema ili kuepuka madhara anayoyapata mtu baada ya matumizi ya muda mrefu.

 

 

Tags