Mar 14, 2017 08:26 UTC
  • Jumanne Machi 14, 2017

Leo ni Jumanne tarehe 15 Jamadithani 1438 Hijria sawa na Machi 14, 2017.

Siku kama ya leo miaka 1402 iliyopita yaani tarehe 15 Jumadi Thani mwaka 36 Hijria, kwa mujibu wa baadhi ya wanahistoria, vilianza vita vya Jamal, baina ya jeshi la Imam Ali bin Abi Twalib (as) na kundi la waasi waliozusha vurugu na fitina. Katika vita hivyo, jeshi la Kiislamu lililishinda kundi hilo ambalo lilianzisha uasi baada ya kushindwa kustahamili uadilifu wa Imam Ali, na hivyo kuamua kuvunja baia na kiapo chao cha utiifu. Viongozi wa kundi hilo ambalo lilijulikana kwa jina la Nakithina yaani wavunja ahadi, walikuwa Twalha na Zubair, ambapo waliamua kukusanya jeshi kubwa na kulichochea kwa matarajio ya kufikia malengo batili ya kutaka kutwaa utawala kwa nguvu.

Vita vya Jamal

Tarehe 15 Jumadi Thani mwaka 771 katika siku kama ya leo miaka 666 iliyopita, alifariki dunia Muhammad bin Hassan Hilli, maarufu kwa jina la 'Fakhrul Muhaqqiqiin', faqihi na msomi mkubwa wa Kiislamu. Mwanachuoni huyo alizaliwa mwaka 682 Hijria na kupata elimu ya kidini kwa mzazi wake, Allamah Hilli na wanachuoni wengine wa zama zake. Fakhrul Muhaqqiqiin ameacha vitabu vingi na miongoni mwavyo ni Manbaul Asrar na Tahswilul Najah.

Katika siku kama ya leo miaka 138 iliyopita, alizaliwa nchini Ujerumani Albert Einstein, msomi mashuhuri wa fizikia na hisabati. Mnamo mwaka 1921 msomi huyo mahiri alipewa tuzo ya Nobel katika taaluma ya fizikia, baada ya kufanya juhudi kubwa za kiutafiti. Utafiti na nadharia za Einstein katika uwanja wa nyuklia zilikuwa na taathira kubwa duniani. Hata hivyo Einstein alisikitika sana baada ya kugundua kwamba, uchunguzi na utafiti wake umetumiwa na baadhi ya nchi kwa ajili ya kutengeneza silaha hatari za nyuklia. Albert Einstein alifariki dunia mwaka 1955.

Albert Einstein

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita yaani tarehe 14 Machi 1978, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilianza kuivamia na kuikalia kwa mabavu ardhi ya Lebanon kwa kisingizio cha kukabiliana na operesheni iliyofanywa na wanamapambano wa Kipalestina pambizoni mwa Tel Aviv. Katika mashambulio hayo jeshi la Israel liliua raia wengi wasio na hatia wa Lebanon na Palestina na kuikalia kwa mabavu sehemu ya ardhi ya Lebanon. Hata hivyo utawala huo ghasibu uliondoka kwa fedheha katika maeneo ya kusini mwa Lebanon mwaka 2000 baada ya kupata kipigo kikali kutoka kwa wanamapambano shupavu wa Harakati ya mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah na kuondoka kwenye eneo hilo.

Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita uchaguzi wa Majlisi ya kwanza ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la kwanza la Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ulifanyika hapa nchini na hivyo kutimiza moja ya malengo ya mapinduzi hayo. Kwa sasa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran ina wawakilishi 290 ambao huhudumu bungeni kwa kipindi cha miaka 4. Wafuasi wa dini za waliowachache nchini Iran kama Wakristo na Wayahudi pia kwa uchache huwa na mwakilishi mmoja katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu.Bunge la Iran hutunga sheria zinazohusiana na masuala ya umma kwa sharti kwamba zisipingane na sharia za Kiislamu. Kazi nyingine muhimu ya Bunge hilo ni kuwasaili, kuwapasisha au kuwauzulu mawaziri wa serikali.