Jan 16, 2017 09:59 UTC

Sura ya Al-A'nkabut, aya ya 19-23 (Darsa ya 706)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 706, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 29 ya Al-A'nkabut. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 19 na ya 20 ambazo zinasema:

أَوَلَمْ يَرَوْا كَيْفَ يُبْدِئُ اللَّهُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ إِنَّ ذَلِكَ عَلَى اللَّهِ يَسِيرٌ

Je! Wao hawaoni jinsi Mwenyezi Mungu anavyo anzisha uumbaji, na kisha akarudisha tena. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi.

قُلْ سِيرُوا فِي الأَرْضِ فَانظُرُوا كَيْفَ بَدَأَ الْخَلْقَ ثُمَّ اللَّهُ يُنشِئُ النَّشْأَةَ الآخِرَةَ إِنَّ اللَّهَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

Sema: Tembeeni katika ardhi na tazameni jinsi alivyo anzisha uumbaji; kisha Mwenyezi Mungu ndiye anaye umba umbo la baadaye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza juu ya kila kitu.

Darsa yetu iliyopita iliishia katika kunukuu mazungumzo ya Nabii Ibrahim (AS) na washirikina wa kaumu yake, ambapo Mtume huyo wa Allah aliwakataza watu hao kuyaabudu masanamu na kuomba riziki yao kwa masanamu hayo. Aya hizi tulizosoma na nyengine kadhaa zinazofuatia ambazo zimekuja katikati ya mazungumzo hayo zinajenga hoja ya kuthibitisha ma'adi  na kuwepo ulimwengu wa akhera, yaani kile ambacho hasa washirikina, wawe wa zama za Nabii Ibrahim au wa zama za Bwana Mtume Muhammad SAW, walikuwa hawakikubali na kuhisi ni jambo lisilowezekana. Aya tulizosoma zinawataka washirikina kutumia akili zao na kutafakari ili waweze kumaizi na kuelewa kwamba kuwaumba viumbe mara ya pili ni kazi rahisi na inayowezekana kwa Mungu aliyeviumba viumbe hivyo mara ya kwanza. Aidha aya zinawataka watu hao waangalie viumbe vingine vilivyowazunguka katika mazingira ya ulimwengu huu wenye adhama ili wabaini pia kwamba Muumba wa ulimwengu huu ni muweza wa kila jambo, kwa hivyo si kazi ngumu na isiyoyumkinika kwake Yeye kuwaumba tena wanadamu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Qur'ani kila mara huwa inawaita na kuwatolea mwito watu watafakari ili kuweza kuelewa hakika za ulimwengu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa uumbaji ni dhihirisho la elimu na uwezo usio na kikomo wa Allah SW katika uhuishaji na ufishaji wa viumbe. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba katika Uislamu umeusiwa na kutiliwa mkazo utalii wenye malengo na wa kufanya utafiti katika ulimwengu wa maumbile ili kujua ukweli na hakika za mambo. Tutaweza kumjua vizuri zaidi Mwenyezi Mungu kwa kuyatalii na kuyachunguza maumbile kwa makini. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa hoja madhubuti zaidi ya kuthibitisha uwezekano wa kuwepo ma'adi na ufufuo, ni uwezo alioonesha Allah SW katika kuviumba viumbe mara ya kwanza.

Zifuatazo sasa ni aya za 21 na 22 za sura yetu ya A'nkabut ambazo zinasema:

يُعَذِّبُ مَن يَشَاء وَيَرْحَمُ مَن يَشَاء وَإِلَيْهِ تُقْلَبُونَ

Humuadhibu amtakaye, na humrehemu amtakaye. Na kwake Yeye mtapelekwa.

وَمَا أَنتُم بِمُعْجِزِينَ فِي الأَرْضِ وَلا فِي السَّمَاء وَمَا لَكُم مِّن دُونِ اللَّهِ مِن وَلِيٍّ وَلا نَصِيرٍ

Wala nyinyi si wenye kushinda ardhini wala mbinguni. Wala nyinyi hamna mlinzi wala msaidizi isipo kuwa Mwenyezi Mungu.

Aya hizi zinaendeleza maudhui ya aya zilizotangulia kuelezea uwezo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu wa kuwafufua na kuwahuisha tena wanadamu baada ya kufa na kubainisha kwamba: kinyume na ilivyo dunia ambayo ni pahala pa kupanda na kulima, akhera ni pahala pa mavuno na malipo ya aliyoyafanya mtu duniani. Kile mlichokipanda katika shamba la dunia, mazao yake ndiyo mtakayokwenda kuyavuna akhera. Hakimu wa Siku ya Kiyama ni Mwenyezi Mungu, Mola aliye na uelewa na ujuzi kamili wa yote mliyoyatenda duniani; na kwa hivyo atakulipeni malipo ya thawabu au iqabu kulingana na matendo yenu hayo; na au kwa wale atakaoona wanastahiki atawaafu na kuwarehemu.

Mtu yeyote asidhani kwamba anaweza katika dunia au akhera kutoka nje ya mamlaka ya utawala wa Allah SW na kukimbia na kukwepa nguvu na qudra yake mbinguni au ardhini. Kokote kule mtakokwenda mtakuwa chini ya mamlaka na utawala wake na ni jambo lisilo na maana yoyote kufikiria kukwepa na kuyakimbia mamlaka ya Allah. Msifikiri kwamba ardhi tu ndiyo iko chini ya utawala wake, hivyo kama mtaelekea kwenye kilele cha mbingu mtaweza kutoka nje ya mamlaka ya utawala wake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba huruma na ghadhabu za Allah zinaambatana pamoja ili waja wema wawe na matumaini ya kupata rehma zake na watenda maovu wahofu na kujihadhari na adhabu yake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kwa kuzingatia aya zingine za Qur'ani irada na muamala wa Allah SW kwa waja wake unafuata msingi wa uadilifu na hekima, na Yeye Mola hamdhulumu hata chembe mja wake yeyote yule. Aidha aya hizi zinatutaka tujue kwamba irada na matakwa ya mwanadamu hayawezi katu kuyashinda matakwa na irada ya Allah japokuwa mwanadamu amepiga hatua kubwa kinguvu na kiuwezo na kuwa na nyenzo na suhula za kisasa kabisa.

 Darsa ya 706 ya Qur'ani inahatimishwa na aya ya 23 ambayo inasema:

وَالَّذِينَ كَفَرُوا بِآيَاتِ اللَّهِ وَلِقَائِهِ أُوْلَئِكَ يَئِسُوا مِن رَّحْمَتِي وَأُولَئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ

Na walio zikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu na kukutana naye, hao ndio wenye kukata tamaa na rehema yangu, na hao ndio wenye kupata adhabu chungu.

Katika aya zilizotangulia, Qur'ani tukufu imeeleza kuwa Siku ya Kiyama kundi moja la watu litaghadhibikiwa na kuadhibiwa na Allah na kundi jengine litahurumiwa na kurehemewa. Aya hii tuliyosoma inazungumzia watu wasio na matumaini na waliokata tamaa ya kusamehewa na kupata rehma za Allah na kueleza kwamba kila mtu anayezipuuza ishara za Mwenyezi Mungu katika mfumo wa ulimwengu wa uumbaji au akazikadhibisha na kuzikanusha aya za Qur'ani kwa msingi wa kufuru na inadi, awe na yakini kwamba atapata adhabu kali Siku ya Kiyama na wala hakuna tumaini lolote la yeye kusamehewa. Kwa sababu ameikufuru asili ya ulimwengu wa uumbaji na vilevile ameikufuru Siku ya Kiyama na ma'adi. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba rehma za Mwenyezi Mungu ni enevu na nyingi mno, na kila mtu anaweza kufaidika nazo kwa kadiri ya uwezo wake, lakini kufru na ukanushaji unamfungia njia mtu ya kufaidika na rehma za Allah. Kama ambavyo mpira uliozibwa pande zote unapowekwa kwenye bahari kuu huwa hauruhusu hata tone moja la maji kupenya na kuingia ndani yake, ndivyo vivyo hivyo ukafiri na ukanushaji haki unavyomzuia mtu kuzifikia rehma za Mwenyezi Mungu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa makafiri tu ndio watu wanaokosa na wanaokata tamaa ya kufaidika na rehma zisizo na kikomo wala mpaka za Allah SW. Wapenzi wasikilizaji, darsa yetu ya leo ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa miongoni mwa waja wake wasiokata tamaa ya kupata rehma zake na wenye kufaidika na rehema zake zisizo na ukomo. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/