Jan 16, 2017 11:14 UTC

Sura ya Al-A'nkabut, aya ya 36-40 (Darsa ya 710)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 710, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 29 ya Al-A'nkabut. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 36 na 37 ambazo zinasema:

وَإِلَى مَدْيَنَ أَخَاهُمْ شُعَيْبًا فَقَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّهَ وَارْجُوا الْيَوْمَ الآخِرَ وَلا تَعْثَوْا فِي الأَرْضِ مُفْسِدِينَ

Na kwa Madyana tulimtuma ndugu yao Shuaibu, naye akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu na itarajieni Siku ya Akhera, wala msende katika ardhi mkifisidi.

فَكَذَّبُوهُ فَأَخَذَتْهُمُ الرَّجْفَةُ فَأَصْبَحُوا فِي دَارِهِمْ جَاثِمِينَ

Lakini walimkadhibisha, basi ukawanyakua mtetemeko wa ardhi, wakapambazukiwa ndani ya nyumba zao nao wamefudikia.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizosimulia yaliyowafika watu wa kaumu ya Nabii Lut (as). Aya tulizosoma zinaashiria wito na ujumbe wa Nabii Shuaib (as) kwa watu wa kaumu yake wa mji wa Madyan na kueleza kwamba: Mtume huyo pia kama walivyokuwa Mitume wengine wote aliwafikishia watu wake wito wa tauhidi na ma'adi, yaani kumwabudu Mungu mmoja tu wa haki na kuamini Kiyama na akhera na akawaambia: madhambi na kumwasi Mwenyezi Mungu kunasababisha ufisadi na uharibifu katika ardhi na kuufanya mfumo wa jamii uwe wa dhulma na wenye utovu wa uadilifu. Lakini kwa masikitiko, kaumu ya Nabii Shuaib pia kama zilivyokuwa kaumu nyengine nyingi zilizotangulia iliukadhibisha na kuupinga Utume wa Nabii huyo. Watu hao waliyapuuza mawaidha na miongozo waliyopewa kiudugu na mtu aliyekuwa na uchungu nao, ambayo yalikuwa na madhumuni ya kuirekebisha jamii ya kaumu hiyo. Qur'ani inasema: mwisho na hatima ya ukadhibishaji na ufanyaji madhambi na maasi watu hao ilikuwa ni kufikwa na adhabu ya Allah papa hapa duniani kwa ardhi yao kukumbwa na tetemeko lililowaangamiza watu hao wote.

Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba tauhidi na maadi, yaani kufufuliwa, ndio ujumbe mkuu wa wito wa Mitume. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa muamala wa Mitume kwa watu wao ulikuwa wa kidugu na kirafiki; si wa namna ya kujikweza na kujiona wako juu  zaidi ya watu wao. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kufanya madhambi tu peke yake hakusababishi kuteremkiwa na adhabu. Kukithirisha na kushupalia kuyafanya madhambi kwa uelewa na kwa nia ya kuifanyia inadi na upinzani haki, ndio husababisha kufikwa na adhabu ya Mwenyezi Mungu.

Ifuatayo sasa ni aya ya 38 ambayo inasema:

وَعَادًا وَثَمُودَ وَقَد تَّبَيَّنَ لَكُم مِّن مَّسَاكِنِهِمْ وَزَيَّنَ لَهُمُ الشَّيْطَانُ أَعْمَالَهُمْ فَصَدَّهُمْ عَنِ السَّبِيلِ وَكَانُوا مُسْتَبْصِرِينَ

Na pia kina A'di na Thamud. Nanyi yamekwisha kubainikieni kutokana na maskani zao. Na Shet'ani aliwapambia vitendo vyao, na akawazuilia Njia, na hali walikuwa wenye kuona.

Aya hii imeashiria hatima ya kaumu za A'ad na Thamud ambazo Mitume wao Hud na Saleh (AS) walipewa jukumu la kuwafikishia watu hao wito wa uongofu. Watu wa kaumu hizi mbili ambao habari zao zimesimuliwa pia katika aya nyengine za Qur'ani waliwakadhibisha Mitume wao hao na wakasimama kuyapinga kwa uelewa kamili maamrisho ya Allah waliyofikishiwa na Manabii Hud na Saleh (as). Qur'ani tukufu inawahutubu watu wa Makka kwamba: watu wa kaumu hizo mbili nao pia walifikwa na adhabu ya Allah; na magofu ya miji yao yaliyoko kusini na kaskazini ya Makka katika njia za kuelekea Yemen na Sham yanaonekana waziwazi mbele yenu na mnayaona mnapopita katika safari zenu lakini hamupati ibra wala mazingatio yoyote.

Kisha aya zinaendelea kwa kueleza kwamba sababu ya watu hao kufikwa na adhabu hiyo ni kumfuata shetani ambaye aliwahadaa kwa mapambo ya kidunia. Pamoja na kwamba walijaaliwa kuwa na nyenzo zote za kuwawezesha kuitambua haki ikiwa ni pamoja na akili, fitra ya ndani ya nafsi na wito wa Mitume lakini walikengeuka njia ya haki na kufuata upotofu.

Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba athari za kihistoria za kaumu zilizopita, ambazo zinaweza kuwa sababu ya kupata ibra na funzo vizazi vinavyofuata zinapasa kutunzwa na kuhifadhiwa. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kazi inayofanywa na shetani ni kuyapamba maovu yaonekane mazuri. Kile ambacho mwanadamu, kutokana na akili na maumbile yake, anakiona ni kiovu na kibaya, shetani hukifanya kionekane kizuri na cha kupendeza. Kwa mfano kujitukuza, kujiona, kujifaharisha na kujivuna kwa utajiri na madaraka ni miongoni mwa mambo ambayo shetani huyafanya yaonekane mazuri mbele ya macho ya mtu.

Darsa yetu ya leo ya Qur'ani inahatimishwa na aya ya 39 na 40 ambazo zinasema:

وَقَارُونَ وَفِرْعَوْنَ وَهَامَانَ وَلَقَدْ جَاءَهُم مُّوسَى بِالْبَيِّنَاتِ فَاسْتَكْبَرُوا فِي الأَرْضِ وَمَا كَانُوا سَابِقِينَ

Na pia Qaruni na Firauni na Hamana! Na Musa aliwajia kwa Ishara waziwazi, lakini walifanya kiburi katika nchi, wala hawakuweza kushinda.

فَكُلا أَخَذْنَا بِذَنبِهِ فَمِنْهُم مَّنْ أَرْسَلْنَا عَلَيْهِ حَاصِبًا وَمِنْهُم مَّنْ أَخَذَتْهُ الصَّيْحَةُ وَمِنْهُم مَّنْ خَسَفْنَا بِهِ الأَرْضَ وَمِنْهُم مَّنْ أَغْرَقْنَا وَمَا كَانَ اللَّهُ لِيَظْلِمَهُمْ وَلَكِن كَانُوا أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ

Basi kila mmoja tulimtesa kwa mujibu wa makosa yake. Miongoni mwao wapo tulio wapelekea kimbunga cha changarawe; na miongoni mwao wapo walio nyakuliwa na ukelele; na miongoni mwao wapo tulio wadidimiza katika ardhi; na miongoni mwao wapo tulio wagharikisha. Wala Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuwadhulumu, lakini walikuwa wenyewe wakijidhulumu nafsi zao. 

Baada ya kueleza hatima na mwisho wa baadhi ya kaumu zilizopita, aya tulizosoma zinaashiria hatima ya baadhi ya watu waliotakabari na majabari wakubwa katika historia kama Firauni, Qarun na Haman. Qarun aliingiwa na ghururi na kiburi kwa sababu ya mali na utajiri mkubwa aliojaaliwa. Utawala na madaraka vilimfikisha Firauni kwenye kilele cha uovu na uasi. Naye Haman alikuwa waziri wa taghuti huyo na mshirika wake katika jinai na maovu aliyoyafanya.

Nabii Musa (as) aliwafikishia mwongozo wa haki na mawaidha watatu hao na akatimiza kikamilifu dhima aliyokuwa nayo kwao. Lakini wao hawakuikubali haki bali waliendelea kushikilia njia na mwenendo wao potofu. Walisimama kumpinga Mtume mkubwa wa Allah, Musa (as) na hata wakafika hadi ya kutaka kumuua. Watu hao waovu na mafasiki walidhani kwamba wataweza kukabiliana na irada ya Mwenyezi Mungu SW. Lakini kwa irada yake Mola ardhi ilimzamisha Qarun, ikamzika yeye na utajiri wake wote; na maji ya Mto Nile yakawagharikisha na kuwaangamiza Firauni na waziri wake Haman.

Kisha aya zinaendelea kwa kuashiria aina tofauti za adhabu za hapa duniani zilizowafika watu wa kaumu mbalimbali, ambazo zimezungumziwa kwa ufafanuzi katika aya nyengine za Qur'ani. Kaumu ya A'ad ilikumbwa na tufani ya mchanga na kokoto iliyowamiminikia mtawalia watu hao kutwa kucha kwa muda wa siku saba na kuwaangamiza. Kaumu ya Thamud iliangamizwa kwa ukelele wa maangamizi na zilzala; na kuna wale waliozamishwa ardhini na waliogharikishwa majini. Zote hizo zilikuwa adhabu za hapa duniani zilizowafika watu hao.

Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba mwisho wa kutakabari na kujikweza ni hilaki na maangamizi. Madaraka, utajiri na vitu vinginevyo haviwezi kumuokoa mtu mwovu na maangamizi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa Allah SW ndiye nguvu kubwa kabisa kuliko nguvu zote; na wale wanaoamua kukabiliana na dini ya haki na wafuasi wa njia ya haki wasidhani kama wataweza kusimama kukabiliana na Allah SW. Aya hizi aidha zinatutaka tuelewe kwamba adhabu ya Mwenyezi Mungu si ya namna moja; bali Yeye Mola ni mwenye anuai za adhabu. Kwa hivyo anaweza kuwaadhibu watenda maovu kwa namna yoyote ile ya adhabu aitakayo. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba hatima na majaaliwa ya kila mtu yamefungamana na amali na matendo yake mwenyewe. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 710 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuepushe na adhabu yake ya hapa duniani, na atulinde na adhabu yake ya huko akhera na atujaalie kuwa miongoni wa waja wake wema. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/