Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (151)
Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Hii ni sehemu ya 151 katika mfululizo wa vipindi hivi vya itikadi ya Kiislamu vinavyokujieni chini ya anwani ya Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain.
Bado tungali tunajadili suala la Uimamu ambalo ni katika misingi mitano ya dini tukufu ya Kiislamu ambapo leo tutazungumzia wajibu tulionao sisi Waislamu kwa maimamu watoharifu wa Nyumba ya Mtukufu Mtume (saw). Mwanzoni mwa vipindi saba vilivyopita tuliuliza swali ambalo hadi sasa limetuwezesha kujua wajibu saba kati ya wajibu hizo ambazo ni: Wajibu wa utiifu wa moja kwa moja kwao na kufuata mienendo yao ya Maisha kwa sababu wao (as) ndio Quráni inayozungumza na dhihirisho la Sunna za Bwana Mtume (saw). Kisha kuna wajibu wa kuwashtakia hitilafu na ugomvi unaozuka miongoni mwetu ili wapate kutuhukumu kwa njia sahihi na ya sawa kwa mujibu wa mafundisho ya Quráni Tukufu na suna za Bwana Mtume (saw). Tunapasa pia kuwarejea kuhusiana na matukio yanayozuka katika zama zetu ili tupate kujua miongozo sahihi ya matukio hayo kwa sababu wao ndio walio na elimu sahihi na kamilifu kuhusiana na Quráni Tukufu ambayo inayobainisha kila jambo. Wajibu wa tatu ni kuwaswalia kwa njia sahihi na kujiepusha kuwaswalia swala ya mkato kwa sababu hilo hilo ni jambo lililokatazwa na Mtume Mtukufu (saw). Wajibu wa nne ni kuwapenda kama kinavyotuamrisha Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Wa tano ni kuwatukuza na kuwaadhimisha kutokana na nafasi yao adhimu na ya juu waliyonayo mbele ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake Mtukufu (saw) na vilevile kutokana na huduma yao muhimu kwa waja wa Mwenyezi Mungu. Wajibu wa sita ni kuwabai na kulinda baia hiyo na kuijadidisha kwa Imam aliye hai kati yao. Wajibu wa saba ni kuwazuru wakati wa uhai na baada ya wao kuaga dunia.
Baada ya kujua wajibu hizo wajibu wa nane ni upi? Hili ndilo swali tutakalolijadili katika kipidi chetu cha leo hivyo endeleeni kuwa pamoja nasi hadi mwisho wa kipindi, karibuni.
Maandiko matakatifu yanatufahamisha kwamba kutoa khumsi ya kisheria ni miongoni mwa haki ambazo Mwenyezi Mungu ameziwajibisha kutoka kwenye mali za Waislamu ili wapate kuitoa kwa ajili ya Ahlul Beit wa Mtume (saw). Na haki hii inazungumziwa kwa uwazi na aya ya 41 ya Surat an-Anfaal ambapo Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala anasema:
وَاعْلَمُواْ أَنَّمَا غَنِمْتُم مِّن شَيْءٍ فَأَنَّ لِلَّهِ خُمُسَهُ وَلِلرَّسُولِ وَلِذِي الْقُرْبَى وَالْيَتَامَى وَالْمَسَاكِينِ وَابْنِ السَّبِيلِ إِن كُنتُمْ آمَنتُمْ بِاللَّهِ وَمَا أَنزَلْنَا عَلَى عَبْدِنَا يَوْمَ الْفُرْقَانِ يَوْمَ الْتَقَى الْجَمْعَانِ وَاللَّهُ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ
Na jueni ya kwamba chochote mlichopata ngawira, basi khums yake (sehemu moja katika tano) ni ya Mwenyezi Mungu na Mtume, na jamaa, na mayatima, na masikini, na msafiri, ikiwa nyinyi mmemwamini Mwenyezi Mungu na tuliyoyateremsha kwa mja wetu siku ya upambanuzi, siku yalipokutana majeshi mawili. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
Ni wazi kutokana na aya hii tukufu kwamba kimsingi na katika hatua ya kwanza khumsi ambayo ni katika ibada za kifedha na kimali ni haki ya Mwenyezi Mungu. Ameijalia haki hii yaani ngawira kuwa mali yake na ya Mtume wake na vilevile ya wale aliowajaalia kuwa makhalifa wa Mtume (saw), yaani Maimamu ambao ndio mfano wa pekee wa jamaa na watu wa karibu ya Mtume (saw). Imepokelewa katika kitabu cha Usuul al-Kafi katika kufasiri maana ya ’Dhawil Qurba’ yaani watu wa karibu ya Mtume (saw) katika aya tuliyosoma kwamba wao ni Imam Ali na Maimamu wengine wa Nyumba ya Mtume (as). Naye Imam Baqir (as) amesema: ‘Wao ni jamaa wa Mtume (saw) na Khumsi ni ya Mwenyezi Mungu na Mtume (saw) na Sisi.’
Na Imam Ali ar-Ridha (as) aliulizwa hivi katika kitabu hicho hicho cha al-Kafi maana ya aya hiyo tukufu: ‘Je, khumsi ya Mwenyezi Mungu ni ya nani?’ Akajibu (as) kwa kusema: ‘Ni ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) na ya Mtume ni ya Imam.’
Ndugu wasikilizaji, wanazuoni na maulamaa wameandika kwa mapana na marefu kuhusiana na haki hii katika utafiti wao na tafsiri ya aya hii, kwa kutegemea hadithi sahihi na za kuaminika kutoka madhehebu zote mbili za Kiislamu. Katika utafiti huo wameweza kuthibitisha kwamba haki ya khumsi ni ya Ahlul Beit wa Mtume (saw) kama amabvyo wanazuoni na wasomi wa Ahlu Bait yaani Shia wameweza kuchambua na kubainisha kwa kina sheria maalumu zinazohusiana na haki hii ambayo hutolewa kwenye mali iliyozidi matumizi ya kila mwaka ya mahitaji ya mtu. Ziada hii ya mapato na matumizi anayoyahitaji Mwislamu katika kipindi cha mwaka mzima hutolewa kimsingi na katika hatua ya kwaza kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kisha Mtume na Maimamu wa Nyumba yake toharifu (saw). Tunaweza kuvirejea vitabu vya fiqhi ili kupata kujua kwa kina sheria zinazohusiana na utekelezwaji wa haki hii kati ya haki za Ahlul Beit wa Mtume (saw).
Tutatosheka hapa kwa kutaja sehemu ndogo tu ya hekima ya Mwenyezi Mungu katika kuwajibisha haki hii ya kifedha katika mali za waja wake na kuwalazimu kuitoa kwa ajili ya Mtume na Ahlu Beit wake (as). Jambo tunalojifunza kutokana na maandiko matakatifu ni kwamba falsafa na hekima ya Mwenyezi Mungu katika kuwajibisha haki ya khumsi kwa waja wake ni kubuni njia ya kheri kwa maslahi ya waja hao kwa kuifikisha haki hiyo kwa walinda-amana maasumu (as) ili wapate kuitumia kwa maslahi ya dini ya Mwenyezi Mungu na kuwafikishia kheri waja wake. Sira na mwenendo wa maisha wa Ahlu Beit wa Mtume (as) unabainisha na kuthibitisha wazi kwamba wao ndio walio katika mstari wa mbele kabisa katika jamii nzima ya mwanadamu katika kutoa kwa njia ya Mwenyezi Mungu na wala hakuna mfano wao katika ukarimu, kujitolea na kuwahudumia wahitaji, hata wakati wao wenyewe wanapohitajia zaidi misadaa hiyo. Hii ni katika hali ambayo wao ndio walio na elimu na ujuzi zaidi kuhusiana na jinsi ya kutumiwa haki hiyo (khumsi) kwa njia inayofaa na ya kumrishisha Mwenyezi Mungu pamoja na maslahi kwa waja wake.
Hili ni jambo la kwanza. La pili ni kwamba kuharamishiwa watukufu hao maasumu (as) sadaka na kutengewa khumsi ni ishara ya kutukuzwa kwao na watu kufahamishwa nafasi maalumu na ya juu waliyonayo mbele ya Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala.
Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi chetu cha juma hili cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapokutana nanyi tena juma lijalo katika kipindi kingine cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain panapo majaaliwa, tunakutakieni nyote wakati mwema na kwaherini.