Jan 16, 2017 10:14 UTC

Sura ya Al-A'nkabut, aya ya 27-30 (Darsa ya 708)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 708, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 29 ya Al-A'nkabut. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 27 ambayo inasema:

وَوَهَبْنَا لَهُ إِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ وَجَعَلْنَا فِي ذُرِّيَّتِهِ النُّبُوَّةَ وَالْكِتَابَ وَآتَيْنَاهُ أَجْرَهُ فِي الدُّنْيَا وَإِنَّهُ فِي الآخِرَةِ لَمِنَ الصَّالِحِينَ

Na tulimtunukia (Ibrahim) Is-haq na Yaa'qub. Na tukajaalia katika kizazi chake Unabii na Kitabu, na tukampa ujira wake katika dunia; naye hakika katika Akhera bila ya shaka ni katika watu wema.

Katika aya zilizopita tulizungumzia kwa muhtasari kuhusu matukio yaliyojiri katika maisha ya Nabii Ibrahim (as). Aya tuliyosoma inahatimisha mazungumzo yanayohusu maudhui hiyo kwa kusema: baada ya Nabii Ibrahim kuhajiri na kuondoka katika ardhi ya kwao ili kwenda kuwalingania watu wengine wito wa haki, Mwenyezi Mungu alimtunukia hiba na hidaya kubwa. Ni ya watoto na kizazi safi na teule cha kuendeleza njia yake; na kwa ukarimu wake Mola watoto hao wakafikia daraja ya Utume na kuwa taa ya kumurika katika njia ya imani kwa watu wa kaumu zao. Waja wateule kama Is-haq na mwanawe Yaaqub, mwana wa Yaaqub, yaani Yusuf na vilevile Musa, Haruna na Suleiman (as), wote walitokana na kizazi cha Nabii Ibrahim (as) na wote hao walipewa jukumu la kufikisha ujumbe wa Allah SW.

Hiba hiyo aliyopewa Nabii Ibrahim ni ya duniani na akhera pia. Ni ya kubakisha jina jema na  kupata malipo mema kwa Allah, kwa sababu mtoto mwema ni kitu cha kujivunia kwa mzazi wakati wa uhai wake na huwa sababu ya kutajwa kwa wema baada ya kufa kwake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba mtoto mwema ni hiba na hidaya ya Allah ambayo huwatunukia waja wema na wateule. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa moja ya malipo mema ya Mola kwa mja duniani ni kumjaalia kuwa na kizazi chema na safi. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba kinyume na mitazamo potofu, dunia na akhera zinaweza kujumuishwa pamoja. Katika utamaduni wa Kiislamu hatakiwi mtu kuitoa mhanga na kuiuza akhera yake kwa ajili ya dunia na haimpasi yeye pia kujitenga na dunia kwa sababu ya kuifikia akhera.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 28 na 29 ambazo zinasema:

وَلُوطًا إِذْ قَالَ لِقَوْمِهِ إِنَّكُمْ لَتَأْتُونَ الْفَاحِشَةَ مَا سَبَقَكُم بِهَا مِنْ أَحَدٍ مِّنَ الْعَالَمِينَ

Na Lut'i alipo waambia watu wake: Hakika nyinyi mnafanya uchafu, ambao hajakutangulieni yeyote kwa hilo katika walimwengu.

أَئِنَّكُمْ لَتَأْتُونَ الرِّجَالَ وَتَقْطَعُونَ السَّبِيلَ وَتَأْتُونَ فِي نَادِيكُمُ الْمُنكَرَ فَمَا كَانَ جَوَابَ قَوْمِهِ إِلاَّ أَن قَالُوا ائْتِنَا بِعَذَابِ اللَّهِ إِن كُنتَ مِنَ الصَّادِقِينَ

Je! Nyinyi mnawaingilia wanaume, na mnaikata njia? Na katika mikusanyiko yenu mnafanya maovu? Basi haikuwa jawabu ya watu wake isipo kuwa kusema: Tuletee hiyo adhabu ya Mwenyezi Mungu ikiwa wewe ni katika wakweli.

Baada ya Nabii Ibrahim (as), aya tulizosoma zimeashiria kwa muhtasari habari za Lut (as) ambaye naye pia alikuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu. Nabii Lut aliishi katika zama moja na Nabii Ibrahim, na alikuwa mubalighi na mfikishaji wito wa dini ya Nabii Ibrahim kwa watu wa kaumu yake. Lakini watu wake sio tu hawakuukubali wito wake bali waliamua kumbaidisha na kumtishia kumuua Mtume wao huyo kwa sababu ya kuwakataza kufanya vitendo vichafu. Aya hizi zimeashiria moja ya vitendo vichafu zaidi kufanywa na wanadamu ambavyo mfano wake havijawahi kushuhudiwa hata kwa wanyama na kueleza kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu Lut (as) alikuwa kila mara akiwaasa na kuwakumbusha watu wa kaumu yake kwamba kuingiliana kimwili wanaume kwa wanaume ni kitendo kiovu mno kwani huwafanya wanaume wasishughulishwe na wanawake na husababisha kutoweka kizazi cha wanadamu. Kitendo hicho pia ni kinyume na utaratibu wa kawaida wa maumbile ambapo hamu na matamanio ya kijinsia katika viumbe huwa ni baina ya dume na jike na ndiyo maana hata wanyama ambao hufanya mambo kulingana na ghariza za kimaumbile tu hawafanyi tendo ovu na chafu kama hilo. Watu wa kaumu ya Nabii Lut  sio tu walikuwa wakifanya amali hiyo chafu lakini staha na haya ya kijamii pia ilikuwa imewatoka kwa kiwango ambacho kinyume na watu wengine wanaofanya maasi hayo kwa kujificha, na mbali na macho ya watu, wao walikuwa wakifanya uchafu wao wa liwati kwenye maeneo ya hadhara huku wakiangaliana wenyewe kwa wenyewe. Kwa mtazamo wao, kitendo hicho kilikuwa aina fulani ya starehe na burudani. Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba watu hao sio tu hawakuyajali mawaidha na maonyo waliyopewa na Nabii Lut na kujirekebisha mwenendo wao mwovu lakini pia walimwambia Mtume wao huyo kwa kejeli na stihzai kwamba: kama Mungu wako anakerwa na haya tunayoyafanya na amepanga kutuadhibu, mwambie basi aiteremshe hiyo adhabu papa hapa duniani ituangamize. Kwa maneno mengine, walitaka kumwambia Nabii Lut kwamba wewe ni mwongo katika madai yako kuwa ni Mtume kwa hiyo usitusumbue sisi na mambo yetu tunayofanya. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba jukumu la viongozi wa dini si kuwalingania tu watu wito wa Allah, bali wanapaswa kupambana na maovu na kujitahidi kuisafisha jamii na mambo machafu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa hata kama ufisadi utazagaa katika jamii hatuwezi kusema, kukataza maovu hakuna taathira yoyote tena kwa hiyo hakuna haja ya kujisumbua. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba Mitume wa Allah wanawashajiisha watu kukidhi ghariza na matamanio ya kijinsia kwa njia sahihi; na kinyume chake wanasimama kukabiliana na upotofu wa kijinsia, maingiliano holela ya kimwili na ya watu wa jinsia moja. Vilevile aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba wakati dhambi inapokuwa haijaenea na ikawa haifanywi hadharani katika jamii inabaki kuwa suala la mtu binafsi, lakini wakati inapovuka mpaka wa staha na heshima ya jamii inakuwa ovu la kijamii na huwa lazima kukabiliana nalo. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba maingiliano ya kimwili ya watu wa jinsia moja, ambayo leo hii yanajuzishwa na kuhalalishwa katika baadhi ya nchi za Magharibi yametajwa kuwa ni tendo ovu na chafu katika dini zote za mbinguni; na Mitume wameamrishwa kupambana nayo.

Darsa ya 708 ya Qur'ani inahatimishwa na aya ya 30 ambayo inasema:

قَالَ رَبِّ انصُرْنِي عَلَى الْقَوْمِ الْمُفْسِدِينَ

 Akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Ninusuru na watu hawa mafisadi! 

Wakati watu wafanya madhambi wa kaumu ile walipomtuhumu Nabii Lut (as) kuwa muongo na kuutilia shaka Utume wake, mtukufu huyo alimuelekea Mwenyezi Mungu na kumwomba aonyeshe muujiza wake kuthibitisha ukweli wa madai ya Utume wa Nabii wake. Muujiza ambao utakuwa ishara ya kuthibitisha ukweli wa ujumbe wake na vilevile utakuwa adhabu kwa waovu na ushindi wa haki dhidi ya batili. Wale ambao wanaona fakhari kufanya madhambi na kuuona utakasifu na usafi wa nafsi ni kitu kiovu ni watu waliofisidika ambao wamekithirisha na kueneza madhambi na maovu na kutaka yaonekane kitu cha kawaida katika jamii. Watu hao wamekengeuka njia sahihi kwa kiasi ambacho kama watu safi na wachamungu watawakumbusha na kuwaasa huwafanyia inda, kejeli na istihzai. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba katika utamaduni wa Kiislamu maingiliano ya kimwili ya watu wa jinsia moja yanahesabiwa kuwa ni uenezaji uharibifu katika ardhi, na mtu anayefanya dhambi na ovu hilo hadharani huhukumiwa adhabu kali. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa tunapoona uharibifu na uovu unaenezwa katika jamii tunatakiwa tukabiliane nao kwa nguvu zote na vilevile tuombe msaada wa Mwenyezi Mungu ili kuweza kuwashinda watu mafisadi na waharibifu.

Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 708 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Mola atuwezeshe kuondoa maovu katika jamii zetu kwa mikono yetu na ndimi zetu au kwa uchache kabisa kuchukia ndani ya nyoyo zetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/