Suratul Qas'as 59-63 (696)
Sura ya Al-Qas’as’, aya ya 59-63 (Darsa ya 696)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 696, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 28 ya Al-Qas’as’. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 59 ambayo inasema:
وَمَا كَانَ رَبُّكَ مُهْلِكَ الْقُرَى حَتَّى يَبْعَثَ فِي أُمِّهَا رَسُولا يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِنَا وَمَا كُنَّا مُهْلِكِي الْقُرَى إِلاَّ وَأَهْلُهَا ظَالِمُونَ
Na Mola wako Mlezi haangamizi miji mpaka ampeleke Mtume katika miji yake mikuu awasomee Aya zetu. Wala hatuiangamizi miji mpaka watu wake wawe madhaalimu.
Katika darsa iliyopita tuliona jinsi Allah SW alivyowajibu watu ambao hawakuwa tayari kuiamini na kuifuata haki kwa sababu ya kulinda dunia yao kwa kuwaambia: Nyinyi mumejionea kwa macho yenu mabaki na magofu ya maskani ya kaumu zilizopita ambazo watu wake ziliwalevya raha na starehe za dunia wakaasi na kupindukia mipaka, nasi tukawaangamiza.
Baada ya hayo, aya ya 59 tuliyosoma inataja kanuni na kaida moja kuu ya Allah katika zama zote za historia na kueleza kwamba: bila ya shaka Mola Mlezi wa ulimwengu hawaangamizi watu bila ya kuwapelekea kwanza Mtume wa kuwafikishia ujumbe wake. Kwa hakika amri ya Mwenyezi Mungu ya kuteremshwa adhabu hutolewa baada ya watu kuwa wamezisikia aya zake Mola kisha wakazikadhibisha. Ikiwa watu watafikiwa na Mtume wa Allah, wakausikia wito wa wahyi utokao kwa Mola, lakini wakaamua kumpinga mjumbe huyo wa Allah na kuamiliana na yeye na dini aliyokuja nayo kidhulma, hufikwa na adhabu na kuangamizwa papa hapa duniani. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba Mwenyezi Mungu hawaadhibu watu kabla ya kutimiza dhima ya kuwafikishia uongofu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kuwakadhibisha Mitume na kusimama dhidi ya haki ni dhulma kubwa ambayo Mwenyezi Mungu anailipia adhabu yake papa hapa duniani.
Tunaiendeleza darsa yetu hii kwa aya ya 60 na 61 ambazo zinasema:
وَمَا أُوتِيتُم مِّن شَيْءٍ فَمَتَاعُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَزِينَتُهَا وَمَا عِندَ اللَّهِ خَيْرٌ وَأَبْقَى أَفَلا تَعْقِلُونَ
Na chochote mlicho pewa ni matumizi ya maisha ya dunia na pambo lake. Na yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu ndio bora na yatakayo baki zaidi. Basi je, hamfahamu?
أَفَمَن وَعَدْنَاهُ وَعْدًا حَسَنًا فَهُوَ لاقِيهِ كَمَن مَّتَّعْنَاهُ مَتَاعَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ثُمَّ هُوَ يَوْمَ الْقِيَامَةِ مِنَ الْمُحْضَرِينَ
Je! Yule tuliye muahidi ahadi nzuri, tena naye akaipata, ni kama tuliye mstarehesha kwa starehe za maisha ya duniani, na kisha Siku ya Kiyama akawa miongoni mwa wanao hudhurishwa?
Aya hizi pia zinawajibu watu ambao kwa kisingizio cha kulinda maisha na neema zao za kidunia hawakuwa tayari kuiamini na kuifuata haki kwa kuwauliza: Je yale ya neema yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu, na yale mliyonayo nyinyi katika dunia hii ya kupita mnayahisi yako sawa, hata hamko tayari kuacha neema hizi za kimaada kwa ajili ya kuzipata neema za milele za Allah? Neema na starehe za kidunia zimeyatia upofu macho yenu na kushindwa kuziona neema za kimaanawi na saada ya milele ya akhera; na hamko tayari kuzifumbia macho na kuzisamehe kwa ajili ya neema hizo za milele? Sehemu ya mwisho ya aya ya 60 inauashiria mwenendo huo kuwa ni kitu kisichokubalika kiakili kwa kuwauliza watu hao je hamtumii akili? Naam; ulinganishaji wa kawaida kabisa humfanya mtu yeyote mwenye akili afahamu kwamba haipasi kupoteza neema za milele kwa sababu ya neema za kupita. Kisha aya zinaendelea kwa kulinganisha hali ya watu wanaoangalia mambo kwa dhahiri yake tu na wale wanaozingatia uhalisia, ambao ni waumini, na kueleza kwamba: wale ambao leo duniani wana yakini na ahadi ya Mwenyezi Mungu na wanafanya amali zao kwa ajili yake Mola, Siku ya Kiyama watalipwa malipo mema; amma wale ambao nyoyo zao zimetekwa na dunia hii ya kimaada na ikawalevya dunia hii ya kupita, badala ya Siku ya Kiyama kuwa na masurufu na zawadi ya taqwa watabeba mzigo mzito wa madhambi yao na kuingizwa kwenye moto wa Jahannam. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba neema za duniani na za akhera, zote zinatoka kwa Mwenyezi Mungu. Hivyo tutahadhari neema zenye mpaka na za kupita za dunia zisije zikatukosesha neema zisizo na mpaka na za milele za akhera; kwa sababu tutakuwa wenye kula hasara isiyomithilika. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa alama ya mtu mwenye akili ni yule asiyetekwa na dunia ya kupita; ambaye hayuko tayari kuyauza makaazi yake ya milele ya akhera kwa haya ya muda ya dunia hii. Badala ya kuhadaiwa na vitu vya dhahiri vya maisha ya dunia, tujitahidi kufikiria zaidi hatima na mwisho wetu. Tuelewe kwamba matokeo ya kushughulishwa na raha za dunia kutokana na mghafala ni idhilali ya kuingizwa kwenye moto wa Jahannam.
Darsa ya 696 ya Qur’ani inahatimishwa na aya ya 62 na 63 ambazo zinasema:
وَيَوْمَ يُنَادِيهِمْ فَيَقُولُ أَيْنَ شُرَكَائِيَ الَّذِينَ كُنتُمْ تَزْعُمُونَ
Na siku atakapo waita na akasema: Wako wapi mlio kuwa mkidai kuwa ni washirika wangu?
قَالَ الَّذِينَ حَقَّ عَلَيْهِمُ الْقَوْلُ رَبَّنَا هَؤُلاء الَّذِينَ أَغْوَيْنَا أَغْوَيْنَاهُمْ كَمَا غَوَيْنَا تَبَرَّأْنَا إِلَيْكَ مَا كَانُوا إِيَّانَا يَعْبُدُونَ
Watasema wale iliyo thibiti juu yao kauli: Mola wetu Mlezi! Hawa ndio tulio wapoteza. Tuliwapoteza kama tulivyo potea sisi. Tunajitenga nao mbele yako. Hawakuwa wakituabudu sisi.
Aya hizi zinaashiria hali ya washirikina Siku ya Kiyama na kueleza kwamba: Wao Siku ya Kiyama hawatokuwa na msaidizi wala kimbilio lolote na wataambiwa na Allah SW: Wako wapi leo wale ambao duniani mlikuwa mkiwafanya washirika wangu katika masuala ya maisha? Kisha aya zinaendelea kwa kueleza kwamba: viongozi wa shirki na ukafiri ambao walikuwa wakitiiwa na kuabudiwa na watu hapa duniani watasimama na kusema: “wao wanadai tu kwamba walikuwa wakitutii na kutufuata sisi na kwamba sisi tulikuwa tukiabudiwa na wao. Lakini ukweli hauko hivyo; wao walikuwa wakifuata matamanio ya nafsi zao. Wakitufuata sisi kwa ajili ya kupata matakwa yao; hivyo wakapotea kama tulivyopotea sisi. Kwa hivyo kwa kweli sisi hatukuwa waola na maabudu wao; na kwa hilo tunajibari na kujiweka mbali nao.” Taswira inayotolewa na aya hizi kuhusu mahakama ya Siku ya Kiyama inafanana na mahakama za duniani, ambapo wakati wahalifu wanapotiwa mbaroni kwa kushirikiana katika uhalifu wa wizi au jinai nyengine waliyofanya, kila mmoja wao humtupia mwenzake mzigo wa dhambi ya uhalifu, na yeye mwenyewe kujisafisha na kujitoa hatiani. Watu waovu watasema tulihadaiwa na wenzetu ndipo tukaishia katika njia hii. Lakini hao watakaowatupia mzigo wa lawama watawaambia, msitubebeshe sisi mzigo wa madhambi yenu, ni nyinyi wenyewe mliasi na kupotoka. Ni wazi madai hayo na kulaumiana kwao huko hakutowasaidia kitu mbele ya mahakama ya uadilifu ya Allah, bali kila mmoja atapata malipo ya amali zake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kutasawari juu ya kuwepo watu au vitu vyenye hadhi sawa na Mwenyezi Mungu na kuvifanya kuwa ni washirika wa Allah ni imani hewa, dhanifu na iliyo mbali na ukweli wa mambo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa mtu yeyote anayewataka watu wamfuate na kumwabudu yeye badala ya Mwenyezi Mungu atafikwa na adhabu kali Siku ya Kiyama. Vilevile tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba watu waliohadaiwa na kupotea huwa wanataka kuwapoteza watu wengine pia. Aidha aya hizi zinatutaka tuelewe kuwa Siku ya Kiyama viongozi na wafuasi wao waliowafuata kwenye upotofu kila mmoja atajibari na kujiweka mbali na mwenzake. Lakini hilo halitokuwa na faida yoyote kwao; na wao wote watatiwa kwenye moto wa Jahannam. Kwa haya machache tunaifunga darsa yetu hii. Tunamwomba Allah atupe mema duniani na akatupe mema akhera na atulinde na adhabu ya moto. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/