Nov 21, 2016 08:00 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Nov 21

Mkusanyiko wa matukio kemkem ya spoti kutoka kila pembe ya dunia ndani ya siku saba zilizopita.........

Taekwondo: Wairani wazoa medali 5 Canada

Wanamichezo wa taekwondo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamenyakua jumla ya medali 5 katika duru ya 11 ya Mashindano ya Mabingwa wa mchezo huo nchini Canada, zikiwemo dhahabu 2. Amir Mohammad Makhshi aliipa Iran dhahabu ya pili siku ya Ijumaa katika kitengo cha wanataenwondo barubaru wenye kilo zisizozidi 63 upande wa wanaume, baada ya kumlemea Nikita Pishanko wa Russia kwa pointi 4-0, mchezo ulipigwa katika uwanja wa michezo wa Bill Copeland mjini Burnaby, magharibi mwa Canada. Siku ya Jumatano Mobina Nejad-Katesari aliipa Iran ya Kiislamu dhahabu ya kwanza katika kategoria ya wanawake wenye kilo zisizozidi 42 baada ya kumchachafya Mhispania Irene Laguna Perez. Wairani wengine waliotia kibindoni medali ni Mobina Babalou aliyepata shaba kitengo cha wenye kilo zisizozidi 55 upande wa akina dada, Ali Baseri medali ya shaba kategoria ya chini ya kilo 55 safu ya wanaume na Parisa Javadi, shaba nyingine safu ya kilo zisizozidi 63 upande wa akina dada siku ya Jumamosi. Mashindano hayo ya dunia yanayofahamika kama World Junior Taekwondo Championships yanayoandaliwa na Shirikisho la Taekwondo Duniani WTF, yalianza Novemba 16 na kufunga pazia lake Novemba 20 nchini Canada, kwa kuwalate pamoja wanataekwondo mabarobaro kutoka nchi 102, zikiwemo Azerbaijan, Bulgaria, Chinese Taipei, Croatia, Cyprus, India, Iran, Mexico, Mongolia, Ufilipino, Russia, Serbia, Korea Kusini, Uhispaani, Uturuki, na Marekani.

Soka: Esteghlal yatinga robo fainali Kombe la Hafzi

Klabu ya soka ya Esteghlal ya Tehran imejikatia tiketi ya kushiriki robo fainali za kuwania Kombe la Mtoano (Hazfi), baada ya kuizaba Saba ya Qom mabao 4-3. Dakika 90 za ada na 30 za ziada hazikuwezi kuamua nani zaidi kati ya timu mbili hizo, katika kipute kilichopigwa ugani Azadi hapa Tehran. Ilibidi mshindi atafutwe kupitia mikwaju ya penati, ambapo The Blues wa Tehran waliibuka washindi wa mabao 4-3.

Timu ya Esteglal ikishangilia bao

Kwa ushindi huo Esteghlal itavaana na Naft ya Tehran katika mchuano wa robo fainali. Kwengineko Naft Gachsaran iliitandika Foolad mabao 3-2 kupitia mikwaju ya penati, namna ambavyo Zob Ahan iliwachapa Watengeneza magari wa Mashin Sazi. Arak na Naft Masjid Suleyman ziligaragazwa mabao 2-1 na Sepahan na Saipa kwa usanjari huo. Orodha ya mechi zilizotinga robo fainali za Kombe la Mtoano ama Hazfi Cup ni hivi: Naft Tehran watatoana udhia na Esteghlal; Sepehan watavaana na Saipa wakati ambapo Watengeneza trekta wa Teraktor Sazi watakua wapimana nguvu na Wachimba mafuta wa Naft Gachsaran. Aidha tutajua nani zaidi kati ya Gostareh Foolad na Zob Ahan katika mechi ya mwisho ya robo fainali ya Kombe la Mtoano.   

Tusker yatwaa Ligi Kuu ya Soka Kenya

Tusker FC wametawazwa rasmi ubingwa wa ligi kuu ya soka nchini Kenya baada ya kukamilika kwa msimu wa ligi nchini humo. Watengeneza mvinyo hao walitunukiwa kombe hilo katika uwanja wa Nyayo jijini Nairobi. Mabingwa hawa wapya wenye makao yake katika mtaa wa Ruaraka jijini Nairobi, ulikuja wiki mbili zilizopita lakini, walikuwa wanasubiri mchuano wa mwisho siku ya Jumamosi dhidi ya mabingwa wa zamani Gor Mahia, ili kutawazwa rasmi. Mabingwa hawa wapya walimaliza vizuri baada ya kupata ushindi katika mchuano wake wa mwisho, kwa kuifunga Gor Mahia bao 1-0 kupitia mshambuliaji Allan Wanga. Baada ya mechi 30, Tusker FC imeshinda ligi kwa alama 61 huku Gor Mahia ikiwa ya pili kwa alama 54. Ulinzi Stars imemaliza katika nafasi ya tatu kwa alama 46, Posta Rangers ya nne kwa alama 45 sawa na Chemelil Sugar ambayo imemaliza katika nafasi ya tano. Tusker FC sasa imeshinda taji hili mara 11. Gor Mahia bado inashikilia rekodi ya ubingwa nchini humo kwa kunyakua mataji hilo mara 15 ikiwa ni pamoja na kushinda taji hilo mara tatu mfululizo mwaka 2013, 2014 na 2015.

Michuano ya Kombe la AFCON upande wa wanawake yaanza

Duru ya 12 ya michuano ya soka ya timu za mataifa ya Afrika kwa upande wa wanawake ilifungua jamvi lake Jumamosi katika mji mkuu wa Cameroon, Yaounde. Licha ya akina dada wa Harambee Starlets ya Kenya kuanza vizuri mchuano wake na Black Queens ya Ghana katika mechi yake ya ufunguzi, lakini hatimaye iliondoka uwanjani kimya kimya baada ya kuzabwa mabao 3-1 mjini Limbe, siku ya Jumapili. Katika mechi iliyotangulia Jumapili, miamba Super Falcons wa Nigeria walituma onyo kwa mahasimu wa kundi lao, baada ya kuisasambua Mali mabao 6-0.

Nigeria itatoana jasho na Ghana huku Kenya ikitazamiwa kuvaana na Mali katika mechi zao za pili za kundi B mnamo Novemba 23. Wenyeji Indomitable Lionesses ya Cameroon wanaongoza kundi A na pointi tatu baada ya kushinda Misri 2-0 siku ya kwanza ya mashindano mnamo Novemba 19. Afrika Kusini na Zimbabwe ziligawana pointi moja kila moja baada ya kutoka sare tasa.

Tenisi: Murray ang'ara na kutwaa Kombe la ATP

Mchezaji tenisi nyota wa Uingereza Andy Murray ametwaa Kombe la ATP baada ya kumgaragaza hasimu wake Novak Djokovic katika fainali za mashindano hayo ya kimataifa. Murray amemchachafya hasimu wake seti 2 za 6-3, 6-4, katika mchezo uliovutia hisia za wengi katika uwanja wa O2 arena mjini London.

Mchezo wa tenisi

Baada ya ushindi huo wa kufana, Murray alisema: "Nina furaha kubwa sana kuwa mshindi, na kuwa namba moja duniani ni kitu cha kipekee sana". Alisema Murray. Akiongeza kuwa ni nafasi ya kipekee sana kushindana na Novak katika mashindano kama haya. Murray, mwenye umri wa miaka 29, amekuwa mchezaji bora katika mashindano 24. Mashindano hayo pia yalimalizika kwa ushindi wa miaka minne wa Djokovic katika kinyan'ganyiro na Msebia huyo huku akimkaribia Roger Federer's. Murray aliyeshinda vikombe 34 kwa mara kumi amebainisha kuwa, na hapa tinamnukulu tena: "Kabla ya hapa tumekuwa tukichuana katika fainali mbalimbali na katika Olimpiki lakini ninayo furaha kubwa kuwa mshindi."

………………………..………TAMATI…………………………….