Mar 01, 2017 08:37 UTC
  • Wanasayansi Wairani waunda chombo erevu cha kupima kasi ya wanariadha

Disemba mwaka jana, Wanasayansi Wairani walifanikiwa kuunda chombo cha chronometer ambacho hupima kasi ya wanariadha. Chombo kilichoundwa na Wairani ni erevu na kinaondoa uwezekano wa kosa la mwanadamu katika kuainisha kasi ya mwanariadha.

Bi. Layla Hamza, mmoja kati ya wanasayansi wa mradi huo anasema lengo la utafiti wao ni kuunda chombo cha kielektroniki ambacho kinasajili muda aliotumia mwanariadha kukimbia kwa kutegemea tu chombo hicho cha kielektroniki na hivyo kuondoa uwezekano wa kosa wakati mwanadamu anaposajili rekodi hizo. Akifafanua zaidi Bi.Layla Hamza anasema: "Katika mradi huu wa utafiti tumejitahidi kuunda chombo cha kidijitali cha kupima kasi ya mwanaridha pasina kuhitajia msaada wa mwanadamu." Anaongeza kuwa chombo hicho kinajulikana kama Chronometer Erevu na inaweza kupima kasi ya mwanariadha aliyelengwa  na kuonesha matokeo hayo katika ubao wa kielektroniki.

Chronometer Erevu

 

Kwingineko Farhad Fuladinia, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Uhandisi wa Umeme katika Chuo Kikuu cha Kiviwanda cha Kermanshah magharibi mwa Iran amefanikiwa kutumia teknolojia ya mawasiliano ya simu za mkononi, GSM,   yaani Global System for Mobile Communications na kwa njia hiyo kuunganisha simu ya mkononi na ufunguo wa kielektroniki wa mlango. Mwanachuo huyo anasema kupitia njia aliyovumbua, mtumizi anaweza kudhibiti ufunguzi au ufungwaji wa mlango wa nyumba yake akiwa popote pale duniani na wakati wowote ule.

Kwa mujibu wa mifumo iliyopo duniani, mtumizi anaweza kutuma ujumbe mfupi kwa mfumo huo na kwa njia hiyo anaweza kufungua mlango. Lakini mfumo huu uliovumbuliwa na mwanasayansi Muirani unampa uwezo mtumizi kuzungumza na mtu aliye mlangoni na kubaini iwapo aruhusiwe au asiruhusiwe kuingia. Aliye mlangoni huruhusiwa kuingia kupitia nywila au paswadi ambayo hutumwa moja kwa moja kupitia ujumbe mfupi ambao huonekana katika chombo kilicho mlangoni. Mfumo unaotumika  wa mawasiliano ya pande mbili katika mradi huu wa kufungua mlango ukiwa masafa ya mbali hujulikana kama  SIM900.

Kwingineko duniani, hivi karibuni watafiti wa Chuo Kikuu cha  Warwick  nchini Uingereza waliunda chombo cha kielektroniki ambacho kinaweza kudhibiti mawimbi katika ubongo. Sensa zilizo katika headset za umeme huweza kusikiliza na kufuatilia mitikiso katika ubongo. Baada ya hapo mawimbi hutumwa katika kompyuta  na hivyo kumpa uwezo mwanadamu kuweza kudhibiti vitu mbali mbali vilivyounganishwa na kompyuta kama vile magari ya kuchezea, yaani toys, yanayoendeshwa kwa remote control.

Utafiti huu ulioongozwa na Profesa Christopher James unamaanisha kuwa, vidude vya watoto vya kuchezea kama vile magari na helikopta vinavyotumia remote control, roboti n.k vinaweza kudhibitiwa kupitia headset kwa kutumia nguvu za fikra katika ubongo.

Chombo chenye uwezo wa kudhibiti mawimbi ya ubongo

Shirika moja la Ujerumani linalojulikana kama Continental Automotive lenye makao yake mjini Hannover linapanga kuwasilisha vifaa kadhaa vya biometriki ambavyo mbali na kuifanya gari iwe erevu litaimarisha pia usalama.

Shirika hilo maarufu duniani limeunda starter ya gari ambayo inawasha gari kwa kutumia alama ya kidole. Kwa hivyo mtu anaweza kuwasha gari lake pasina kutumia ufunguo na kwa kutugemea tu alama ya kidole. Kwa msingi huo si tu kuwa wizi wa magari utakuwa mgumu zaidi bali hata pia watoto na vijana hawataweza kutumia gari pasina idhini ya mzazi au mwenye gari.

Hali kadhalika katika dashboard ya gari lenye kutumia mfumo huo wa kielektroniki kutakuwa na kamera yenye uwezo wa kubaini utambulisho wa mwenye kuendesha gari. Kwa hivyo kwa mfano hata kama mtu atalazimishwa kuweka alama yake ya kidole aliyechukua gari kwa nguvu hawezi kuliendesha kwani gari hilo huondoka kwa mujibu wa picha iliyoarifishwa katika mfumo wa kompyuta.  Mfumo huo erevu katika gari pia utakuwa na uwezo wa kutambua ni vituo vipi vya radio dereva anavipenda mbali na kudhibiti nyuzi joto ndani ya gari.

 

Na wahandisi wawili nchini Marekani wamewasilisha mpango wa kuunda gari maalumu la wasafiri katika uwanja wa ndege wa kimataifa. Gari hilo litakuwa na uwezo wa kupima uzito wa mizigo na pia kuchunguza pasi za wenye kusafiri kwa njia ya scanner.  Hali kadhalika gari hilo la kielektroniki lililopewa jina la Nexus mbali na kupima uzito wa mizigo linaweza pia kiuchunguza kwa mtazamo wa kiusalama isiwe na mada za milipuko na vitu vingine vilivyopigwa marufuku. Gari hilo ambalo halitegemei dereva lina uwezo wa kubeba watu wanne na pembeni mwa kila kitu kina chombo chenye scanner ya kuchunguza pasipoti. Gari hilo pia lina uwezo wa kumchunguza msafiri mwili wake wote kwa kutumia scanner na hivyo kubainisha iwapo amebeba vitu vilivyopigwa marufuku au la. Baada  ya kukamilika awamu hiyo ya uchunguzi na ukaguzi, gari hilo huwapeleka wasafiri katika eneo ambalo linatajwa kuwa ni 'eneo salama' na baada ya hapo wasafiri wanaweza kuelekea ndani ya ndege moja kwa moja pasina kupitia milango ya kawaida ambayo husimamiwa na wanaadamu. Kwa hivyo katika siku za usoni wasafiri watakuwa wakifika katika uwanja wa ndege na kuiniga katika gari hilo na baada ya ukaguzi watafikishwa karibu na eneo la kupanda ndege na kuelekea katika safari zao.

Gari erevu la kuchunguza mizigo na wasafiri wa ndege

Wapenzi wasikilizaji kwa habari hiyo kuhusu gari la Nexus ndio tunafika mwisho wa makala yetu ya mafanikio katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia, hadi wakati mwingine panapo majaliwa yake Mola, kwaherini.