Sura ya Al-A'nkabut, 8-13 (704)
Sura ya Al-A'nkabut, aya ya 8-13 (Darsa ya 704)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 704, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 29 ya Al-A'nkabut. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 8 na ya 9 ambazo zinasema:
وَوَصَّيْنَا الإِنسَانَ بِوَالِدَيْهِ حُسْنًا وَإِن جَاهَدَاكَ لِتُشْرِكَ بِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ فَلا تُطِعْهُمَا إِلَيَّ مَرْجِعُكُمْ فَأُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ
Na tumemuusia mwanaadamu kuwafanyia wema wazazi wake. Na ikiwa watakushikilia unishirikishe Mimi na usiyo kuwa na ujuzi nayo, basi usiwat'ii. Kwangu Mimi ndio marejeo yenu, na nitakwambieni mliyo kuwa mkiyatenda.
وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَنُدْخِلَنَّهُمْ فِي الصَّالِحِينَ
Na walio amini na wakatenda mema, bila ya shaka tutawaingiza katika (watu) wema.
Katika zama za mwanzoni mwa Uislamu, baadhi ya vijana walisilimu, wakamwamini Bwana Mtume Muhammad SAW na kuachana na ibada potofu ya kuabudu masanamu. Lakini baba na mama wa vijana hao walikuwa washirikina na waabudu masanamu; hivyo wakawataka watoto wao hao waiache dini ya haki aliyokuja nayo Bwana Mtume. Hata baadhi ya akina mama wakaamua kususia kula ili kuzivuta na kuziathiri hisia za nyoyo za watoto wao; lakini pamoja na yote hayo hawakufanikiwa kuwatoa watoto wao katika dini ya haki ya Uislamu.
Aya hizi tulizosoma zinawahutubu vijana hao na watu wote wanaoishi kwenye koo na familia za ukafiri na shirki kwamba: wakati mafungamano ya damu na kifamilia yanapogongana na mafungamano ya kiimani na kidini, kulinda imani ya dini ni muhimu zaidi kuliko kutafuta ridhaa ya wazazi wawili; wala haifai mtu kuacha dini na imani yake kwa sababu ya hisia za huruma na upendo. Tab'an ni jambo la lazima mtu kuhakikisha daima anachunga na kulinda heshima ya wazazi wake wawili na kujitahidi kuwasaidia kadiri ya uwezo wake na kutofanya ajizi katika kukidhi mahitaji yao.
Kisha aya zinaendelea kwa kuwahutubu watu wote wa familia, wawe wazazi au watoto wao kwa kuwaambia: matendo na amali zenu zote mnazofanya duniani zinahifadhiwa na iko siku mtalazimika kuwajibika kwa amali zenu; na watu pekee watakaokuwa pamoja na waja wema na watoharifu Siku ya Kiyama ni wale waliokuwa waumini na wakafanya amali njema. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kuwafanyia wema na hisani wazazi ni suala la kiutu mutlaki na lisilo na mjadala. Wawe ni Waislamu au makafiri, inapasa kuwaheshimu na kuwahudumia wazazi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kuwalingania watu wafuate shirki, kwa hakika ni kuwaita kwenye jambo la kijahili na lisilo na hoja; kwa sababu shirki haina mashiko wala msingi wowote wa kiakili na kielimu. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba inapasa watoto wawe huru katika kuchagua njia sahihi ya kufuata. Baba na mama hawawezi kuwalazimisha watoto wao wafuate njia waliyofuata wao.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 10 na 11 ambazo zinasema:
وَمِنَ النَّاسِ مَن يَقُولُ آمَنَّا بِاللَّهِ فَإِذَا أُوذِيَ فِي اللَّهِ جَعَلَ فِتْنَةَ النَّاسِ كَعَذَابِ اللَّهِ وَلَئِن جَاءَ نَصْرٌ مِّن رَّبِّكَ لَيَقُولُنَّ إِنَّا كُنَّا مَعَكُمْ أَوَلَيْسَ اللَّهُ بِأَعْلَمَ بِمَا فِي صُدُورِ الْعَالَمِينَ
Na katika watu kuna wanao sema: Tumemuamini Mwenyezi Mungu. Lakini wanapo udhiwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, wanayafanya mateso ya watu kama ni adhabu ya Mwenyezi Mungu. Na inapo kuja nusura kutoka kwa Mola wako Mlezi husema: Hakika sisi tulikuwa pamoja nanyi. Kwani Mwenyezi Mungu hayajui yaliomo vifuani mwa walimwengu?
وَلَيَعْلَمَنَّ اللَّهُ الَّذِينَ آمَنُوا وَلَيَعْلَمَنَّ الْمُنَافِقِينَ
Na kwa yakini Mwenyezi Mungu atawatambulisha walio amini, na kwa yakini atawatambulisha wanafiki.
Aya hizi zinaendeleza maudhui ya aya zilizotangulia kwa kuashiria kundi jengine la Waislamu ambao huwa waumini wanapokuwa katika raha, ustawi na uneemevu wa kimaisha. Lakini inapobidi, na ikawalazimu kulinda imani zao kwa kukabiliana na tabu na misukosuko, hutoka nje ya mstari wa imani na wakawaacha mkono pia Waislamu wenzao. Amma wakati misukosuko na matatizo hayo yanapoondoka, na waumini wakapata tena nguvu na uwezo, watu hao hujionesha kuwa wako pamoja nao kwa kuwaambia: sisi tumekuwa kando yenu na pamoja nanyi kila mahala, kwa hivyo ni washirika pia katika ushindi wenu huu. Aya zinaendelea kusema: Mwenyezi Mungu SW ni mjuzi wa batini za wanadamu wote na anajua ni nani walio tayari hata kuhatarisha maisha yao kwa ajili ya kulinda imani zao, na nani ambao kwa sababu ya tabu na msukosuko mdogo tu huwa tayari kupoteza imani zao. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba imani za baadhi ya watu ni za mdomoni tu si za moyoni! Kwa hivyo tusimwamini kila muumini wa kujinadi tu, kwa sababu imani ya kweli inadhihiri na kuthibiti pale watu wanapotingwa na tabu na misukosuko. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa baadhi ya wakati kusilimu na kuiamini haki pamoja na kulinda mtu imani yake huwa kuna gharama zake ambazo waumini waliokhitari kufuata njia ya haki inawabidi waikubali na kuihimili. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba wanafiki ni watu mabarakala. Wakati wa shida na hatari hukimbia na kujiweka mbali, na wakati wa raha na ushindi hujitia kimbelembele kwa kuonesha wako pamoja na waumini ili na wao wanufaike na matunda na mafanikio yaliyopatikana.
Darsa ya 704 ya Qur'ani inahatimishwa na aya ya 12 na 13 ambazo zinasema:
وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لِلَّذِينَ آمَنُوا اتَّبِعُوا سَبِيلَنَا وَلْنَحْمِلْ خَطَايَاكُمْ وَمَا هُم بِحَامِلِينَ مِنْ خَطَايَاهُم مِّن شَيْءٍ إِنَّهُمْ لَكَاذِبُونَ
Na walio kufuru waliwaambia walio amini: Fuateni njia yetu, nasi tutayabeba makosa yenu. Wala wao hawatabeba katika makosa yao chochote kile. Hakika hao ni waongo.
وَلَيَحْمِلُنَّ أَثْقَالَهُمْ وَأَثْقَالا مَّعَ أَثْقَالِهِمْ وَلَيُسْأَلُنَّ يَوْمَ الْقِيَامَةِ عَمَّا كَانُوا يَفْتَرُونَ
Na kwa hakika wataibeba mizigo yao na mizigo mingine pamoja na mizigo yao. Na kwa hakika wataulizwa Siku ya Kiyama juu ya waliyo kuwa wakiyazua.
Washirikina wa Makka walikuwa wakifanya kila njia ili kuwatoa waumini katika Uislamu na kuwarejesha kwenye shirki na ukafiri. Aya tulizosoma zinasema: watu hao walikuwa wakiwaambia wale walioamini: rudini kwenye njia yetu na njia ya wazee wetu waliotangulia, na iacheni hiyo njia ya Muhammad. Ikiwa haya tuyafanyayo si makosa wala si dhambi, hakutokuwa na dhara yoyote kwetu sisi na kwenu nyinyi; na kama yatakuwa ni kosa na dhambi, sisi tunabeba dhima ya madhambi yenu; na nyinyi hamtokuwa na kosa lolote. Aya zinaendelea kwa kuwajibu watu hao kwa kusema: wao wanasema uongo kwa hayo wanayodai, kwa sababu mtoaji malipo ya adhabu na thawabu ni Mwenyezi Mungu, sio wao. Wao hawana uwezo wa kumwondolea adhabu aliyetenda madhambi na kumfanya asamehewe. Na bila ya shaka, kama mtu atapotoka kwa kufuata maneno hayo potofu na akatoka kwenye njia ya imani, ataadhibiwa Siku ya Kiyama. Na yule mshirikina aliyempotosha, mbali na kubeba mzigo wa dhambi zake mwenyewe, atabeba pia dhambi za mtu aliyempotosha. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba maadui hawakomi katu kuwaandama waumini. Kuna wakati huwaandama kwa maudhi na mateso, na wakati mwengine kwa ahadi hewa na za uongo ili kutaka kuwarejesha kwenye njia ya kufru na shirki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa katika mtazamo wa Kiislamu juu ya ulimwengu, hakuna mtu awezaye kubeba mzigo wa dhambi za mtu mwengine, au kudai kwa kumwambia mimi nabeba dhima ya madhambi yako! Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba mtu anayewapoteza watu wengine anakuwa mshirika katika madhambi yao na anabeba mas-ulia pia ya madhambi ya watu wengine watakaopotoka kupitia yeye. Tab'an hilo halipunguzi kitu katika dhambi za mtu mwenyewe aliyekubali kupotezwa. Wapenzi wasikilizaji, darsa yetu ya leo imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuoneshe haki na atupe taufiki ya kuifuata, na atuoneshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/